Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku

Mambo 27 niliyojifunza kwenye miaka yangu 27 ya kuishi

Leo ni kumbukumbu ya siku yangu ya kuzaliwa, leo nimetimiza miaka 27. Hata siamini kuwa nimeishi duniani kwa miaka 27, na pia nina furaha sana ya kuwa hai kuuona mwaka huu wa 27 maana najua kuishi, kuwa hai ni zawadi. Kwenye makala hii naenda kukushirikisha mambo 27 niliyojifunza kwenye miaka yangu 27, nimechagua kuandika mambo 27 kwasababu ya umri mpya nilioutimiza…

1. Unapopitia wakati mgumu, jua kuwa haudumu

2. Mabaya yanaumiza sana, yana tuacha na vidonda ndio maana tunayakumbuka kiurahisi kuliko mazuri

3. Unapopitia mazuri na kuwa na furaha, jitahidi kutofikiria mabaya, jitahidi kufurahia kwa asilimia 100 kama vile unavyohuzunikaga kwa asilimia 100 ukipitia mabaya

4. Hivyo ulivyo sasa, sivyo utakavyokuwa kesho. Ila hayo mabadiliko yanahitaji nguvu zako na mabadiliko yako ya jinsi unavyoona mambo. Wekeza kwenye kesho yako

5. Ndoto zako unazozifikiria zinaweza kutimia, ila unahitaji kujitoa, kuamini na kuzifanyia kazi kila siku hata kama kwa wakati huo zinaonekana zipo mbali

6. Ukiwa na hasira jitahidi kutulia kabla haujasema vitu utakavyovijutia au kuumiza wale unaowapenda au haujafanya maamuzi utakayoyajutia ukipoa

7. Jifunze kufikiria mwenyewe kwenye kila jambo, usipende kufuata mkumbo, maisha ni yako

8. Jifunze kujisikiliza, sikiliza sauti yako ya ndani

9. Hata kama dunia nzima ina vita, jitahidi kutengeneza dunia yako binafsi yenye amani, furaha na upendo

10. Kwenye maisha tunaumizwa na vitu mbalimbali tunavyopitia, jitahidi kupona, jitahidi kutafuta uponyaji wa moyo ili usijiumize wewe na usiwaumize wengine, ili uishi maisha vizuri

11. Samehe waliokukosea, jisamehe na wewe kwa makosa unayoyajua uliwafanyia watu au ulijikosea mwenyewe

Bonyeza Haka Kusoma Makala Hii : Jinsi ya kujisamehe

12. Jitahidi kujiongelesha maneno chanya, tunajiongelesha sana kimoyomoyo kuliko tunavyoongea na wengine, jiongeleshe maneno mazuri, iinakujenga

13. Maisha ni kuishi, ishi, furahia kuwa hai, pumzika, furahia chakula, furahia kuwa na marafiki, furahia kuwa hai, maisha ni mafupi, tengeneza kumbukumbu nzuri, ishi

14. Tafuta kuwa na marafiki wa kweli, sio lazima mfikirie vitu sawa, ila wawe na upendo wa kweli kako. Si lazima wawe wengi, ila wawe bora.

15. Usitumie watu kwenye maisha, ishi kiukweli lakini pia ishi na watu vile ungependa watu waishi na na wewe

16. Tafuta namna na ujasiri wa kujiondoa sehemu zinazokudhuru, usiishi halafu ukaja kujuta au kulalamika baadae

17. Usijilinganishe na wengine, jifunze kufurahia ulichonacho na maisha yako

18. Unaweza kubadilika. Maisha yana nafasi ya pili kwa kila mmoja kuishi mabadiliko anayoyataka. Hata kama unahisi wewe ni mlevi utakuwa kwa pombe, ukiamua kubadilika unaweza.

19. Ukichagua njia ya kupita kwenye maisha yako (kazi fulani, mume/mke nk), utakutana na mazuri na mabaya, jitahidi kufurahia njia uliyochagua, na punguza kuwaza maisha yako yangekuwaje usingechagua hiyo njia, jitahidi pia kuvumilia magumu ya hiyo njia na kufurahia mazuri yanayokujia

20. Punguza kulalamika sana kwenye maisha. Punguza kujiona wewe ni mwathirika wa kila linalotokea, badilisha mtazamo wa vile unavyojiona

21. Usisahau kufanya vitu vinavyokupa furaha. Tunapokuwa watu wazima tunaachaga ule ‘utoto’ na ndio maana tunapotezaga hata furaha kwenye maisha.

22. Ishi maisha yenye maana, maisha ambayo wewe mwenyewe unayapenda na unajivunia kuishi. Ishi maisha yako

23. Jitahidi kuishi upekee wako, watu wengi ni kopi ya Diamond anavyovaa, anavyotembea, anavyoongea, ishi uhalisia wako. Usijibadilishe ili ukubalike au upendwe, tafuta watu kukupenda vile ulivyo. Usivae kitu fulani kisa fulani kavaa, au kafanya, fanya yale uyatakayo wewe kwenye maisha yako bila presha au maigizo

24. Maisha ni mabadiliko, kukua ni kubadilika. Kubali kubadilika, kuwa mepesi kukubali mabadiliko. Usiogope hatua mpya, usiogope mabadiliko.

25. Kuwa mwepesi kukubali na kuishi katika hali yoyote ile. Huwa tunaumia sana kwasababu ya kutokukubali

26. Wakati hupotea haraka sana, jitahidi kuishi katika wakati uliopo, kama upo harusini, kuwepo harusini, usiwe Twitter, muda kidogo tu harusi itakuwa imeisha na huo wakati utakuwa umepita. Nimeona mara kadhaa tunaenda sehemu ili kupiga picha na kuondoka, jitahidi kufurahia kuwepo pale maana ukiondoka hapo wakati wa kuwa hapo unakuwa umepita na unaweza usirudi tena sehemu hiyo kwenye maisha yako. Ishi kama vile haujui unakufa lini, kwasababu ni kweli haujui. Ishi kama ndio siku yako ya mwisho duniani, kwasababu ni kweli inaweza kuwa.

27. Watu wanaokuzunguka wana mchango mkubwa sana na ubora wa maisha unayoishi / utakayoishi. Unaweza kuishi na watu wanaoinua nafsi yako, wanaokupa furaha, kukusukuma kuwa bora, kukusaidia kukua/kupona au kuacha tabia fulani mbaya na kuja kuwa mtu ambaye wewe unajivunia. Unaweza kuishi au kuzungukwa na watu wanoua nafsi yako, kipaji nk, watakaokuumiza, kukushusha hata kushindwa kujiamini, kukufanya ukose furaha. Ili kuishi maisha bora jitahidi kuzungukwa na watu wazuri kwako, wanaokusukuma kuwa bora, wanaokuamini, wanaoinua nafsi yako.

La mwisho ni jitafute, tumia muda wako kujitambua, kujua ni lipi unapenda kwenye maisha, lipi unaamini, kipi unapenda kufanya nk. Jitafute

Na hayo ndio mambo niliyojifunza, niambie kwenye comment una umri gani na ni mambo gani umejifunza kwenye maisha?

One Comment

 • Ismail

  Nina umri wa miaka 22 sasa na nimehitimu kidato cha sita nwaka huu na kipindi nasoma niliweza jupitia changamoto nyingi sana na hiyo inatijana na sababu ya kwamba tabia ya maisha yangu ni kwamba mimi si mtu muongeaji sana na si mtu ninaye penda kutaniana na watu ambao sina mazoea nao.
  Hivyokutokana na hilo baadhi ya wanafunzi niliyokuwa nikisoma nao walikuwa hawapendi sana ninapokuwa nao ninapokaa kimya nikiwasijiliza wanacho kiongelea ama na hawakupenda kunishirikisha yale waliyokuwa waki yafikia maamuzi endapo ikitokea mimi sikuwepo katika mazingira hayo..
  Sikujuwa ni kwa nini walikuwa wakifanya vile ,ila nimekuja kugundua kwamba walikuwa wananiogopa kuongea na mimi ila tu pale ninapo anzisha mazungumzo nawao.
  Mazoea ya wao kuongea na mimi yamekuja kuanza pale tu ambapo tumefanya mahafari ya kidato cha sita na nika kabidhiwa cheti cha nidhamu maisha yangu yakawa vizuri sana pamoja na wao .
  Hivyo nikagundua kwamba watu hupenda kuishi na watu wanao endana kwa tabia yao na endapo ikitokea mtu katika mazingira yao yupo katika tabia tofauti na wao huonekana ni mtu mwrnye kujitenga sana na mwenye kujiona sana pia ni mwenye upekee…

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป