Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku

Jinsi ya kujisamehe

Kwenye maisha yangu nimesema vitu ambavyo nikivikumbuka najutia kusema au najisikia vibaya, nimefanya vitu ambavyo nikivikumbuka nakuwa mpole najawa na huzuni.

Wote tushasema vitu, tushasahau kufanya vitu fulani, tumeshawahi kuwakosea wengine kiasi kwamba hata kama wametusamehe sisi bado tunajihukumu mpaka leo, kwa vile sisi ni binadamu basi na uhakika sio peke yangu ambaye nilichukua muda na kupata shida ya kujisamehe mwenyewe kwa makosa niliyoyafanya kwangu mwenyewe au kuwafanyia wengine.

Kuna tofauti kati ya kusikia vibaya kwa kujihukumu na kusikia aibu, leo naongelea kujisikia vibaya kwa kujihukumu mwenyewe ingawa umeshasamehewa au uliomba msamaha ukakataliwa lakini bado wewe mwenyewe unashindwa kuachilia lile kosa ulilofanya na hivyo kujihukumu na kujisikia vibaya kila ukikumbuka.

Pia Soma : Jinsi ya kusamehe

Muda wote ninaojisikia hivi huwa najikumbusha kuwa hii hisia ndio inayonifanya niwe na utu, ni kawaida kujisikia huzuni, hii hisia ya kujutia ndio inakusaidia kutorudia, kujifunza na kubadilika kama utataka. Isingekuwepo sijui ningekuwa mtu wa namna gani, ni hisia ambayo inanifanya nione ubinadamu wangu.


Kujisamehe ni jambo la muhimu kwasababu hauwezi kuwa unajihukumu maisha yako yote kwa jambo ulilolifanya inafika muda inabidi tu uachilie, upate amani, ujue kuwa ulikosea na hilo kosa liwe sehemu ya stori ya maisha yako, usipojisamehe unalibeba na linakuwa ni maisha yako yote maana utabeba majuto milele.

Kuna mambo machache yanayonisaidia kujisamehe ndio ninayoenda kukushirikisha leo, nayo ni;

Ongea na mtu, hata kama sio uliyemkosea

Muda mwingine kuongea na mtu kuna kupa wazo jipya lakini pia muda mwingine kaombe msamaha kwa uliyemkosea. Muda mwingine unahitaji tu kutoa hizo hisia unazosikia au unahitaji mtu mwingine aone hilo kosa ulilofanya kwa jicho la tofauti lakini pia muda mwingine unahitaji amani inayopatikana kwa kujua kuwa umesamehewa na yule uliyemkosea.

Kubali kuwa una mapungufu

Unaweza ukawa umejifunza kutoka kipindi kile mpaka sasa lakini binadamu una mapungufu haujui yote na muda mwingine kuwaza kwako kunaingiliwa na historia, una fikira fulani kwa watu wa aina fulani, mapungufu yako lazima yataumiza watu, sio kwamba nakubali na nakusapoti uende uumize watu duniani hapana, ila nakuambia haya ili ujipe neema uone ni jinsi gani wewe pia ni sehemu ya dunia na ya watu ambao hawajakamilika.

Jikumbushe kuwa umefanya jambo baya ila wewe sio mtu mbaya

Mpaka leo sijawahi kutana na mtu mwenye lengo, nia na mawazo ya yeye duniani aishie kuwa mtu mbaya kila mmoja wetu anapenda kuwa mtu mwema, afe akumbukwe kwa mema aliyoyafanya. Inawezekana umefanya jambo baya ila wewe sio mtu mbaya kuna mambo mengi yanachangia hapo, maamuzi mengi mabaya unefanya na yamekufikisha hapo ila ndani yako wewe sio mtu mbaya, ni mtu mwenye tamaa kubwa sana ya kuwa mtu mzuri.

Jioneshe neema

Wakati ule ulipofanya ulilolifanya ulikuwa haujui unayoyajua sasa, jioneshe neema maana wewe ni binadamu unaekua unayejifunza kutokana na uliyoyafanya, mwisho wa siku wewe ni binadamu tu. Najua wengi huwa tuna matarajio makubwa sana ya uwezo wetu wa kuwa watu wema kwa watu ila mara nyingi ukweli hauko hivyo. Na ndio maana kipimo hicho hicho tunachojipimia tunawapimia wengine na tunaweka matarajio makubwa kwa wengine pia lakini mwisho wa siku wao ni watu tu.

Ukijionesha huruma na kujua kama wewe ni binadamu ( huwa tunajiambiaga maneno makali na mabaya kimoyomoyo ambayo kikawaida huwezi kumwambia mtu unayempenda au rafiki yako), hivyo pia badilisha maneno unayojiambia kimoyomoyo. Jiambie maneno yanayokuonesha neema. Lakini pia jua kuwa ulifanya ulilofanya kutokana na mahali ulipokuwapo na vitu ulivyokuwa unavijua wakati ule. Ni hali ya kibinadamu. Wewe ni binadamu (binadamu unauwezo wa kufanya mambo mabaya na mazuri).

Chukua muda kujifunza kuhusu kosa ulilofanya

Kwanini ulilifanya (saikolojia yako) na maumivu uliyosababisha kwa wengine kupitia hilo kosa kama watakubali kukushirikisha. Njia nzuri ya kutorudia ni kujua trauma iliyosababisha ufanye hivyo na maumivu uliyosababisha

Kukubaliana na matokeo ya kitendo chako

Ukweli ni kuwa hakuna utakalofanya litakalobadilisha matokeo ya kosa lako. Huu ukweli unaumiza lakini pia unafariji na kukufanya uangalie ni jinsi gani utazuia hili kosa kutokea tena huko mbele. Kujihukumu muda mwingine kuna kuaminisha kuwa kuna jambo inabidi ulifanye ili ustahili kusamehewa, kwenye makosa mengine, kuna mambo unaweza fanya ili kurudisha mahusiano, ila mara nyingi hakuna jambo la kufanya ili kufuta/ kujisahaulisha kosa ulilofanya.

Jiahidi kutorudia kosa.

Hali nyingine ikijitokeza kama ile wewe sasa unajua vyema kutokurudia makosa. Kuna msemo unasema, ‘kosa si kosa bali kurudia kosa’. Kosa ni kosa ila ukirudia ni makusudi kwasababu unajua jambo jema la kufanya hali inapojirudia. Jitahidi kubadilika taratibu usiwe na matarajio ambayo hayawezi kutimia unapotaka kubadilika, ukiwa na matarajio makubwa utahisi hauwezi kubadilika na hivyo wewe ni mtu mbaya na haustahili kujisamehe.

Pia Soma : Kama unataka kubadilisha maisha yako…

Jikumbushe kumbukumbu nzuri za mambo uliyoyafanya pia

Ili ujue kuwa una uwezo wa kufanya mazuri ila pia unastahili kujisamehe kwa vile una wema ndani yako. Mfano kama ni mahusiano na unashindwa kujisamehe kwasababu ulifanya usaliti, katika safari yako ya kujisamehe kila unapokumbuka usaliti, kumbuka pia vile ulivyofanya mazuri kwenye mahusiano yako kabla ya usaliti, ukiwaza mazuri kwa muda mrefu yanakusaidia kujiona kwa picha kamili ya ubinadamu ulionao.


Kuishi bila kujisamehe kwenye maisha kunatesa, kwasababu tunatembea na mabaya yote tuliyoyafanya kwenye maisha, tunahisi hatustahili furaha kwenye maisha kwa vile tulifanya ubaya fulani na hivyo tunaishi maisha ya ovyo kihisia, kiakili na kimatendo kwavile tunajiaminisha kuwa tunastahili hayo maisha kwa ubaya tuliofanya. Kutokujisamehe kunafanya kosa lako kuwa ndio stori yako ya maisha badala ya kosa lako kuwa sehemu ya stori yako ya maisha. Stori yako ya maisha ni kubwa zaidi tu ya makosa uliyofanya, maisha yako pia yanawema uliowahi kuufanya, kuna mengi zaidi ya ubaya au makosa.

Sio kila mahali unaweza ukasamehewa na wale uliowakosea na kama haujasamehewa ni vizuri kuheshimu maamuzi na muda wanaochukua kukusamehe na kaa mbali mpaka watakapokuwa tayari, lakini pia kutosamehewa haimaanishi wewe pia usijisamehe.

Kila mtu anajipa uhuru unaotokana na kusamehe/ kujisamehe mwenyewe na hili linatokana na muda wa mtu kudili na vidonda vilivyotokea, ninachojaribu kusema hili ni swala binafsi ambalo mtu anaweza akalifanya mwenyewe. Jisamehe ili upate furaha hata kama haujasamehewa ( lakini nina tumaini haujasamehewa wakati pia ulionesha nia ya kuomba msamaha na ulionesha kubadilika kwao ila tu hawajakusamehe, isije ikawa haujasamehewa kwasababu haujaomba msamaha, siongelei hilo)

Unastahili nafasi ya pili, jipe nafasi ya pili kuishi maisha ya furaha. Haijalishi ni jambo gani ulilowahi kulifanya kwenye maisha yako, unastahili neema. Unastahili furaha tena, unastahili kujisamehe na kuishi huru na kuwa mwepesi moyoni. Unastahili kukumbuka yale uliyofanya kama somo na sio kioo cha kukufanya ujisikie wewe ni mtu mbaya.

Eunice

4 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป