Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Dondoo za Maisha

Sababu 6 zinazowafanya watu wengi wafeli kwenye maisha

Swali la ‘kwanini watu wengi hushindwa kwenye maisha?’ ni swali ninalojiuliza sana. Ninajiuliza kwasababu mimi sitaki kushindwa, sitamani kufeli kweny maisha. Huwa nawaza, tumeanza shule pamoja, sekondari pamoja , na labda tupo vyuoni pamoja lakini pia labda tunasali wote, kwanini watu wengine hushindwa kwenye maisha na wengine hufanikiwa?
Hushindwa kufikia malengo yao
Hushindwa kufanya kusudi la maisha yao
Hushindwa kuzitunza familia zao na kulea watoto wao
Hushindwa kuwa marafiki wazuri kwa watu wanaowazunguka
Hushindwa kumuwakilisha Kristo vizuri kupitia maisha yao
Hushindwa kuishi maisha waliyoyafikiria walivyokuwa watoto.

Nikifikiria haya yote, nakumbuka maneno ambayo rafiki yangu aliniambia, fikiria umekufa na ukaenda mbinguni halafu Mungu akakuonyesha maisha ambayo ungetakiwa kuyaishi halafu hukuyaishi,utajisikiaje?

Najua nitajisikia vibaya sana. Mimi bado ni kijana mdogo ambaye najifunza na kukua kwenye maisha, ni jambo zuri lakini pia linatisha kwasababu huu ndio muda wa kufanya maamuzi kwa ajili ya kuelekea kule Mungu alikonipangia au pia kuikata hiyo njia na kuenenda ninayoitaka. Huu ndio muda wa kufanya maamuzi mengi sana ambayo yana matokeo si tu sasa lakini pia miaka yote ijayo.

Mungu yeye anatuwazia mawazo mema na anatupa uwezo wa kuchagua njia na maisha tunayoyataka kuishi “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho- Yeremia 29:11”.

Katika kufikiria kwangu nimewaza mambo machache ambayo yanaweza kumfanya mtu kushindwa kwenye maisha, najua kuna mengi lakini tuangalie haya katika picha ya tofauti kidogo.

Ushauri na wapi tunakoutoa
Ushauri sio mbaya, tena kama kuna kitu tunatakiwa tuwe nacho sana ni ushauri. Tunatakiwa kushauriwa sana katika maisha. Kuna msemo unasema kwamba “mtu mwenye hekima hujifunza kupitia makosa ya wengine, bali mtu mwenye akili hujifunza kupitia makosa yake”.

Hii inamaanisha tukiishi kama watu wenye hekima hatutokuwa na haja ya kukosea kila mahali kwani tutakuwa tumejifunza kupitia wengine, ila tukienenda kwa akili tutataka tufeli wenyewe katika kila kitu kwanza. Basi tusikilize ushauri sana ili tusifeli sisi kila mahali, tusikilize ushauri ili tuishi kwa hekima,lakini pia tatizo linakuja pale tunapotoa ushauri,wale watu wanaotushauri.

Pia soma : Mambo ya kuzingatia unapotoa na kupokea ushauri

Usitake kushauriwa kufanikiwa kwa mtu aliyeshindwa katika hilo eneo, na ndio tunapata watu wanaoshauriwa kuhusu mambo ya mahusiano kwa watu ambao hawajaonyesha mfano mzuri katika mahusiano,kiufupi watakuvunja moyo na kukuacha usiamini katika mahusiano pia.
Ushauri sio lazima uwe wa maneno, hata jinsi unavyoona watu wanavyoishi maisha yao ni ushauri tosha.

Pia Soma : Jinsi ya kujua kama upo njia sahihi kwenye maisha yako

Ushauri hautakiwi kukuvunja moyo katika kufanya jambo, ninaposema wenye hekima huangalia makosa ya wengine haimaanishi wakiyaona na wao wanaamini watafeli katika hilo jambo ila wanakaa chini na kufikiria njia ambazo mengine alifeli na yeye anaweza kufanikiwa kivipi pale ambapo yule mwengine alifeli. Tuwe makini tunapotoa ushauri, tusifuate presha ya marafiki, ushauri ni jambo zuri ila watu wanaotupa ushauri ndo swala la kulifkiria kidogo kabla haujaupokea ushauri.

Marafiki tulionao au watakaokuja
Marafiki wanasehemu kubwa kwenye maisha yetu, kuna marafiki ambao wanakuwa karibu zaidi ya ndugu. Tuangalie urafiki kati ya Yonathan na Daudi uivyokuwa na jinsi gani wawili hao walivyokuwa wakiongezeana katika maisha na si kupunguziana.

Je marafiki zako wanakuongozea au kukupunguzia? Katika malengo yako wanakusukuma kwenda mbele au kukurudisha nyuma? Je marafiki zako wanakusaidia kukua katika maisha auhawakusaidii chochote? Kuna muda itabidi uache marafiki fulani fulani kwasababu unapoelekea kwenye maisha hauwezi fika kwasababu upo nao.

Usiongozane na mzigo safari yako katika malengo yako ikawa ngumu.

Nakumbuka kuna kipindi nilimwacha best friend yangu kwasababu niligundua ananirudisha nyuma na ninapoenda siwezi kufika nikiwa naye, watu wote walifikiria nimefanya maamuzi magumu sana lakini nilikuwa najitambua na kujua ninachokihitaji kwenye maisha na kwenye urafiki ambacho nilikuwa sikipati katika ule urafiki.

Kuna msemo unasema “nionyeshe marafiki zako nitakuambia wewe ni mtu wa aina gani”. Lakini pia kuna mwingine unasema “ni heri rafiki mmoja wa kweli aliyekaribu kuliko marafiki 1000 wauongo”. Na Neno linasema ajitengenezeaye marafiki weni anatafuta uharibifu wake mwenyewe. Chagua marafiki zako vizuri, watu unaowaweka karibu kwenye maisha yako, marafiki kwako wasiingie kwenye maisha yako kwa bahati mbaya, hata Yesu aliwachagua watu ambao alitaka kufanya nao kazi hapa duniani na kutimiza kusudi la Mungu. Urafiki kwako usiwe wa bahati mbaya, lakini pia ombea marafiki ulionao na watakaokuja.

Ombea urafiki wako. Nakumbuka nilipokuwa nakuja chuo kwa mara ya kwanza niliombea hata watu nitakaokaa nao kwenye chumba cha hostel lakini pia marafiki nitakaowatengeneza katika kipindi hiki. Kama wewe ni kama mimi, unawaza kuzeeka pamoja na marafiki zako, kwamba utakuwa karibu nao kihivyo, basi ombea sana kwasababu hata shetani atapingana nanyi akiona mnaelekea kuzuri kwa ajili ya kusudi la Mungu. ( Mithali 18:24).

Kutokujaribu na kutokujifunza vitu vipya
Sijajua woga wa kushindwa unatoka wapi, au woga wa kuona aibu kwamba watu watanifikiriaje. Hata nilipotaka kuanzisha hii blogu nilikuwa na maswali mengi sana, na ndio maana sikuianzisha toka mwaka jana,namshukuru Mungu kwamba nimeyashinda hayo maswali na kuanzisha blogu. Kwanini watu wengi hushindwa kujaribu kwenye maisha? na hutoa sababu kama hizi:

  • Nyumbani kwetu hatufanyagi vitu kama hivi
  • Hakuna aliyewahi kufanikiwa kufanya hili
  • Nitaonekanaje kwa watu nikifanya haya
  • Kama nikishindwa je?
  • Muda sina

Jamani tujaribu vitu mbalimbali kwenye maisha, muda tunao. Huo muda tunaoangaia muvi, tungejaribu kupiga gitaa, kusoma lugha nyingine, kuandika hata vitabu au hata kusoma vitabu. Tujaribu mambo mbalimbali hauwezi jua Mungu anakupeleka wapi.

Nilianza mwaka wangu wa pili na chuo wakatangaza kufundisha lugha ya kichina nikasema ngoja nisome, na nilipoanza kusomea nikapata nafasi ya kwenda China kwa wiki tatu. Wakati naanza sikuwaza kwamba nitaenda huko ila nilisoma tu. Tujaribu vitu mbalimbali, tujaribu nafasi mbalimbali jamani. Muda upo, wote duniani tunapewa masaa 24 lakini wengine wanafanikiwa katika hayohayo na wengine wanashindwa katika hayo hayo. Nafasi na wakati hupewa kwa wote, tuzitumie vizuri.
Tuzikamate nafasi kwa nguvu zetu zote kama kuna watu wangetakiwa kuwa na bidii katika maisha ni sisi waKristo.

Kuvunjika moyo na kutokuanza
Unajua hata watu wote waliofanikiwa kwenye maisha walivunjwa moyo, tena sana. Lakini walianza hivyohivyo. Mimi ninaamini hadi sasa Bill Gates anavyotaka kuleta Window mpya watu wanamvunja moyo, lakini anafanya kwasababu anaamini katika kile anachokifanya. Usikubali kuvunjika moyo. Watu wengi wanandoto na mambo ya kufanya kwenye maisha ila wanaacha kuanza na hivyo ndoto zao zinabaki kuwa ndoto kwenye madaftari. Anza, usisubiri upate hela nyingi, anza kidogo, anza hapo ulipo.

Usivunjike moyo kirahisi, anza malengo yako.
Je unataka kumhubiria mtu usisunbiri mpaka usome Biblia yote, nenda na hayohayo uliyonayo.Usisikilize sauti inayokuambia kwamba haujui vingi, kwani si unaweza kumwambia mtu unayemuhubiria ngoja nikafuatilie zaidi, sio lazima uwe na majibu ya vitu vyote lakini anza.

Mahusiano
Sisi kama vijana tunaingiza muda mwingi katika mahusiano kuliko katika ndoto zetu. Tunafocus miaka mitano kwenye mahusiano ambayo tunakuja kuachana, lakini pia tunaingia kwenye mengine miaka mingine mitatu na kuachana. Kwanini hatutumii nguvu kubwa kama hii kwenye ndoto, malengo na kujiboresha sisi kama sisi kama tunavyotumia kuboresha mahusiano tuliyonayo. Sisemi kama hatutakiwi kuboresha mahusiano lakini angalia uzito uliouweka kwenye mahusiano na uliouweka katika kufanya kusudi la Mungu.

Eunice.

9 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป