Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku

Mawazo ya Jumatano : Mwisho wa siku furaha yako ni kazi yako kujipa

Hivi karibuni nimeingia kwenye mahusiano na kijana mmoja mwema sana. Kwenye dunia hii yenye watu wa aina mbalimbali kijana huyu namuona ni kati ya wale waliofanikiwa kubakiwa na utu wema ambao watoto wengi huwa nao na huupoteza wanavyokuwa, ila naona yeye bado yuko vile vile na roho, na upendo na kuangalia maisha katika jicho la wema.

Kijana huyu anajitahidi, sana. Anajitahidi kufanya mema. Anajitahidi tuwe kwenye mahusiano yenye furaha na amani. Na mimi nafurahi kuwa naye, namuona ni baraka kwenye maisha yangu. Ila katika muda wote ambao tumekuwa kwenye mahusiano nimejifunza mambo mengi na la muhimu ambalo nimejifunza ni kuwa maisha yangu ni wajibu wangu, mwisho wa siku furaha ya moyo ni kazi yangu kujipa.

Bonyeza hapa kusoma : Mambo 5 yatakayokusaidia kudili na watu wagumu

Haimaanishi kuwa mkiwa kwenye mahusiano hauna wajibu wa kuwa amani na furaha ya mwenzio, ila namaanisha kuwa hata kama mtu atajitahidi sana kuwa amani na furaha yako, kama moyoni huna furaha, umejawa na maumivu nk hakuna namna utaona furaha kwenye yanayoendelea, cha zaidi ni utamtesa huyo mtu kuenda mbele na nyuma kufanya yote kukuletea furaha ambayo wewe mwenyewe umeshindwa kuitafuta na kujipa moyoni.

Ushawahi kutana na watu ambao kila unachofanya kwao hakuna jema? hautaga weza kuwapa furaha? basi ujue hao moyoni kwao kuna shida, lakini pia wanahisi ni kazi ya watu wengine kufanya a, e, i, o, u ili wao wawe na furaha. Ila ukweli ni kuwa unaweza ukaishi kiasi kwamba unafuraha moyoni hata yanayoendelea yakawa hayakusumbui kwasababu umeamua kujipa furaha na kuona dunia na maisha katika hali chanya. Na duniani kuna watu wawili, wale wenye furaha moyoni, na wale wanaosubiria wengine wawafurahishe. Hao kundi la pili ni watu wanaochosha kuishi nao, kwasababu wameacha kuwajibika kuhusu furaha na amani zao na wanawapa watu wa nje mzigo, kwa kazi ambayo wangefanya wenyewe.

Unaweza kuwa mtu wa kundi la pili, kwa kushindwa kusamehe, kwa kuchukia chukia kila linaloendelea, kwa kuwa mtu mwenye mawazo hasi kwa kila linalotokea, kwa kuiangalia dunia katika hali hasi kila saa, kwa kufikiria kuwa watu wanatakiwa wafanye mambo yanayokufurahisha muda wote na wapo kwenye maisha yako kwaajili ya kukufurahisha wakati ukweli ni kuwa watu tuna mambo mengi sana yanayoendelea na muda mwingine hawafikirii kuwa kila wanalofanya walifanye kwa kukuumiza au kukufurahisha, unaweza kuwa kwenye kundi la pili kwa kuwa umeumizwa na una uchungu moyoni kutokana na uliyopitia ambayo inabidi uyaachilie.

Bonyeza hapa kusoma : Mawazo ya Jumatano : Kila unayekutana naye ana tatizo lake analopitia

Kama wewe ni mmoja wa watu uliopo kundi la pili basi unaweza kubadilika kama utaamua kwa kujua kuwa una wajibu wa kujipa furaha mwenyewe, unawajibu wa kuona vitu katika hali chanya mwenyewe, unaweza kuanza taratibu kujitambua na kujua mambo gani yanakuletea furaha halafu ukiyajua uzidi kuyafanya, unaweza kuachilia na kusamehe unapokosewa, unaweza kujikumbusha kuwa duniani pia kuna mambo mengi chanya yanayotokea zaidi ya mambo mengine hasi yanayoendelea, unaweza kuwachukulia watu ulionao kwenye maisha kama watu ambao wewe pia una wajibu wa kuwafanyia mema bila kutegemea malipo nk.

Acha kulaumu dunia, kulaumu watu kwa kukosa furaha moyoni na maishani, furaha yako ni wajibu wako, maisha yako yapo mikononi mwako ni wajibu wako kuishi na kuenenda nayo vile unavyokubali na unavyoona yafaa, mwisho wa siku furaha yako ni kazi yako kujipa, kila mtu anayake yanayomuendea ikiwemo kujipa furaha wao. Haumdai mtu furaha na amani maishani. Badala ya kuondoka kwenye kila mahusiano kwa kuhisi wengine ndio wana shida, badala ya kuachana na kila rafiki au kumlalamikia kila unayekutana naye kuwa hawakufanyii mema, labda jaribu kujiangalia moyoni kama wewe mwenyewe unajipa furaha, wewe mwenyewe unafuraha na amani maishani/moyoni mwako mwako, usitegemee watu wakutendee yale usiyojitendea wewe mwenyewe, kukupa furaha ya kweli moyoni na maishani ni kazi yako.

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป