Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku

Kudharauliana kutaisha lini?

Leo nilikuwa nakula mahali, akaja Dada mmoja akawa anaongea na wakaka (nahisi wanajuana au wanafanya kazi pamoja). Alipoondoka walichukua muda kuigiza vile alivyokuwa anaongea ( kutokana na sifa ya kabila lake), walichukua muda mrefu kweli. Kiasi kwamba mazungumzo yao na vilivyokuwa vinawachekesha ni kuhusu kabila la yule mdada walivyo, na jinsi yule mdada anavyofanya kila kitu cha kabila lao (kuongea nk).

Hiki hakikunishangaza, kilinifanya niwaonee huruma. Maana kama hawakuwa na chakusema zaidi ya yule mdada (kwa muda wote ule) na kabila lake, inamaana maisha yao hayako na vitu vya kuvutia zaidi ya kuwasema wengine..

Kilichonigusa, ni pale yule mkaka aliposema kuwa kabila la yule mdada wanawadharau kabila lingine kutoka mkoa mwingine, na hilo kabila lingine kwenye huohuo mkoa linawadharau kabila la yule mdada kwenye mkoa mmoja.

Hapo ndipo nikawaza, hivi kudharauliana kutaisha lini?

Sio tu kikabila, na kuona kabila lingine kuwa halifai nk ( ingawa wengine hufanya kama matani, lakini huwezi jua mpokeaji anachukuliaje).. Naongelea kwenye maisha kwa ujumla..

-Mwenye Mali kumdharau asiye na Mali kwa mfano..

Au

– Aliyesoma kumdharau asiyesoma

– Mwenye akili darasani, kumdharau asiye na akili darasani
– Watu wote wanaowadharau walinzi

Au hata mweupe kumdharau mweusi..

Au aina mbalimbali za dharau ( kuwaangalia watu chini) tunazooneshana kwenye maisha, nilizowahi kuzionesha, au nilizooneshwa na watu.

Dharau.

Nahisi ukiwa nayo, unakuwa ni wale watu wanaodhani wao ndio wenye dunia, wao ndio wenye kumiliki kifo, wao ndio watabaki walivyo mpaka mwisho wa dunia, wao ndio wanajua mwanzo hadi mwisho, wao ndio wema, wanaostahili, wakuheshimiwa na wengine wote takataka.

Nahisi kuna muda vitu hutufanya tusahau, kuwa sisi tulizaliwa uchi, sisi ni udongo, sisi ni binadamu, tunaokosea, tunaokosewa pia.

Sisi si Mungu, na hata mipango yetu tunayoipanga mara nyingi haitokei kama vile tulivyopanga.

Sasa kwanini tunamdharau mwingine? Udongo mwenzetu?

Kwanini tunamuona mtu aliyeumbwa kwa udongo na Mungu kama sisi pia kuwa hafai, mtu ambaye Mungu alichukua muda wake kumuumba, kwasababu tu kazaliwa tofauti na sisi?

Kwanini utofauti wetu usitufanye kumshukuru Mungu zaidi nakuona jinsi alivyo mbunifu, badala ya kuchukiana na kuanza kujiweka juu zaidi ya wengine?

Ukiwa juu na ukawadharau wachini, unafaidika nini?

Wakati wote ni udongo, ambao Mungu akiamua kuchukua pumzi yake, tunarudi kuwa udongo?

Naamini tukishajua maisha ni kusaidiana, nakuhitaji kama vile unavyonihitaji..

Wote ni udongo, na Mungu anatuthamini wote kwa usawa, na mbele zake hakuna aliye bora, alimtuma mwanae afe kwaajili ya wote, labda tutaamza kumthamini kila mtu, sawa.

Aliye vaa suti, na ambaye ana matatizo ya akili mtaani kwetu, Mungu anatuona sote sawa.

Labda muda umefika nasisi kuwapenda wenzetu kama tunavyojipenda, kuwaonea huruma kama vile Mungu anavyotuonea huruma.. Kujua sote ni udongo, wote ni sawa.

Utofauti wetu, usitufanye kudharauliana.. Ila utusaidie kumuona kila mmoja wetu kama wa pekee sana, maana ndivyo tulivyo.

Eunice

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป