Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Dondoo za Maisha,  Maisha ya kila siku

Mambo 3 ya kuyajua unapohama nyumbani na kwenda kujitegemea

Kuna muda unafika kama kijana unaamua kwenda kujitegemea, kuishi mwenyewe, kutafuta maisha mahali pengine mbali na nyumba ya wazazi. Muda huo ukifika kwako au ukiamua kufanya uamuzi huo, hivi ni vitu vya kuvijua katika maandalizi yako ya kuhama nyumbani kwa wazazi;

– Woga na maswali uliyonayo ni ya kawaida

Ukiamua kwenda kuishi mwenyewe kukutana na changamoto za maisha peke yako lazima upate ule woga ambao ni jambo la kawaida. Woga kuhusu maisha yatakavyokuwa, wasiwasi wa kuishi mbali na wazazi, maswali kama je utaweza? Vipi ukiishiwa hela nk. Kuishi na wazazi ni sehemu salama, kwa vile wengi wetu hatuingii gharama yoyote nyumbani, tunaishi na watu tunaowapenda hivyo tunapata mahitaji mengi kiurahisi nyumbani, ukienda kujitegemea haya yote unayakosa, hivyo wasiwasi, maswali na woga ni jambo la kawaida.

Ila ni muhimu kujua kuwa kuhama nyumbani ni jambo la muhimu kwako, litakujenga kusimama mwenyewe kwenye dunia. Alama moja wapo inayoonyesha kuwa mzazi amefanikiwa kwenye malezi ni kuweza kulea mtoto anayeweza kusimama na kupambana na changamoto za dunia mwenyewe. Wanyama wote hufanya hivyo, na binadamu pia. Hivyo usiache woga ukakufanya ukaacha kwenda kukutana na dunia, muda umefika nenda kapambane mwenyewe.

– Muda umefika wa kuyajua maisha wewe kama wewe

Unapoishi nyumbani, mawazo yako yote yanatokana na imani, mawazo, mwenendo wa maisha mnavyoishi kwenu. Hata siku moja hauwazi kuwa kuna watu sehemu nyingine wanaoishi tofauti na vile mnavyoishi. Unapohama nyumbani unaenda kujifunza kuhusu mitindo mingine ya maisha na jinsi watu wengine wanavyoishi. Haimaanishi wao wako sahihi na kwenu mnakosea hapana, ila inakupa wigo mpana wa kuona yapi utayapenda uyachukue kwenye maisha yako na yapi uyaache. Kuishi mwenyewe kunakupa fursa ya kuamua kutengeneza maisha yako na jinsi vile utaamua kuishi mbali na presha za wazazi au mawazo yao.

– Tengeneza jamii yako utakayopenda ikuzunguke

Maisha yetu siku hizi ni tofauti na zamani, wengi wetu tunajuana na watu wa kwenye mitandao kuliko tunavyojuana na majirani. Kama umehama nyumbani na unaenda kuishi mbali, jitahidi kutengeneza urafiki na watu, upate jamii yako, ufahamiane na watu wanaoweza kuwa msaada kwako unapokutana na changamoto yoyote ukiwa mbali na wazazi na familia. Jitahidi kupata vitu vya kufanya, urafiki nk. Tengeneza maisha yanayokufurahisha kwenye mji huo uliohamia ili ujisikie pia kama upo nyumbani maana hapo ndio nyumbani kwa muda huo.

Mambo mengine ya kuyaangalia ni uchumi, ni muhimu kujifunza matumizi mazuri ya hela, kula vizuri vyakula unavyopika mwenyewe, ni muhimu kuangalia kuhusu usalama wako pia kwenye sehemu hiyo uliyohamia na unayoishi nk. Haya nitayaongelea kwenye makala nyingine ila kwa sasa niambie kwenye comment kama umeamua kwenda kujitegemea na unaenda mkoa gani?

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป