Napenda kujua jinsi ya kuishi vizuri na watu ili nimuwakilishe vizuri Kristo kupitia maisha yangu, napenda kuwa na hekima katika maisha yangu, napenda kuenenda katika njia impendezayo Mungu, napenda kuwa na maneno mazuri ya kuwafariji watu hasa katika dunia hii yenye misukosuko na mapito mengi ambayo watu hupitia, napenda kujawa na nguvu za Mungu, napenda nifahamu mimi ni nani kutoka kwa Yule aliyeniumba, napenda nifahamu kusudi la kuumbwa kwangu, zaidi ya yote napenda kufahamu wapi naenda lakini pia nini ninaamini.

Mimi ni mtu ambaye huwa napenda kufuatilia vitu kwa undani kabla sijajiunga navyo ili niwe na uhakika wanaendana na misingi yangu, lakini pia huwa napenda kufanya machaguo sahihi ili nisije kuona wivu kwa wale waliochagua mengine ambayo nitofauti na yangu kwasababu hiyo huwa nafanya uchunguzi wa jambo kwa undani zaidi.Ikija kwenye kumfuata Yesu,uchunguzi huu huwa naufanya katika Neno la Mungu.

Neno la Mungu ni ramani ya mkristo. Napenda kusema ni ramani kwasababu vyote nilivyovielezea hapo juu na zaidi vinapatikana kwenye Neno la Mungu.

Biblia ni ramani kwa mkristo inaelezea dunia imeanzia wapi (Kitabu cha MWANZO) mpaka dunia itaishia wapi (kitabu cha UFUNUO WA YOHANA). Ni ramani inayotuonyesha jinsi tunavyotakiwa kuishi na vitu tunavyotakiwa kufanya, jinsi ya kumpendeza Mungu lakini pia jinsi wenzetu walivyomtafuta Mungu kabla ya kizazi chetu.

Neno la Mungu linatupa nguvu na kutuondolea woga, tukumbuke kama Mungu alitamka tu Neno lake na dunia ikawa, si zaidi hili tunalolisoma kubadilisha maisha yetu kabisa? ( Kwa maana neno la Mungu ni hai tena lina nguvu; ni kali kuliko upanga wenye makali kuwili, linachoma kabisa na kutenganisha nafsi na roho, viungo vya mwili na mafuta yaliyomo ndani yake; na kutambua nia na mawazo ya mioyo ya watu- Waebrania 4:12).

Neno la Mungu linatueleza Mungu ni nani, na tunapata kumjua kwa ukaribu sisi wenyewe kupitia maandiko, tena neno la Mungu linatutofautishia ukweli na uongo. Wakristo tusome neno la Mungu, linatusaidia sana katika dunia hii ya sasa ambapo vitu vingi vinatuchanganya sana.

Kipindi cha Yesu wakati anajaribiwa na shetani, Yeye mwenyewe mwalimu wa kweli alituonyesha ni jinsi gani ya kumshinda shetani, ni kujawa neno la Mungu ndani yetu Luka 4:1-12, kwa namna hii alimshinda shetani kwa kumwambia imeandikwa- yaani imeandikwa katika Neno la Mungu. Mabinti wazuri wa Kristo tusome neno litubadilishe tabia,mienendo na kutufanya tumjue Mungu zaidi. Lakini pia Daudi katika Zaburi anasema “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi – Zaburi 119:11”.

Vijana tujawe neno tushinde tamaa za ulimwengu ili tuwe chumvi na nuru katika huu ulimwengu, Vijana tujawe neno tutofautishwe kwalo ndani ya dunia hii na mahali popote Mungu allipotuweka.

Biblia sio kitabu cha stori ni kitabu chenye maneno yenye nguvu ya kubadilisha fikra, uelewa, mwenendo lakini pia maisha yetu kwa ujumla.

Vijana tusome Biblia tuijue kwa undani imani tunayoiamini ili tuweze kuielezea kwa wale walio karibu yetu na kujibu maswali ya imani tuliyonayo (1 Petro 3:15-Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu.

Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu), napenda tuisome Biblia ili tuijue imani tuliyonayo na huyu Yesu lakini pia Nguvu zake kwa undani, tusiamini kwa sababu wazazi wanaamini, bali tuamini kwa ajili yetu na kwasababu tumesoma na kumjua Mungu kwa undani.

Tunalo neno la Mungu kwasababu hii basi, tuyachunguze maandiko. Tujiangalie sana tusije tukawa tunajua maneno ya watumishi sana kuliko Neno la Mungu. Kwasababu naamini Mungu analiangalia Neno lake ili alitimize na si ya watu, sasa kama tumeshika maneno ya watu sana kuliko Neno lake hatupo sehemu nzuri kiroho.
Kwa ufupi nielezee faida za kusoma neno la Mungu,

 • Maisha yetu yanategemea neno la Mungu- Mathayo 4:4 “Lakini Yesu akamjibu, “Imeandikwa, ‘Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno analotamka Mungu”. Yesu alimjibu shetani hivi baada ya kujaribiwa kula mkate.Hii ni kweli kwasababu Neno la Mungu ndio inatupa maelekezo katika maisha, ndio linatupa kusudi katika maisha yetu, kwahiyo tusije tukadhani kuwa maisha yetu ni vyakula, la hasha maisha yetu ni Neno la Mungu ambalo linaimarisha hata kiRoho chetu. Mtu ni Roho, Nafsi na mwili, tusijetukaujenga mwili kwa mkate na kusahau kujenga Roho kwa Neno la Mungu na hivyo kushindwa kuishi kama Yesu alivyosema katika mstari huu.
 • Kujua maisha ya Kristo na jinsi ya kuishi maisha yetu katika kumpendeza yeye: katika vitabu vya Mathayo,Marko,Luka na Yohana tunaona jinsi gani Yesu aliishi maisha yake akiwa hapa duniani. Ili tuishi maisha ambayo yanampendeza Mungu ni vyema tukajua maisha ambayo Yesu aliishi lakini pia tukajua misingi ambayo aliisema kwa ajili ya wale wanaomfuata, tukajifunza mafundisho aliyoyatoa alipokuwa duniani ili kuyafanya hayo, Neno la Mungu limeelezea vizuri maisha ya Yesu lakini pia maisha ya mitume waliomfuata baada ya Yeye kumaliza kazi.
 • Kupata tumaini la maisha: Neno la Mungu linatupa tumaini katika njia mbili
 1. Tunaposoma habari za watu waliotembea na Mungu na kuona jinsi Mungu alivyowashindia tunajifunza, tunakua katika imani lakini pia tunapata tumaini kwa yale tunayoyapita, tunaposoma habari ya Daniel katika tundu la simba na jinsi Mungu alivyomtunza akatoka mzima, tunapata tumaini katika jaribu au tatizo lolote tunalolipia kwa maana tunaamini kama alifanya kipindi kile hata sasa anaweza kufanya- Waebrania 13:8-“Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele”. Kwahiyo kama alifanya kipindi kile,atafanya na sasa kwa maana ni Yeye yule. Na hili linatupa tumaini ya maisha yetu hapa duniani.
 2. Tunapata tumaini ya mambo yajayo, tunaishi tukijua kwamba mwishoni tunashinda, tunajua kuhusu Mbingu mpya, tunaishi tukijua duniani sio kwetu, makazi yetu ya kudumu yapo kwa Baba, na anatuandalia makao, tukishashinda yote ya dunia tutaenda kuishi naye milele. Na shauri sana mabinti wenzangu tusome ufunuo ili tujue tunapoelekea baada ya mwisho wetu wa maisha ya hapa duniani kwani tuklijua hilo tutaishi maisha haya kama maandalizi ya maisha yajayo, hatutaishi kama tumefika duniani ila tutaishi kama tunapita duniani.
 • Kujua wapi tunaelekea na matukio ya siku za mwisho, nilikutana na mtu mmoja nilipokuwa sekondari ambapo tulikuwa tunaongelea kuhusu mambo ya kifo na imani. Aliniuliza nikifa naenda wapi na matukio ya siku za mwisho, nilipo muuliza yeye hili swali alinijibu akifa anabadilika na kuwa gesi na nyota kisha atakaa kwenye mawingu na kuangaza usiku kama nyota zinavyofanya kila siku. Nilishtuka sana kwasababu sijawahi jua kuwa kuna watu hawajui matukio ya siku za mwisho, lakini pia nilishtuka sana kwamba anadhani atakuwa nyota, Neno la Mungu linaelezea matukio ya siku za mwisho, mabinti tulisome tujue tunaelekea wapi. (kujua kuhusu siku za mwisho unaweza ukasoma kitabu cha Ufunuo kinaelezea mengi).
 • Kujitambua sisi ni nani, kuna siku nilikuwa darasani na wanafunzi wenzangu na katika maongezi yetu tukawa tunaongelea Neno la Mungu, na ndipo nilipomwambia rafiki yangu ,”hivi unajua Mungu anampango na maisha yako”,nilimwambia maneno hayo wakati tunaongelea mipango ya maisha yetu kama vijana ambapo yeye aliongelea mengi sana aliyotaka kujifanyia kuhus maisha yake. Ndipo rafiki yangu alipopigwa na butwaa na kushangaa kwani maisha yake yotehakuwahi kujua Mungu anakusudi na maisha yake, na kwamba Mungu anamjua kwa jina lake. Mabinti wenzangu katika karne hii ambapo watu wamechanganyikiwa hadi kuhusu jinsia zao walizozaliwa nazo, napenda tujitambue kupitia Neno la Mungu, napenda tujue sisi ni nani kwa Mungu.
 1. ” Lakini ninyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani akawaingizeni katika mwanga wake mkuu”- 1 Petro 2:9
 2. “Ninyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika” – Mathayo 5:14
 3. “Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, wale ambao wameitwa kufuatana na mapenzi yake. Mungu hufanya hivyo kwa faida yao. Wale ambao Mungu alikwisha kuwachagua tangu mwanzo, pia aliwateua wafanane na Mwanae, ili Mwana awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale ambao Mungu aliwateua tangu awali pia ali waita; na wale aliowaita pia aliwahesabia haki; na wale aliowahesabia haki aliwapa utukufu wake- Warumi 8:28-30
 4. “Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.”- Warumi 8:17
 5. “Lakini katika mambo yote haya sisi ni washindi, naam, na zaidi ya washindi, tukiwa ndani yake yeye aliyetu penda”- Warumi 8:37. Na haya ni machache amabyo Neno la Mungu linatuambia kuhusu sisi, naomba usome zaidi ili ujitambue ndani ya Kristo wewe ni nani.

Tukijitambua sisi ni nani, na ni wa thamani kiasi gani kwa Mungu hatutohangaika kama mabinti kutafuta thamani au kutaka kujijua sisi ni nani kwa wanaume, mavazi au vitu tulivyonavyo. Neno la Mungu linatuambia thamani yetu tuliyonayo kwa Kristo zaidi ya wanaume au hata vitu tunavyomiliki.

 • Kuujua uongo wa dunia hii ila pia kuangalia kila kitu kupitia misingi ya Mungu, unajua dunia inapoelekea kuna vitu vingi vinapotoshwa na jinsi Mungu alivyoviumba. Yatupasa kusoma Neno la Mungu ili kuutenga ukweli na uongo kupitia Neno la Mungu ili tuishi kwa kumpendeza Mungu na sio kufuata mienendo inayoletwa na dunia. Biblia ina kila jibu la maswali yetu, Neno linasema hakuna jipya chini ya jua, kwa hivyo haya yote yalikuwepo na Neno la Mungu limegusia kila ishu na mambo yanayotokea duniani kwa mtazamo wa kiMungu. Tusome Neno tuujue mtazamo wake ili tumpendeze yeye katika maisha yetu.
 • Kutambua chakula kipi cha kiroho kukila na kipi kukiacha, hapa sanasana naongelea walimu na manabii wa uongo, Neno linasema siku za mwisho hawa watakuwa wengi. Je kama mkikristo unauwezo wa kutofautisha mafundisho ya ukweli na ya uongo ukiyasikia? Je utajuaje haya ni ya uongo? Utayajua haya ni ya uongo kwa kuwa umejawa na Neno la kweli la Mungu ndipo utakapogundua kuwa Neno limepindishwa kwa ajili ya matumizi binafsi.Biblia inasema siku za mwisho watu watatumia Neno la Mungu kwa manufaa yao, utajuaje kama hapa limetumika tofauti na makusudi ya Mungu kama haujasoma Neno mwenyewe? Matendo ya Mitume 17:11-12
  “Watu wa Beroya walikuwa waungwana zaidi kuliko watu wa Thesalonike. Walisikiliza neno la Mungu kwa hamu wakachambua Maandiko kila siku ili waone kama waliyokuwa wakiam biwa na Paulo ni kweli. Wengi wao waliamini, ikiwa ni pamoja na wanawake maarufu wa Kigiriki na wanaume wengi” Tunaona watu waberoya wanasifiwa kwa kuyachunguza mafundisho, sio kwa kuwasikia wahubiri tu, la hasha bali kuwasikia na kwenda kuangalia kama waliyoambiwa yanafanana na kile Neno kinasema. Mabinti napenda tujue neno mpaka tufike kiwango cha kuchagua ya kuyasikia na yapi sio ya kuyasikia kuna walimu na manabii wauongo, tumejiandaaje katika kupambanua wa ukweli na wauongo? (https://somabiblia.com/jinsi-ya-kuepusha-udanganyifu-na-mafundisho-ya-uongo/)
 • Lakini pia kulijua ili kuwahubiria mabinti wengine wanaotuzunguka na kuwatia moyo kupitia Neno la Mungu.
 • Kupata majibu ya maswali yanayotuzunguka, mfano mzuri ni mimi na maisha yangu. Kuna mambo mengi ambayo yanatokea katika maisha na mazingira ambayo huwa nipo kwa hivyo huwa najiuliza mbele za Mungu kitu fulani anakichukuliaje, lakini nimekuja kujua kuwa hakuna kitu kipya chini ya jua hivyo majibu yote yapo kwenye Biblia, tukitaka kujua kuhusu swala fulani katika dunia tusome Neno linasemaje kuhusu hilo swala ili tumpendeze Mungu. Tungekuwa tunasoma neno kuna mambo mengi ambayo hayakutakiwa kuwa tunabishania makanisani au hata kwenye maisha kwasababu Neno liko wazi kuhusu hayo mambo.

Kuna faida nyingi za kusoma Neno ambazo nitaziongezea kwenye sehemu ya pili, lakini kwa leo inatosha. Tusome neno, kwasababu ni njia moja wapo ambayo Mungu anaitumia kuzungumza nasisi. Tunataka kupata hekima ya kiMungu katika mambo na maisha yetu lakini pia hata maamuzi,Mungu yu tayari kuzungumza nasi kupitia Neno lake.Lakini pia ukiwa unaanza kusoma Neno la Mungu usisahau kusali na kumuomba Roho Mtakatifu akufundishe na kukuelekeza yale unayoyasoma.

Eunice.

You May Also Like

10 thoughts on “Umuhimu wa kusoma biblia kwa mkristo

 1. Well, I am a Christian enough. – Eunice Tossy

  […] ninapoomba, ninapopitia mambo mbalimbali katika maisha. Kila siku naendelea kukua ndani yake. Also Read: Mkristo na Neno la Mungu –Nimekubalika na ninapendwa na Yesu Kama yule mwizi pale msalabani, all that matters is […]

 2. Gossip Series: Effective ways to stop gossiping – Eunice Tossy

  […] READ: Neno la Mungu na Mkristo […]

 3. Vitu 10 vijana wanapaswa kuanza kuvifanya mapema kwenye maisha yao. - Eunice Tossy

  […] 1)Kumjua Mungu kwa kusoma Neno lake. […]

 4. I am scared - Eunice Tossy

  […] putting what I do for God, first. and putting Jesus, not so far that I can reach Him when I remember or need something from […]

 5. Vitu 10 vijana wanapaswa kuanza kuvifanya mapema kwenye maisha yao. – Eunice Tossy

  […] 1)Kumjua Mungu kwa kusoma Neno lake. […]

 6. Mambo yanayotokea kanisani yanayonipa maswali magumu kuhusu ukristo – Eunice Tossy

  […] — Kwanini wakristo hawasomi Biblia […]

 7. kinge

  Asante kwa ujumbe huu. Kusoma na kuelewa Bibilia ni muhimu sana.

  1. Eunice Tossy

   Ni kweli, asante sana kwa kusoma makala hii

   1. kinge

    Karibu

 8. Mambo ya kufanya unapopitia magumu – Eunice Tossy

  […] mistari ya Biblia: kama unataka kujua umuhimu wa kusoma Neno la Mungu unaweza kusoma hapa . Lakini kuwa na mstari wa Biblia unaokupa nguvu na kukumbusha ushindi katika kipindi unachokipitia […]

Share Your Thoughts With Me

Translate »