Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

man checking woman s temperature
Guest Post

Jinsi kutegemea wengine wakupende kunavyokukosesha furaha kwenye maisha

Watu wengi hawajui namna furaha inavyoathiri sehemu zote za maisha yao. Wengine husema watafurahi wakipata kazi, wengine husema watafurahi wakipata watoto, wengine husema watafurahi wakimaliza masomo, wengine husema watafurahi wakiwa na vyeo n.k lakini ukweli ni kuwa pesa, cheo, umaarufu, mali na kuhitimu masomo huwa hakuleti furaha inayodumu bali huleta furaha ya muda.

Furaha ya muda ni kama vile sherehe utafurahia sherehe lakini baada ya sherehe unabaki na huzuni. Furaha ya kweli inatokana na kutosheka mwenyewe kwa maisha yako.

Haina maana usitafute pesa, vyeo, mali, watoto, marafiki nk, hapana. Bali inamaanisha ufurahie kila hali inavyokuwa.

Katika malengo 10 watu hujiwekea 9 huwa hayatimii, na hilo moja halitimii kama wanavyopanga hivyo mwisho wa siku mtu hujiona wa kufeli. Watu wengi hawajui kuwa maisha huwa yanakuja tofauti na mipango yetu, hii ndiyo sababu wengi hawana furaha na wachache sana ndiyo wanaofurahia maisha yao.

Ikiwa umetambua kuwa katika malengo 10 unayoweka 9 huwa hayatimii kama unavyopanga maana yake kila siku unafanikiwa isipokuwa unafanikiwa tofauti na ulivyotarajia. Furaha yako inakwenda kuathiri maisha yako yote.

Ikija kwenye mahusiano sasa, mahusiano ambayo hayana maelewano mazuri huwa hayadumu. Hakuna mahusiano ya upande mmoja.

Kama kwenye urafiki, ndoa, biashara au mahusiano yoyote yale ni upande mmoja tu ndiyo unaofanya juhudi za kuhakikisha mahusiano yaanadumu yafuatayo hutokea :
– Lawama huongezeka

– Mtu mmoja anakuwa kero kwa mwengine mfano unatuma sms 10 hazijibiwi zote na unapiga simu hazipokelewi maana yake unamsumbua mtu ambaye hataki mawasiliano yako.

– Mmoja atateseka sana, hapati usingizi, hamu ya kula inaisha, uchovu, hamu ya kufanya kazi inatoweka, kuugua mara kwa mara, hasira za hapa na pale, kukwazana na kila mtu, kujichukia nk.

Ikiwa huna furaha kwa jambo lolote ni wazi utateseka sana.

Je unajipenda sana au umemwachia mwengine akupende? Huwezi kumpenda mtu kwa dhati ikiwa wewe hujipendi kwa dhati. Kama utaamua leo kuwa 100% ya furaha yako unajipa wewe hakuna mtu atakaekusumbua akili. Watu wengi hawajiamini kwa sababu hawajipendi. Huwezi kujiamini kama hujipendi.

Pia Soma : Jinsi ya kujiamini

Embu nikuulize swali hivi unapojitazama kwenye kioo ni fikra gani huwa zinakuja haraka? Unaona uzuri wa sura yako? Unaona ubaya wa sura yako? Unaona namna ambavyo pua yako huipendi? Namna ambavyo macho yako yamekaa vibaya? Namna ambavyo midomo yako imekaa vibaya? Namna ambayo kichwa chako kimekaa vibaya? Namna ambavyo rangi yako ni mbaya?

Pia Soma : Jinsi kuukubali mwili wangu ulivyo kulivyonifanya nijiamini na nijione mrembo

Ikiwa huwa unajitazama kwenye kioo kisha unaona dosari za sura yako tu ni wazi hujipendi. Kama kila wakati unawaza kuhusu ubaya wa sura yako na maumbile yako lazima utakuwa na hasira za kila wakati. Hasira za kila wakati zinakwenda kuathiri namna unavyofanya maamuzi. Hasira zako zinakwenda kuathiri usingizi wako, hasira zako zinakwenda kukuongezea maumivu makali, hasira zako zinakwenda kuvuruga mfumo wa homoni na kupelekea kitambi, hasira zako zinakwenda kukufanya uongezeke uzito, hasira zako zinakwenda kuathiri usingizi wako, hasira zako zinakwenda kuharibu kinga ya mwili. Watu wenye hasira hufa mapema sana kwa magonjwa ya moyo na mshtuko. Hasira inakwenda kufanya ubongo usiweze kudhibiti fikra zako badala yake hisia ndiyo zinakwenda kutawala maamuzi yako.

Amygdala ni sehemu ya ubongo ambayo hupokea hisia, hasira, vitu vinavyoleta hisia za kupigana ambapo sehemu hiyo ikiwa inafanya kazi sana kuzidi Prefrontal cortex huweza kumfanya mtu kuwa katili sana. Watu wachache sana huzaliwa wakiwa na huruma sana na wingi wa huruma ndiyo upendo wa dhati. Huwezi kujipenda kwa dhati ikiwa huna huruma kwako mwenyewe. Huwezi kumwonea mtu huruma ikiwa wewe mwenyewe huna huruma kwako mwenyewe. Huwezi kumjali mtu ikiwa hujijali mwenyewe.

Watu wenye kujipenda sana huwa hawana lawama.

Ukiona mtu kila siku anakutishia, anafoka, lawama kila wakati, hata umpe pesa nyingi kiasi gani hatoi shukurani, hata uombe msamaha kiasi gani hawezi kusamehe usijitese sana mtu huyo anatatizo kwenye akili. Akili inayoongozwa na fikra badala ya hisia huwa ipo sawia na mtu mwenye kuongozwa na akili badala ya hisia huwa anafanya maamuzi mazuri hasa nyakati ngumu sana.

man in red polo shirt smiling

Ikiwa mtu hawezi kudhibiti hisia zake kamwe hawezi kudhibiti tabia zake. Ni vigumu sana kujirekebisha tabia kama unaona huna makosa kila siku. Ikiwa unaona upo sahihi kwa kila jambo ni wazi unatatizo kubwa sana kwenye ubongo.  Kiburi huzuia mtu kuelewa, kiburi huanza kwenye kushindwa kudhibiti hasira. Watu wanaojua kuwa wanakosea huwa wepesi kuomba msamaha na huwa wepesi kusamehe makosa ya wengine. Ukiona mtu anakuchukia  tatizo lipo kwake si kwako ni vigumu mtu kukuchukia kama yeye anajipenda.

Pia Soma : Jinsi ya kusamehe

Huwezi kumtukana mtu ikiwa hujawahi kutukanwa maana yake huwezi kuongea lugha ya kigeni ikiwa hujawahi kusikia lugha hiyo mantiki yake ni kuwa watu hulipa kisasi kwa yake waliyofanyiwa. Mtu atakuwa jeuri kwa sababu alifanyiwa ujeuri utotoni. Mtu atakuwa hatimizi ahadi kwa sababu aliahidiwa hakutekelezewa ahadi. Mtu atakuwa mwenye wivu sana kwa sababu amezoea kuona wengine wakiwa na wivu. Mtu atajichukia kisha ataonyesha chuki hiyo kwa wengine. Mtu hawezi kukuchukia kama hajawahi kusikia taarifa zako mbaya au kukusema kwa ubaya hivyo usijichukie kisa watu wanakusema vibaya wengi huwasema wengine kwa ubaya kwa sababu wanajichukia wao wenyewe.

Watu hawaoni vitu kama vilivyo bali wanaona vitu kama wao walivyo. Ukiona mtu anakupenda ujue amefanya hivyo kwa sababu anajipenda ikiwa hajipendi hawezi kukupenda. Mtu akiwa anajichukia atakuonyesha chuki wewe. Watu wengi wanateseka kwa sababu ya chuki, wivu, hasira.

Huwezi kuwa na furaha wakati huwezi kusamehe waliokukosea. Huwezi kuwa na furaha wakati unamwonea wivu mwenzako. Huwezi kuwa na furaha wakati unajiona tabaka la chini.

Ukiwa na wivu sana huwezi kufurahia maisha yako kwa sababu utakuwa unataka mashindano na wengine. Ukipata pesa utahofia kama rafiki zako wamepata pesa kukuzidi na ikiwa wamepata pesa kukuzidi utajiona hujapiga hatua yoyote. Ikiwa unapitia kipindi kigumu na unatatizo la wivu ukipata taarifa kuwa rafiki yako maisha yake ni mazuri utazidi kujichukia na kujiona mwenye mikosi, fungu la kukosa.

Furaha haiwezi kukaa kwa mtu mwenye wivu, chuki, kisasi. Anza kujipenda wewe mwenyewe bila kutarajia pongezi, shukurani, kusifiwa nk. Hamasa kubwa sana inatokana moyoni mwako wala siyo kwa wengine. Ikiwa unategemea uambiwe unakipaji ndiyo ujue unakipaji huwezi kufanikiwa. Ikiwa unasubiri watu wakikutumia sms ndiyo ujue unapendwa utajichukia milele. Watu unaowategemea wakupe furaha huwezi kuwaona nyakati ngumu na wanaweza kuwepo ila wasifanye vile unataka wewe hivyo maumivu yatazidi kwako.

Jipende.


Imeandikwa na Mwanasaikolojia Said Kasege, Temeke, Dar es salaam. Mawasiliano : +255766862579, +255622414991

Share Your Thoughts With Me

Translate »