Lived Experiences / Maisha ya kila siku

Unapopitia magumu… (Sehemu ya Pili).

Reading Time: 3 minutes
Zaburi 121:1

Hello, karibu kwenye sehemu ya pili, unaweza kusomasehemu ya kwanza HAPA

Leo namalizia na vitu ambavyo vimeweza kunisaidia kuyapitia magumu

Naomba niseme kwa vyovyote vile Mungu ndiye anayetuvusha salama katika hali zozote tunazozipitia ila hivi vitu vunatusaidia kuwa na uelewa lakini pia tabia za kiushindi hata kama tunapitia magumu.
Kwa leo nitapenda kumalizia na:

 • Usisahau kuandika vile vitu unavyovipitia na vitu unavyoviombea: Hii inanguvu sana ya kukuonyesha ni wapi umetoka na ni wapi Bwana amekupeleka, hata siku nyingine unapopitia tatizo na kusoma tena utakuja kuona ni jinsi gani na ni wapi Bwana alikuvusha.
 • Uwe unatamka na kujikumbusha mambo unayo mshukuru Mungu kwayo: Katika kipindi kigumu jikumbushe na umshukuru Mungu sana. Najua ni rahisi kuangalia tatizo lako kwa muda wote,lakini jaribu kutoa macho yako kwenye tatizo lako na uanze kumshukuru Mungu kwa mambo mbalimbali yanayotokea katika maisha yako, hata nafasi ya kuiona siku nyingine ni jambo la kumshukuru Mungu kwalo.
 • Nenda kawatie moyo wengine: Hakuna muda mzuri unaoweza kumtia mtu moyo kama unapopitia magumu, kwani kwa kufanya hivyo unaongeza imani yako pia, lakini zaidi ya hivyo unaonyesha kwamba unaamini mambo chanya katika maisha yako. Lakini pia unajikumbusha yale Mungu aliokuvusha na kumkumbusha mwengine kwamba yeye pia atavuka. Tusijijengee tabia ya kukaa ndani wakati tunapitia magumu, nyanyuka ongea na watu, watie moyo,washauri, kwa maana ukiona tatizo la mwengine lako halitakuwa kubwa tena. Lakini je ni mtu gani anayeelewa tatizo vizuri zaidi ya yule aliye kwenye tatizo pia? Kwahiyo nenda. Sijasema uende ukalalamike au kuzungumza mambo hasi bali nenda mkatiane moyo na ukawatie watu moyo wenye matatizo, huku ukiamini Mungu yu kazini.
 • Fuatilia kwa undani tatizo lako: Mara nyingi vitu vinavyotutisha ni vile tusivyovijua kwa undani, na huwa hatujavifuatilia sana kiundani. Jaribu kufuatilia kwa undani tatizo lako likoje, usiogope tu kuwa kwakuwa una UKIMWI utakufa, je umefuatilia kwa undani UKIMWI ukoje, na walionao wanaishije? Huo ni mfano tu ambao unaweza ukatumika katka hali yoyote unayoipitia jaribu kuangalia kwa undani imekaaje, kabla haujakata tamaa,kuogopa na kuvunjika moyo.
 • Kaa mbali na watu wanaosema maneno hasi: Jamani kwenye kinywa kuna nguvu ya mauti na uzima, angalia sana unachotamka ila pia angalia unachotamkiwa. Katika kipindi hiki kaa mbali sana na watu wanaoongelea kushindwa katika tatizo lako, kwani kama vile ukivaa ukapendeza na mtu akakusifia moyo wako na kujiamini kwako huwa kunaongezeka, ndivyo ilivyo kwa tatizo kipewa maneno hasi, imani yako inashuka.
 • Washirikishe watu wako wa karibu: Ukiwa na tatizo usikae nalo ndani peke yako, washirikishe watu wako wa karibu, ipo nguvu inayopatikana kwa kuwashirikisha wengine na kuona kuwa hauko peke yako unaepigana, ipo nguvu katika kuwa na watu wawili au watatu pamoja nawewe katika hilo swala unalopitia. Usife peke yako, wala usichukue maamuzi magumu wakati haujawashirikisha watu. Unaweza kukuta kumbe tatizo hilo kuna mwingine alishapitia au halikuwa tatizo la wewe kuchukua maamuzi magumu kiasi hicho.
 • Sikiliza mahubiri : Mahubiri yanatia moyo kama jinsi shuhuda zilivyo, kipindi hiki jitahidi uende kanisani kwani Mungu huzungumza nasi pia kwa vinywa vya watumishi wake. Hata kama haujisikii kuamini yanayohubiriwa lakini kitendo cha kutamkiwa tu Neno linafanya kazi katika maisha yako.
 • Jikumbushe Baba yako ni nani (Priscilla Shirer): Mhubiri Priscilla Shirer anasema ukipitia mataizo jikumbushe Baba yako ni nani, unajua hii ni kweli, kama tungekuwa tunaishi kama watoto wa Mfalme ambaye kweli ndio Baba yetu, tungekuwa tunapitia matatizo tofauti kidogo na watu wasiojua kuwa Baba yetu ni mfalme.Mtoto wa mfalme hana wasiwasi wa Baba yake kulipa madeni kwa maana anajua fedha na dhahabu ni mali yake, anajua Bba yake ni mponyaji na vitu vingine vingi. Baba yetu ni mkuu sana, mwaminifu na mwenye uweza. Tujikumbushe hilo.
 • Napenda kujua pia vitu unavyovifanya ukipitia magumu, lakini pia usisahau kuomba bila kukoma. Neno linasema” Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”- Yeremia 29:11, na hili nalo ni kweli hata unapopitia magumu,Yeyey bado anakuwazia mema, na katika hilohilo jaribu atafanya mlango wa kutokea kwa maana njia zake si kama zetu, na inapendeza sana mapenzi yake yakitimizwa kwetu.

  Eunice

  Share Your Thoughts With Me