Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku,  Self Care

Mambo 5 yatakayokusaidia kudili na watu wagumu

Au Mambo 5 ya kujua / kufanya unapokutana na watu wagumu


Watu wagumu wapo kila mahali, majumbani, kwenye koo zetu, kazini, vyuoni na hata kwenye mahusiano yetu.

Watu hawa ni marafiki, walimu, wazazi, mabosi, ndugu na hata wapenzi wetu.

Unaweza ukawa umekutana na watu wagumu, au wewe ndio ukawa mtu mgumu😁🙊, ila leo nitaongelea tu kama umekutana nao, mambo ya kujua na ya kufanya.


Mara nyingi watu wagumu hupenda kukuaminisha kuwa ni makosa yako ndio yanayosababisha wao wawe wagumu kwako, ila ukiangalia kwa ukaribu ugumu huwa ni tabia yao sio matokeo ya makosa yako.

Lakini pia kama vile ninavyoenda kushea jinsi unavyoweza kuwajibika kwaajili yako, kila mtu anatakiwa awajibike kwaajili yake kwahiyo si sawa kukulaumu wewe kuwa ndio chanzo cha wao kuwa wagumu wakati kama kweli wangekuwa na lengo la kujiendeleza binafsi wangefanyia kazi ugumu wao kwaajili yao.

Hilo ndio jambo la kwanza ambalo ningependa ujue, inawezekana ni tabia yao, inawezekana ni kushindwa kutatua matatizo yao, inawezekana ndivyo walivyoamua kuishi lakini kukulaumu wewe ni moja wapo ya njia ya wao kujisikia kuwa kuna sababu ya wao kuwa wagumu, kuna sababu ya wao kuwa hivyo walivyo na hawana haja ya kujiangalia shida zao ili kuzitatua kwa vile wameshakulaumu wewe kuwa ndio chanzo.

Na unajikuta unabadilika ili kuwafurahisha ukiamini kuwa labda hiki au kile unachokifanya ndio sababu lakini bado haisaidii. Bado kwao hautoshi kwa kila unachokifanya.

Watu wagumu wanachosha, kimawazo, kihisia na kimwili.

Kusema ukweli watu wagumu wanakuja katika njia tofauti, wengine ni wagumu kukusikiliza, wengine ni wagumu kukuelewa, wengine ni wagumu kwa vile wanakufanyia roho mbaya, wengine ni wagumu kwa vile wanataka kukufanya maisha yako sehemu fulani yawe magumu, wengine ni wagumu kwa vile wanakataa kubadilika katika jambo fulani nk.

Ila katika yote, nimeona kuna mambo matano yanayonisaidia mimi kudili ninapokutana na watu wagumu, nayo ni;

1. Tafuta amani yako

Iwe kwa kukaa au kwa kuondoka tafuta amani yako.

Huwa tunapenda kuamini kuwa tunauwezo wa kugusa mioyo ya watu na kuiponya. Au tunaweza kubadilisha watu.

Ukweli ni kuwa mtu hubadilika anapoamua. Mtu hubadilika mwenyewe.

Ukiamua kukaa, jua ni jinsi gani unaweza ukaweka amani yako moyoni huku ukijua huyo mtu alivyo.

Kuna kitabu nilisoma na mwandishi akasema, ‘usiwaruhusu wakufanye uwachukie’. Ni ngumu kimatendo kutomchukia mtu wa hivi, ni ngumu hata kwangu, lakini kama utaweza nahisi ni jambo zuri sana kutowapa muda wako na nguvu zako kwa kuwachukia.

Ila tafuta amani yako ya moyo na mawazo kwanza.

2. Uwe na mipaka nao

Ukimwachia mtu wa hivi atakupanda kichwani. Ukimwachia atakufuatilia katika kila jambo la maisha yako.

Yani kila eneo anaweza akawepo, kama sio kuwepo yeye basi atakuwepo kupitia mawazo yako.

Watu wagumu huwa wanaonaga kuwa wanaweza kuvuka mipaka ya kila mtu na kumiliki mida ya watu pale wanapoamua.

Uweke mipaka naye. Au uwe na mipaka ambayo wewe unaijua juu ya huyu mtu. Kwamba labda nitakaa naye nikianza kuona ashaanza kunifanya nikasirike, naondoka. Au tunakutana tu jioni au vyovyote vile mipaka yako inavyoweza kuwa.

Weka tu mipaka inayokusaidia kutunza amani yako.

(Haya yote yanafanya kazi pale ambapo wewe hauna namna ya kuondoka au kuachana na huyo mtu mgumu kwa haraka. Maana kama unaweza kuondoka, ondoka kwa vile baada ya kukaa kwa muda na watu wagumu unaweza pata vidonda ambavyo vinachukua muda hata kupona.)

3. Ondoa mawazo ya kuwa unaweza kumbadilisha

Kama umeamua kumfanyia mema, vizuri. Ila usimfanyie mazuri ukihisi kuwa ataona uzuri nakubadilika.

Watu hubadilika wanapoamua.

Wanapoona kubadilika kwao kuna umuhimu kwao, au kunafaidisha maisha yao kwa namna moja au nyingine. Au kunawafanya wajisikie watu wazuri kwa namna moja au nyingine.

Hauna nguvu sana kwenye maisha ya mwingine kama unavyodhani unayo au kuliko yeye alivyo na nguvu juu yake.

Na muda mwingine watu wagumu wanavidonda mpaka vipone ndio wanaweza kubadilika, wewe hauwezi kujua kinachowafanya wawe hivyo.

Hivyo tua mzigo na mawazo ya kuwa utambadilisha.

Utajichosha.

Na angalia na kuwa makini na jinsi vile unavyoumizwa kwenye hiyo hali uliyopo.

Unastahili amani pia.

Jua kuwa ni yeye, na ndivyo alivyochagua kuwa na kuishi, cha msingi ni wewe kujua jinsi ya kuishi naye ambapo ugumu wake haukuathiri kama anavyotaka ukuathiri. Kujitenga kiakili na drama zake na kuona kuwa ishu zake ndizo zinazompelekea kuwa hivyo. Mwisho wa siku yeye pia ni binadamu

4. Kuwa makini ili usibadilike ukawa kama wao

Binadamu ni matokeo ya mazingira yetu kwahiyo watu wanaotuzunguka wanachangia sana sisi kuwa na tabia, mawazo na mienendo tuliyonayo.

Hiyo haimaanishi hatuna wajibu wa kujichunguza ili tubadilishe yale tusiyoyapenda na hivyo ni kazi yako kuangalia ni tabia gani unazichukua kutoka kwa watu wagumu.

Inaweza ikawa hata namna ya kumjibu au namna ya kujizuia asikuumize ambayo ukiendelea nayo kwa muda mrefu inakuletea madhara kuliko faida au inakufanya wewe kuwa mtu mgumu, una wajibu wa kuziacha kwaajili yako mwenyewe.

Ukikaa na watu wagumu kwa muda mrefu unaweza kuwa mtu mgumu, hivyo kujiangalia ni namna gani kukaa nao kumekubadilisha ni jambo zuri.

5. Punguza matarajio

Ukishamfahamu mtu, punguza matarajio yako kwake.

Usitegemee sana ukamilifu au mabadiliko ya kweli ya ghafla kutoka kwake, matarajio ndio huwa yanaumiza.

Matarajio ni upanga ukatao kuwili, kwa namna moja ni mazuri kuwa nayo, lakini pia si mazuri kuwa nayo hasa katika hali kama hii.

Ukiwa na bosi mgumu kwa mfano, ukafanya kazi yake, usitarajie sana kuwa atafurahia kwa vile umefikia kiwango anacholalamika kila siku kuwa haufiki, inaweza isimfurahishe pia.


Na hayo ndio mambo yanayonisaidia ninapokutana na watu wagumu, mambo gani hukusaidia wewe kudili na watu wagumu?

Eunice

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป