Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Career Guide,  Maisha ya kila siku

Faida na Umuhimu wa Kujitolea

Kujitolea mimi nakuelezea kama kitendo cha kutoa muda, ujuzi, uwezo na nguvu kwaajili ya kufanya jambo fulani ambapo mara nyingi huwa hautegemei malipo ya kifedha, ila malipo pekee unayopata ni hisia nzuri unayojisikia baada ya kufanya wema.

Hivi karibuni kumekuwa na maswali na mabishano mengi yanayohusiana na kujitolea.

Je, kuna umuhimu?

Au tunatumia muda bure?

Au wanatutumia tu kwa bure kabisa bila kutulipa kiwango ambacho elimu yetu inahitaji?

Maswali ni mazito na yanahitaji kufikiri sana kwakweli

Ila ngoja nikushirikishe kidogo faida za kujitolea ninazozijua:

Mwanajamii ndiye mjenga jamii

Mimi napenda sana kazi za jamii, naamini kwamba kujitolea inanifanya kulitumikia taifa langu na kuijenga jamii yangu.

Unajitambua na kujua uwezo wako

Kutokana na kufanya kazi na watu mbalimbali, kuishi na watu mbalimbali na pia kupitia changamoto mbalimbali unapata kujitambua wewe ni nani, una uwezo gani nk.

Njia rahisi ya kujua kazi inayokufaa na isiyokufaa pia ni kujitolea katika kazi hiyo ili uone kama utapenda kuifanya au la lakini pia unajua eneo gani la kiofisi uongeze bidii na eneo gani uko vizuri sana.

Unajifunza vizuri mambo ya kazi na maisha

Kujitolea pamoja na vijana wenzio kuna kukutanisha na vijana wenye imani, mitazamo na tabia tofauti.

Lakini pia wakati unajitolea na kufanya kazi unapata uzoefu, ambao pia unaweza kuuweka kwenye CV na kujifunza vitu vipya.

Unakua kitabia pia (personal development)

Kuna mambo kuhusu sisi ambayo tunajifunza kila siku, na muda mwingine hatuoni umuhimu wa kubadilika kwa vile hatuna sababu. Tukienda kazini inaweza ikawa gharama sana maana hakuna mtu anayekulipa umuingizie hasara.

Hivyo nadhani kujitolea kunakusaidia kujitambua na kuona vitu gani uvibadilishe kwaajili yako mwenyewe pia, na inaweza ikawa hata kujitolea kukakufanya ujiamini zaidi, kitu ambacho ni kizuri kwenye maisha.

Unatengeneza kumbukumbu nzuri kwenye maisha na kujifunza jinsi ya kuwa raia anayewajibika kwenye nchi yako

Mara nyingi hatuoni umuhimu wa kufanyia jambo mema nchi yetu kwakuwa hatuna madaraka.

Lakini nahisi huu mtazamo unatufanya tusione wajibu wa kulitumikia taifa kwa kuwa tu wewe ni mzaliwa wa taifa hilo.

Nakumbuka kabla ya kuanza kazi yetu ya kujitolea Mwanza tulipewa semina kuhusu raia na wajibu wake kwa nchi, kujenga nchi yetu ni kazi yangu na yako pia. Kwa kujitolea katika sekta unayoipenda kuibadilisha, kuiongezea kitu nk unalijenga taifa pia.

Lakini pia unatengeneza kumbukumbu za maisha. Nilipata nafasi ya kuishi Mwanza ambapo sijawahi kuishi hapo kabla na pia kwenda Shinyanga kwasababu tu ya kujitolea. Niliishi na watu ambao tulicheka, tulijifunza, tulikula na kufanya mengi pamoja ambao pia wamenibadilisha na kunisaidia kukua katika namna moja au nyingine.

Na huo ndio umuhimu wa kujitolea kwangu, ambao naona unazidi hata majibu ya maswali hapo juu.

Je, umeshawahi kujitolea?? Na faida za kujitolea kwako ni zipi?

Eunice

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป