Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku

Kama unahisi umechelewa kwenye maisha…

Siwezi kukudanganya, hivi karibuni nimekuwa nikijisikia kama vile maisha yangu yanaenda taratibu sana, yani kama vile mambo sehemu nilipo natakiwa niwe mbele.Ni mchanganyiko wa wivu kwa vile naangalia vile wengine wako mbele halafu mimi niko nyuma ukilinganisha na wao, ukijumlisha na kujilinganisha na ukimalizia na kukosa furaha ya hapa nilipo.Najua kila mtu anaweza akapata hizi hisia, katika dunia tuliyopo ambapo thamani yetu inatokana na vitu tulivyovifanya, tulivyonavyo, sehemu tulizowahi kwenda na mambo mbalimbali ambayo tumefanikiwa, kuna muda ukijiangalia unaona haufikii kule, haufikii pale dunia au watu wanataka tufike, au haujafikia kiwango cha wewe kuonekana bora.

Inawezekana ukijiangalia kimahusiano unaona haufikii kule wengine wapo kimahusiano, kielimu, kimavazi au katika namna yoyote ambayo ukiangalia maisha yako unaona yako nyuma au yanaenda taratibu.

Labda ulipanga ukifika miaka fulani uwe umetimiza ndoto fulani au hata umeoa/umeolewa na mpaka sasa bado, na unahisi maisha yanaenda taratibu. Ukiangalia kila mtu anayekuzunguka yuko kwenye ndoa, na nyingine umetoka kusimamia au unatarajia kusimamia jumamosi ijayo, wengine wamepata elimu za juu kuliko wewe, hata kuwa tu na gari kabla yako.

Kiasi kwamba ukiangalia maisha yako unajiona kama huyu mtoto:

Hivyo ndivyo nilivyokuwa najisikia na kujiona.

Labda maisha hayakutakiwa yawe ni kwa haraka kiasi gani unafikia malengo, labda tunakosea, labda ilitakiwa iwe ni jinsi gani tunafurahia kila kitu tulichonacho wakati tunaelekea kwenye hayo malengo.

Labda kufikia malengo haikutakiwa kuwa mwisho wa maisha. Sasa hivi najiona niko nyuma kwasababu wengine wanafanya kazi mimi nasoma, baadae nikimaliza kusoma nitaona niko nyuma kwasababu sina gari wengine wanafanya kazi na wanamagari, yani sitokuja kumaliza kujiona niko nyuma ya watu.

Badala ya matukio ya maisha na vitu tunavyopata kwenye maisha kupima uthamani wangu, labda viliwekwa ili nivifurahie tu na nisiweke thamani yangu kwenye kuwa na hivyo vitu.

Ikiwa natumia vitu kujiona nina thamani basi nitasubiri mpaka niolewe ndo nijione wa thamani, nikimaliza hapo nitasubiri nipate watoto ili niwe na thamani tena, yani hayo mashindano hayataisha. Mimi nimeamua kufurahia maisha katika hali yoyote niliyopo.

SOMA:Kwa wasio na baba, kutoka kwa asiye na baba

Nimegundua kuwa Mungu anajua mahali nilipo, na tena ni mpango wake niwe kwenye stage hii sasa hivi. Ninaweza nikajiona niko nyuma, lakini Neno linasema anajua mwisho wangu (Isaya 46:10) na anampango na maisha yangu (Yeremia 29:11), hata hapa nilipo anapajua na ni mpango wake. Naamini hata kama nahisi maisha yanaenda taratibu Yeye ndo amepanga yawe hivyo, na kwavile kuishi ni Kristo, naomba niishi hii sehemu nilipo kwaajili ya utukufu wake.

Na Mungu kaniweka kabisa pale nilipo.

Ukiangalia sana sehemu ulipo na unaposhindwa kuridhika na kufurahi hapo, unapoteza nafasi ya kumtumikia Mungu ukiwa hapo lakini pia unapoteza zawadi au somo ambalo ungejifunza katika hiyo hatua ya maisha yako. Angalia katika mtazamo chanya, na jiambie vitu ambavyo ungemwambia aliyepo katika hiyo sehemu pia. Jipe neema utapita hiyo stage katika muda wa Mungu.

Kama wewe unahisi maisha yako yanaenda taratibu katika hali yoyote ambayo unaona uko nyuma, jikumbushe uko kwenye majira. Nakumbuka tulivyokuwa high school tulikuwa tunaenda shule na rafiki yangu siku moja na tukawa tunaongelea kuhusu kuwa na nyumba na magari, na tulikubaliana kwamba hayo yote tutayatimiza, na tutakuja kuwa nayo ila sio kwa wakati ule, kwasababu tulikuwa shule na tusingeweza maisha hayo kwa wakati ule.

Muda mwingine tuna haraka sana na kusahau kwamba kila jambo lina wakati wake, unataka nyumba, Mungu anajua unataka. Na zaidi ya hivyo anajua wakati bora wa wewe kuwa na hiyo nyumba, jikumbushe WAKATI. Kama unahitaji makubwa na mazuri, kusubiri inabidi kuwe karibu nawe. Kusubiri kuwe rafiki yako, sio kila jambo linabidi liende kwa pupa kwa kufuata presha yoyote ile, mambo mengi kwenye maisha yanahitaji utulivu na maamuzi yenye hekima sana.

Unajua kuna wakati mioyo hainaga vitu vizuri sana au inakuwa haiko mahali salama kimawazo, kuna muda tunatoa mawazo kwenye kitu cha muhimu na kuanza kuwaza vitu vingine, tunashindwa kujali tulivyonavyo na kuangalia tusivyonavyo, ndio wakati kama huu ambao mara nyingi tunajisikia tuko nyuma. Tukiacha kufikiria sana kuhusu maisha ya wengine tutaacha hata kujilinganisha, maana kujilinganisha ndio kunatupa hisia za kuona sisi tuko nyuma kuliko wengine.
Kama unajisikia uko nyuma kimaisha, nikutie moyo kwamba hautobaki hapo milele, miaka mitano ijayo hautakuwa sehemu hiyohiyo uliyopo sasa. Nikutie moyo mambo hubadilika, na vitu hubadilika, utafika kule unatamani kufika, lakini kwa muda ambao Mungu amepanga, subiri.
Eunice.

21 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป