Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

man standing beside his wife teaching their child how to ride bicycle
Maisha ya kila siku

Kwa wasio na baba, kutoka kwa asiye na baba.

“Asilimia 63 ya vijana wanaojiua wanatoka kwenye nyumba zisizokuwa na baba”-Statistics

Kama hiyo picha inakufanya ukumbuke mbali, au usikumbuke popote kwa sababu hauna kumbukumbu zozote, tupo wote usijali. Baba yangu alifariki nilipokuwa na miaka mitatu kutokana na kufeli kwa ini kwa sababu ya ulevi. Mpaka sasa imekuwa miaka 20 toka afariki.

Katika muda wangu wote wa kuishi sikuwahi kufikiria sana kwamba hayupo, mpaka siku moja niliyokuwa sekondari ambapo nilikuwa nachota maji nyumba ya jirani mida ya usiku, na mtoto wa mwenye nyumba alikuwa nje usiku huo, halafu baba yake akaja kumwambia aingie ndani kwa kuwa ni usiku.

Hilo jambo liliniuma sana na niliwaza sana kwanini liliniuma, na ndipo nilipogundua namimi nilikuwa nataka nipate mtu wa kuniambia niingie ndani usiku ule, mtu wa kunilinda, kazi ambayo wababa wamepewa kwa familia zao, ila sikuwa naye. Na hapo ndo nilipoanza kuona pengo lake kwa uwazi zaidi. Niliona mengi, niliona wababa kwenye graduation walivyokuwa wanafurahia sherehe za watoto wao, niliwaona kanisani, niliwaona wakifungulia magari watoto wao, niliona walivyowabeba, na niliwaona wakiwapa hela za matumizi.

Bila ya kujua na mimi nilitafuta jinsi ya kuziba pengo, nikatafuta mtu wa kuwa naye kwenye mahusiano lakini kwangu alikuwa anaziba pengo,nilikuwa nategemea afanye mambo ambayo baba yangu angetakiwa kufanya, na aliposhindwa nilikasirika, kwanini hakuweza kuziba pengo, nikaachana naye. Nikawa na mwingine, na mwingine tena,nikaachana nao kwasababu hiyohiyo, na hivi karibuni nimejua kisaikolojia hiyo tabia inaitwa “Daddy Issues”.

Unajua Mungu aliiumba hii dunia ienende katika mifumo fulani na isipo timia matatizo hutokea, Mungu aliiumba dunia akaiona njema, ila dhambi ilipoingia ikaathiri ule wema ambao Mungu aliuona.

Na ndivyo ilivyo, wanasaikolojia wanasema makuzi ya mtoto na jinsi anavyokuwa vinaathari kubwa ya vile anaweza kuwa akiwa mtu mzima.

Na asilimia kubwa ya jinsi anavyokuwa utotoni itakuja kumuathiri ukubwani, kwa mfano inasemekana watoto wasiobembelezwa wakilia, wanakuwa watu wazima ambao wanaficha maumivu yao kwasababu hakuna wakuwabembeleza au kuyajali.

Mungu alimuumba baba kama mlezi, mlinzi na mwanaume wa kwanza ambaye anaweza kukuonyesha upendo kabla ya mahusiano. Na daddy issues haziji kwa wale tu waliokuwa hawana baba kabisa kuna wengine baba wapo kiumbo lakini hawapo kihisia kwa watoto wao, wao pia huwa wanapata daddy issues, na sio wanawake tu, na wanaume pia wanaweza wakawa na daddy issues kwa upande wao.

Katika kuongelea hii topic nimejisikia kugusia hii, Mungu amenipatia mama ambaye amaweza kuziba pengo na kwa muda sasa nimejisikia kawaida, mama ambaye ni mpiganaji aliyefanikiwa kunitimizia ndoto zangu nyingi, na katika kuandika hii topic simaanishi kwa namna yoyote kwamba ana mapungufu katika malezi au katika njia yake ya malezi, mi ninaongelea lile pengo la kukosekana kwa uwepo wa baba kwenye familia, na kwasababu mama ameziba nyanja zote za pengo hilo kasoro kihisia., hilo pengo ndio ningependa niliongelee.

