Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku

Kama umepokea habari mbaya yenye kubadilisha maisha yako

Kuna siku, saa au sekunde unayoweza kusikia habari ambayo inabadilisha maisha yako kabisa tofauti na yalivyokuwa jana. Yako peke yako, maana maisha ya wengine huendelea kuwa kama yalivyokuwa, wakati wewe unaona dunia yako imefika mwisho.

Kuna siku, maneno ambayo ulikuwa unayasikia kwa wengine, mambo kwenye maisha ambayo ulikuwa unayaona yako mbali sana na wewe, au hayawezi kukupata, hukufikia na kwa wakati huo maisha yako vile ulivyoyazoea, vile unavyoyajua hubadilika

Maisha hayatabiriki. Mipango huacha kwenda tunavyopanga. Lakini kujua haya haimaanishi kuwa mipango inapoharibika haituumizi au haituharibii maono ya jinsi tulitaka maisha yetu yawe.

Kama umepata habari ambayo unaona inaenda kubadilisha mwelekeo wa maisha yako, naomba nikupe pole, pole sana na nikutie moyo kuwa haya yote tunayopitia ndio maisha, muda mwingine unakuwa juu ya mlima, muda mwingine unakuwa chini kwenye mabonde na huzuni na uchungu. Hili nalo ni sehemu ya maisha kulipitia, hili nalo ndio kuishi.

Kama umepata habari ambayo inaelekea kubadilisha maisha yako jua kuwa ni sehemu ya safari yako ya kipekee ya maisha. Jua kuwa kila lenye mwanzo lina mwisho wake na hivyo hali unayoisikia sasa hautaisikia milele, jambo hili linakupa fursa ya kuishi maisha kitofauti, tofauti na mipango yako, ila ukikubali mapema na kuachilia itakuwa rahisi zaidi kulipitia kuliko kuwa na majuto, huzuni na uchungu kipindi chote unapopitia hilo jambo.

Kama umepata habari ambayo inaelekea kubadilisha maisha yako, jua kuwa maisha ndivyo yalivyo. Hakuna ajuaye kesho au mbele yake itakuwaje, ni mambo mapya kwetu sote yajayo, yatakayotukuta, tutakayoyapitia.

Maisha ndivyo yalivyo, maisha ndio haya.

Eunice

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป