Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku

Mawazo ya Jumatano : Kufeli kwenye maisha ndio kuishi

Likija kwenye swala la kufeli, mara nyingi linaonekana ni jambo la kudharauliwa, kuogopwa na kuepukwa. Lakini vipi kama tukichukulia kufeli kama sehemu ya kujaribu, kujifunza na kuishi?


Watu wengi tunaogopa sana kufeli, kiasi kwamba tunaogopa kuishi, tunaogopa sana kuwa wa kwanza kufanya jambo na kufeli kiasi kwamba hatujaribu, tunaogopa sana tukifeli watu watatufikiriaje kiasi kwamba tunajinyamazisha mbele za watu ili tusibadilishe vile wanavyotufikiria.

Nakumbuka nilivyokuwa chuo tulijifunza kuhusu aina za wajasiriamali, na aina moja wapo ilinifikirisha sana. Aina hii ni ya mjasiriamali anayeanzisha biashara halafu ikifika ukubwa fulani, anaiuza. Yani yeye anapata furaha ya kuanzisha vitu, kuvikuza kidogo na kuviuza. Yani ile inampa furaha sana, na kumsisimua moyo kiasi cha kuwa ni kitu anapenda kufanya kwenye biashara zake anazozianzisha. Nikawa nawaza huyu mtu inaonekana haogopi kufeli, au anachukulia kufeli kama sehemu ya kujaribu kiasi kwamba anaenda na kuanzisha vitu halafu anaviuza anaenda kuanzisha upya tena. Wengi wetu tukishatulia pamoja kukatiki, hatuwezi tena kufikiria niache hili nikaanze jipya maana hili tayari limetiki kwanini nikajitupe tena ulingoni?

Lakini tunasahau kuwa maisha yapo kwenye kujaribu, kuanza upya sio vibaya na kufeli ni sehemu moja wapo ya safari, ni sehemu moja wapo ya kuwa hai, kuishi. Hauwezi kuishi maisha yako yote huku ukiwa umefanya maamuzi sahihi mwanzo mwisho, utakuwa hata haujajifunza, haujakuwa na uliishi maisha yako ili uwe salama tu maana ulikuwa unajilinda na kukosea. Kuishi maana yake kujaribu, kukosa, kufeli nak. Kama vile kupata, kufanikiwa nk ilivyosehemu ya maisha ndivyo hayo mengine pia yalivyo. Hatujazoea kuona kufeli kama sehemu ya kuishi na kuendelea mbele baada ya kufeli na ndio maana wengi huchukua muda mrefu sana kunyanyuka au hushindwa kunyanyuka kabisa na kujisamehe baada ya kukosea / kufeli.

Na kutozoea huku kunaweza kuwa kumekuja kutokana na tuliyopitia tulivyokuwa watoto, unajua vile ukifeli darasani ilikuwa inaonekana kama ni kitu kibaya sana kiasi kwamba unaadhibiwa kwa kufanya hivyo, hii inaweza kutujengea kufikiria kuwa kufeli ni jambo la kuogopwa, ni jambo la kuepukwa, ni jambo la aibu kulipitia.

Nahisi ninachojaribu kukiongelea hapa ni kuwa inabidi tubadilishe mtazamo wetu kuhusu kufeli, ni vizuri kuangalia kufeli kama jambo la kujifunza, kama sehemu ya maisha na kuishi, labda tukibadilisha mtazamo huu itatusaidia kuondoa woga wa kujaribu.


Kama ungependa kujiunga group langu la WhatsApp ambalo natuma makala hizi moja kwa moja, BONYEZA HAPA.

Na pia kama unapenda kusapoti uendeshwaji wa blogu hii kifedha, unaweza nisapoti kwa kutuma kiwango chochote utakachopenda kwenda namba hii 0627975502. Fedha hizi zinanisaidia kulipia hosting ya blogu hii.

Share Your Thoughts With Me

Translate »