Nakumbuka kuna siku nilikuwa posta-Dar, nilikuwa nawaza na kusikitika kwamba sina baba, na nikasikia Mungu akiniambia “hata kama ungekuwa na baba wa kimwili ingekuwa na utofauti lakini asingeweza kuwa na wewe kila mahali, kwa maana sasa upo posta ungemwacha nyumbani, ila mimi nipo na wewe hapa ulipo sasa, na popote utakapoenda kwa wakati huohuo”. Kuanzia pale nikaanza kujifunza jinsi ya kumchukulia Mungu kuwa ni Baba. Unajua sijui kwa wengine ikoje ila mimi nimepata shida sana kumuita Mungu Baba na kumaanisha kwasababu sijawahi kumuona hivyo, na sijawahi kujua kama Baba Mungu anakuwaje.

Kutoka kwa mimi ambaye sina baba wa kimwili kwenda kwako ambaye hauna baba wa kimwili, uwe mwanamke au mwanaume, nakushirikisha mambo yaliyonisaidia kuponya vidonda vya kukosa baba kwenye maisha, vilivyonisaidia kukubali na kuishi na hilo pengo la kukosekana uwepo wake. Na mambo hayo ni haya:

Amini na jifunze kumuona Mungu kuwa ni Baba

Kama vile Mungu alivyonijibu mimi, naamini anamjibu kila mtu anayeumizwa na kukosekana kwa baba wa kimwili kwenye maisha yao, Yeye yupo kila mahali,uwezo wake unazidi hata baba wa kimwili. Tukimwita saa hiyohiyo hana haja ya kupanda gari anakuwa amefika. Ni kweli baba wa kimwili walipaswa kuwakilisha vile Baba Mungu anafanya kwenye maisha yetu, lakini kibinadamu ni vigumu sana kuwa asilimia mia kama Yeye, hivyo mwache nafasi yake ya uBaba aichukue na atimize na kukuonyesha mapenzi yake kwako. Jifunze kudeka kwake,jifunze kumuomba kwa ukaribu kama vile unamuomba Baba na sio Mungu aliye mbali.

Kuna mistari mingi kwenye Biblia inayoengelea jinsi Yeye anavyopenda na anavyotamani tumuone Baba kwenye maisha yetu, na vile Yeye ni Baba kwa wasio na Baba,

  • Zaburi 103:13
  • Warumi8:15
  • Wagalatia 6:4
  • Marko 14:36
  • Luka 12:29-31
  • Mathayo 7:11
  • 1 Yohana 3:1
  • Yohana 14:23
  • Zaburi 68:5

Yani kiufupi Biblia nzima inaonyesha vile Mungu anatupenda kama wanae na anatukubali na anapenda tumuite, tumuone Baba kwetu pia.

Kubali kuwa huo nao ulikuwa mpango wa Mungu kwenye maisha yako

Nilipopitia unyanyasaji wa kijinsia, niliumia sana kwasababu niliwaza na kuamini kwamba kama ningekuwa na baba yangu, angenilinda, nisingepitia hilo. Inawezekana ingekuwa kweli au inawezekana pia isingekuwa kweli kwasababu wapo ambao wamekuwa abused na baba zao pia, lakini katika hili nilijifunza kuwa bado sijakubali kuwa hayupo. Naamiini Mungu anampango na maisha yetu, na anatujua tangu tumboni mwa mama zetu hivyo ni jambo la kuamini kuwa hata kutokuwepo kwa baba zetu kwasababu yoyte ile inayoweza kuwa imechangia, Mungu anajua hilo swala. Na alijua kabla hatujazaliwa na katika yote ni kwaajili ya mema yetu, embu fikiria kama baba yangu angekaa mpaka sasa hivi na kuendelea kuwa mlevi ningepitia yapi? Ni yapi Mungu kaniepushia kwa kifo chake? Au ni yapi kamuepushia kupitia,kwa kupitia kifo chake pia?

Kutafuta uponyaji halali wa hisia na vidonda tulivyonavyo kutokana na pengo la baba

Katika kuumia kwangu nilijaribu mahusiano ili kupona, wewe unatumia nini? Unaweza ukawa unatumia kazi, mapenzi au pombe. Viache ili upate uponyaji wa vidonda vyako kwanza, hata mahusiano ukiingia bila expectation ya yule mtu awe baba yako( kitu ambacho hawezi kuwa) yanakuwa mazuri sana.

Tafuta uponyaji wa vidonda ulivyovipata ukiwa mtoto ambavyo vimekufanya uwe hivi leo. Ambavyo vinaathiri vile unarespond katika hali fulani, vile unakuwa na hasira bila kujua zimetoka wapi, na hili ni rahisi ukijitambua na kujichunguza, ukisoma vitabu vinavyohusu uponyaji wa kihisia, lakini zaidi ya yote unaweza pata ushauri nasaha (therapy).

Hivyo vimenisaidia mimi, vinaweza kukusaidia pia. Lakini pia ukisikia hisia yoyote ile kutokana na pengo lake, usiizime bali iruhusu na uichunguze chanzo chake na huwa unaihisi wakati gani. Hisi hisia zako, zisikilize, ongea na watu kuhusu hilo, andika chini, pata msaada wa kisaikolojia, lia kuhusu kukosekana kwake, na umia ili upone.

Kuwa na marafiki wa jinsia nyingine na jifunze kutoka kwao kuhusu jinsia hiyo

Kwa vile mimi ni mwanamke na nimekuwa karibu sana na mama, iliniwia vigumu sana kuwaelewa wanaume, kwahiyo kuwa karibu na watu ninaosoma na niaosali nao bila kuingiza mapenzi kumenisaidia sana kujua jinsi ya kuishi nao, ningekuwa na baba ningejifunza kupitia yeye, lakini kwa vile hayupo nimejifunza kupitia marafiki na watu wazima wanaume wanaonizunguka. Hakuna aliyeziba pengo lake, na sidhani kama anaweza akatokea ila wamenisaidia katika namna moja ama nyingine na wameboresha maisha yangu kwa uwepo wao kwenye maisha yangu.

Kuwa mtu bora, timiza mapenzi ya Mungu, ishi kwa kusudi ukijua kwamba hata kama angekuwepo angejisikia raha kuwa na wewe kama mwanae.

Mama yangu aliniambia kitu ambacho nimekaa nacho mpaka leo “kama baba yako angekuwepo angejisikia vizuri sana kwa jinsi unavyofanikiwa na jinsi umekuwa bora”.

Na hayo maneno yamenifanya nijisikie katika mafanikio yangu, pia na yeye angefurahia, na niendelee kufanya mema zaidi. Sio kwa ubaya katika kutafuta kupendwa au kuonekana ninafaa, ila katika kukubali kwamba nayeye angefurahia mafanikio yangu.

Zaidi ya yote Mungu ni Baba yako, anaweza kutimiza vyote na zaidi ya vile baba wa kimwili anaweza kutimiza, Baba yako wa mbinguni anakupenda zaidi ya mtu yoyote duniani, na ingawa wao wanaweza kukutelekeza, Mungu Baba hawezi kufanya hivyo.

Takwimu zinaweza kusema zinavyosema, lakini haimaanishi maisha yetu yanabidi yaishie vile takwimu inavyosema watu wenye historia au hali zetu huishia, tunaweza kuwa tofauti, tunaweza kuishi kitofauti, tunaweza badilisha takwimu na historia.

Kutoka kwa asiye na baba, kwenda kwa asiye na baba,
Eunice

7 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป