Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku

Kwa mwanaume anayewaita ita wanawake barabarani

‘Embu cheka, ukinuna sura inakuwa mbaya’

‘ Oya suruali nyekundu’

‘ Una shepu nzuri sana’

Na maneno mengine ambayo siwezi kuandika hapa.

Ukimuuliza mwanamke kitu kikubwa anachokiogopa kwenye maisha, atakuambia kubakwa. Kingine ni kutembea sehemu ambapo kuna wanaume wengi wamekaa. Mwanamke yuko radhi abadilishe njia, au ‘ajitoe ufahamu’ ili kupita mbele ya wanaume wengi.

Sababu kubwa ni kuwa watamwita, na sio kiheshima. Watamwita kwa maneno ambayo yanamfanya ajisikie kama chombo ambacho kiko kwaajili ya kukaguliwa nao, watamgawanya wanavyotaka haswa kwa maneno yanayoashiria mwanamke yupo pale kwaajili ya kufanya naye mapenzi au kuanzisha mahusiano, na akiwa hawajibu au hama muda nao, watamtukana.

‘Muone kwanza mbaya’

‘Muone kwanza hiki na kile’

Kiufupi ni kama vile umejiaminisha kila mwanamke ni mali yako ambayo wewe unapaswa kuimiliki isipotaka unaivunja.

Kiufupi ni kama vile unapata bichwa kwa kumdhalilisha mwanamke.

Kiufupi unadhani mwanamke anawajibu wa kukupa attention kila ulipo asipokupa unaificha aibu yako kwa kumponda yeye.

Kiufupi unaishi kwenye dunia ambayo inafurahia wewe kujisikia vizuri kutokana na yale ambayo unamfanyia mwanamke, haijalishi mazuri au mabaya. Na ndio maana wengine wanapongezwa hata kwa kumbaka mwanamke kwasababu aliwaonesha dharau.

Hakuna kitu nachukia kama kuitwa itwa barabarani, huwa natembea na earphone kwasababu hiyo.

Lakini maisha hayakutakiwa yawe hivyo, sikutakiwa kuangaliwa kwa tamaa kila ninapopita, sikutakiwa kuonekana kama chombo cha kufanyia ngono.

Kwa wanaume mnaowaita ita wanawake barabarani, mnanifanya nijisikie vibaya, hata kwenda dukani tu naenda nikiwaza jambo kama hili ambalo unaweza kuliacha.

Nikuulize swali, kwanini unaniita?

Haunijui.

Unajua siwezi kusimama.

Hauna lengo la kunifahamu mimi kama mimi.

Sikujui.

Kwanini unaniita.

Kwanini unadhani nina muda wa kusikia sauti yako na maneno yako ambayo yananifanya nijisikie vibaya?

Kwanini unadhani napenda kuyasikia?

Kama haujui sipendi kuyasikia, nataka tu niende dukani kwa amani nirudi nyumbani, nataka niende mjini bila kuambiwa na mtu nisiyemjua kuwa nisinune.

Kwa mwanaume anayeita ita wanawake barabarani ningependa ujiulize kwanini unafanya hivyo, unapata nini?

Na kama unafanya hivyo ili marafiki zako wakuone mwenzao, badilisha marafiki, hao hawakushauri kufanya lolote zuri.

Kama unafanya ili ujisikie mwanaume uliyekamilika, badilisha maana yako ya uanaume. Kama ili ujisikie mwanaume ni lazima umshushe mwanamke chini, uanaume wako hauna thamani, hauna nguvu.

Mwanaume mwenye nguvu ni yule anayewainua wote waliopo kwenye maisha yake. Sio kuwashusha.

Unayomfanyia mtu usiyemjua, bila kujua kuwa huyo ni dada wa mtu, mpenzi wa mtu, mama wa mtu, huyo ni binadamu anayestahili heshima, ndio hayo hayo anayofanyiwa mama yako, mpenzi wako, dada yako na atakayofanyiwa mwanao maana na wenzio pia hawawaheshimu wanawake unaowaheshimu na kuwathamini wewe.

Heshimu wanawake kwasababu ni binadamu wenzio wanaostahili heshima.

Kwa mwanaume anayewaita ita wanawake barabarani, badilika. Jiheshimu, heshimu wanawake.

Eunice

3 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป