Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya Chuo

Kama unajisikia vibaya kwenda diploma wakati wenzio wanaenda degree

(Tembelea maishayachuo.com kupata makala, dondoo na msaada kuhusu chuo kutoka kwa waliomaliza vyuo)

Kwenda diploma wakati watu wote uliosoma nao wanaenda kusoma degree chuoni ni kitu kinachoumiza na kukufanya ujisikie vibaya. Na muda mwingine hao watu unaweza kuwa nao chuo kimoja hivyo mnaonana.

Inauma aisee.

Kwa wale wanaoenda kusoma diploma chuoni, wakati wengine mliokuwa nao wanaenda degree ningependa niwatie moyo kwa mambo haya machache;

Kila mtu kwenye maisha ana safari yake

Japokuwa mlianza wote shuleni, kila mtu kwenye maisha ana safari yake na jinsi mambo yake yatakavyomwendea. Hata mtakaokuwa wote diploma mkimaliza wengine wataendelea, wengine wataenda kazini, wengine watapata kazi. Kila mtu anasafari yake, hivyo sasa hivi inabidi ukubali kuwa safari yako ni tofauti na ya wengine, na hivyo ndivyo maisha yalivyo.

Maisha siyo mashindano

Kwa kwenda diploma sio kwamba umeshindwa, kwa wao kwenda degree sio kwamba wameshinda. Maisha sio mashindano. Maisha ni safari.

Kila mtu anatembea peke yake kwenye hiyo safari, hakuna mtu anayeshindana na mwengine kwenye hiyo safari, hivyo usijisikie kama umeshindwa kwenye safari ya maisha yako, muda mwingine hivyo ndivyo safari yako ya maisha ilivyopangwa kuwa.

Pia Soma: Kushindana kwenye maisha na jinsi inavyotuathiri

Hauwezi jua kusudi lako huko

Huwezi jua unapoenda diploma Mungu amekupangia nini huko, hauwezi jua njia hii unayopitia ina nini kwaajili yako na maisha yako, labda diploma utakuja kupenda kusomea jambo jingine kwaajili ya degree? 🤷🏿‍♀️ Hakuna ajuaye kesho.

Muda mwingine mipango yetu, mambo tunayoyataka hayatokei kama tunavyotaka yawe ila maisha inabidi yaendelee

Kuliko kukaa na kujidharau, kujihuzunikia, muda mwingine ni jambo zuri kukubali kuwa sisi tunapanga, Mungu anacheka. Mipango tunayopanga muda mwingine haiendi kama tunavyotaka iende na hivyo hatuwezi kuilazimisha, mambo mengine yako nje ya uwezo wetu wa kuyafanya yatokee.

Sio jambo baya kusoma diploma, sio jambo la kudharaulika au kudharauliwa au kujidharau. Ni jambo la heshima kusoma, level yoyote ile unayosoma. I’m so proud of you kwa kwenda kusoma.

Pia Soma : Kama unahisi umechelewa kwenye maisha

Kwa unayeenda kusoma diploma, nimefurahi kuwa umepata chuo na unaenda kusoma chuo, kwa vile haijalishi matokeo yako kidato cha sita yalikuwaje maisha lazima yaendelee na wewe kwenda kuendelea kusoma kunaonyesha kuwa unajitahidi, na uko tayari kuyafanya maisha yaendelee.

Ni matumaini yangu utabadilisha vile unavyojiona na kujiponya vile unavyojisikia, maana hilo ndio jambo kubwa sana linaloweza kuathiri kujiamini na maisha yako diploma, suijali watu wanasemaje, watu kazi yao ni kusema, usiku kulala, mtu anayesema jambo fulani muda mwingine linaonyesha vile mtu alivyo na sio wewe ulivyo.

Natumai utapona na kujisikia vizuri kwa level hii uliyopata kusoma kiasi kwamba maneno ya mtu au watu wanavyokufikiria haikuumizi. Ila inakutia moyo kuendelea maana safari yako ya maisha ni tofauti na yao.

Usijisikie vibaya unapoenda diploma wakati wenzio wanaenda degree

Eunice

(Kupata dondoo hizi na nyingine nyingi, pata kitabu cha Your Guide to University Life, kinachokusaidia kupata majibu ya maswali na kila jambo unaloweza kupitia kama mwanachuo, kwenye kitabu hiki utapata ushauri kutoka kwa waliomalia chuo kuhusiana na maswala ya pesa na biashara, urafiki, supp, carry, disco, mahusiano, migomo, mambo ya kufanya ukipata skendo chuo, jinsi ya kudili na walimu wasumbufu, ushauri wa mitindo, jinsi ya kujiandaa na maisha ya mtaani ukiwa chuo na mada nyingine kedekede, kukipata kitabu hicho kwa Tsh 5000/= tu, bonyeza hapa)

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป