Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

hand touching unemotional black woman in traditional neck rings
Maisha ya kila siku,  Random

Kutokujua Kiingereza si Ujinga.

Kiingereza ni lugha.

Kiingereza ni lugha.

Kiingereza ni lugha.

Lugha ya kigeni.

Kiingereza sio kipimo cha akili, ubunifu, ufahamu au daraja lako la maisha.

Nahisi nimeongelea vile nasumbuka moyoni na mambo mbalimbali, kwa mfano vile nilikuwa nachukia mpaka nimekuja kupenda kuishi Mbagala, na vile nimeumizwa na watu wa kanisani, ila leo naomba niongelee jambo jingine ambalo linanikera kama mtu ambaye Kiingereza sio lugha yangu ya kwanza.

Kuna ile dhana ambayo imejengeka kwenye akili za watu bila wao kujua au kwa kujua, ya kuwa kiingereza ni kipimo cha akili na daraja la maisha (utajiri au umaskini).

Kuna vile tunawaangalia watu wanaoongea kiingereza kwenye jamii kwa utofauti na kuna namna tunawaangalia wale wanaokosea kiingereza kwa utofauti na hivyo kuwadharau au hata kusambaza video zao za walivyokosea.

Ni hivi, kiingereza ni lugha, ni kama vile Kihaya, Kishona, Kibena, Kikuyu, Kifaransa, Kihispaniola, na Kichina. Kiingereza ni lugha hivyo mtu unauwezo na maamuzi ya kujifunza au kutojifunza, kiingereza ni lugha unayoweza kukosea kama unavyokosea ukiongea Kiswahili.

Kama Kiswahili unakosea muda mwingine kwanini moyo ushuke ukikosea kingereza? Kama kuna maneno mengine ya kiswahili haujawahi hata kuyasikia ndio umejifunza Leo, kwanini umshangae mtu ambaye pia amesikia neno jipya la kiingereza Leo? Hata wale waliopo nchi ambazo kiingereza ndio lugha yao ya kwanza wanaangalia kamusi, na wao pia wanamaneno hawajawahi kuyasikia au kuyatumia. Lugha ina tabia moja hivi; unakuwa mzoefu na mjuzi sana wa maneno unayoyatumia sana.

black and white book business close up

Kuna ile namna ambayo naona bado kuna “utumwa” kwenye jamii nyingi za kiafrika, hasa likija swala la Kiingereza/ au kuishi na Wazungu. Nilipokuwa Malawi, kuna mama alikuwa anatafuta Dada wa kazi, na aliweka vigezo kuwa hataki mdada asiyejua kiingereza, hataki mwanae akue huku akiongea kichichewa (ambayo ndio lugha yao ya taifa). Hivyo alikataa mtu anayeongea kichichewa.

Mimi naweza kumuelewa anakotokea mpaka kusema yote haya, katika jamii ambayo tunawaangalia wanaoongea kiingereza kama watu waliozaliwa matawi ya juu, ni lazima mtu atamani kumlea mwanae kwa mfumo huo ili aihifadhi ile “Hadhi” ya familia yake. Hakuna asiyetaka kuonekana matawi ya juu, na hiyo ndio sababu kila siku watu wanaigiza maisha.

Naongelea hili kwasababu nimelipitia pia, kila Mara ambapo nilikuwa naedit kitu nilichokiandika kwenye Facebook ama Twitter, nilikuwa naedit ili nisionekane mjinga/mshamba kwa kuwa nimekosea. Mpaka nilipoona post za wazungu ambao walikosea maneno pia walipokuwa wakinitumia meseji ndipo nilipoona kuwa nilikuwa najitesa kusoma Mara mia meseji kabla sijaituma, kiingereza ni lugha na wewe si mjinga kama hauijui, jipongeze tayari unajua lugha ambayo inakufanya uwasiliane kwenye maisha, na usikute unajua mbili (ya kikabila na Kiswahili). Kuna watu wanavumbua vitu mbalimbali bila kujua kiingereza, kwahiyo kiingereza sio kipimo cha ukubwa wa IQ.

Katika ulimwengu wetu mambo mengi yamerahisishwa, kuna application hadi za kutranslate lugha + na kamusi hauna haja ya kujiona mjinga.

Labda niseme hili, sio kwamba nawapinga wanaojifunza au naidharau, Mimi naongelea mitazamo inayotudidimiza na kutufanya watumwa wa lugha ambayo sio yetu, wa lugha ambayo ni uamuzi kujifunza.

Kama unajifunza ningependa ujifunze kwasababu unapenda lugha, ila sio ujifunze kwasababu utaondokana na ushamba na ujinga au uonekane matawi. Nimegundua ushamba lazima uwepo kwenye maisha ndio maana huwa tunajifunza, kila mtu ana mara ya kwanza ya kukutana na jambo fulani, hivyo ushamba ni hatua ya kwanza ya kujifunza.

Ushamba sio kitu kibaya ni kwamba haujawi kutana na jambo fulani, na hilo sio jambo baya, ulizaliwa kutoka tumboni sio duniani. Kwahiyo kila unachokiona duniani ni kipya kwako.

Kama unatumia kiingereza kujionyesha ubora wako kwenye jamii, au kujionyesha upo daraja fulani kwenye maisha inabidi ujiangalie mara mbili, kwanini unahangaika hivyo kwaajili ya watu wanaokutazama (tena unahangaika na lugha ambayo sio yako kuwadharau watu wako?) Inawezekana hata haujikubali wewe kama wewe,vile ulivyo, au pia haukubali nchi yako na kuona vya wengine ndio bora, nalo hili ni tatizo.

Kuna vitu Vingi sana tumepoteza kama waafrika kwa kushikiria lugha na mitazamo ya weupe. Ni kweli kila bara lina mambo yake mazuri na mabaya, ila inaonekana tuko vizuri sana kupokea yote tutakayoletewa kiasi cha kujidharau sisi wenyewe na kujiona mambo yetu yote hayafai kabisa, na kuita hilo swala “maendeleo”.

Na ndio maana leo, mwanafunzi wa chuo anachanganya lugha, mpaka anakosa namna ya kujieleza kwa ukamilifu kwa kutumia lugha moja (Mimi wa kwanza katika hili), katika nchi ambayo kiswahili ndio lugha ya taifa, sijaona sababu ya kuinua kiingereza kuliko hata kiswahili chenyewe. Kuna ile namna ukifika chuo, na ukawa unachanganya lugha ndio unakuwa umewahakikishia hata wale wasiojua kuwa upo chuo, wajue upo chuo. Hii dhana nayo haikosawa.

China wanaongea kichina na wanaipenda lugha yao mpaka wanatufundisha sisi, na kwa vile tunapenda lugha za wenzetu na kupenda kwao, basi tuko tayari kuacha vyote kwaajili yao. Badala ya kuendeleza vitu vyenye maana, kama India wanajulikana kwa Computer Science, sisi tunaendelea kudharauliana kwa lugha.

Naomba tubadilishe mtazamo/dhana. Lugha inakusaidia kuwasiliana, lugha ni asili na kitambulisho chako, tujivunie lugha yetu ya kwanza kuiongea, ambayo ni kiswahili kwa watanzania wengi. Kama unapenda na unaona umuhimu jifunze lugha zingine, Ila usiwe mtumwa na kufungwa na mitazamo hasi.

Eunice

15 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป