Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Mahusiano

Jambo la muhimu kulizingatia unapokuwa kwenye mahusiano

Hakuna kitu kizuri kwenye maisha kama mahusiano, na hakuna kitu kinachoumiza pia kama mahusiano. Katika eneo hili watu walifanikiwa kusogea mbele kwenye maisha na kutimiza ndoto zao, hapa hapa pia watu waliharibu ndoto zao na maisha yao. Hivi karibuni nimejifunza jambo fulani ambalo ni muhimu kuliangalia ili kuona mwelekeo wa mahusiano yako, na katika makala hii ningependa kukushirikisha jambo hilo, nalo ni;

Kuangalia kama uliyenaye anaweka nguvu sawa kwenye uhusiano kama wewe unavyofanya

Tuwe wakweli, hakuna kitu kinachochosha kama kujihisi wewe peke yako ndio umewekeza nguvu kwenye uhusiano wenu kwenda. Hii inaweza kuwa kwasababu yeye hajui kuwa kuna vitu unavitegemea avifanye kwako au inawezekana ni kwasababu hajali tu kuwekeza nguvu kwako au ni mvivu au labda ameona mpo pamoja anaona atulie sio muhimu tena kuwekeza nguvu kama wakati bado anakutafuta hamjaingia kwenye mahusiano.

Hili ni jambo ambalo hutokea kwenye mahusiano na ni muhimu kuliongelea kabla haujafika kuchoka. Ukiwa kwenye mahusiano na mtu unahitaji kuona pia kuwa anawekeza kwenye uhusiano wenu kama vile wewe unavyowekeza, uhusiano ni wa watu wawili hivyo ni muhimu mkawa timu inayofanya kazi pamoja. Inaweza isiwe mnafanya mambo sawa kwenye mahusiano lakini ni muhimu kuona kuwa mwingine pia anavitu analeta kwenye uhusiano na sio peke yako unayejishughulisha kupanga na kuandaa vitu kwaajili ya uhusiano wenu.

Watu wengi hasa wanawake wamefundishwa na kukuzwa kujitoa sana ili kupendwa, wanaume pia hufanya hivi likija kwenye swala la kutoa pesa. Ukweli ni kuwa upendo haununuliwi, na si lazima utoe vitu kwa namna ya pesa au nguvu zako ili upendwe au uonyeshe upendo. Ninachoongelea kwenye hili jambo ni kule kuona kwamba na mwenzio pia yupo ndani ya uhusiano huu kama vile wewe ulivyo.

Yani kama ni kwenye swala la kupanga mkutane, basi na yeye hushiriki siku moja moja kupanga sio kila siku wewe ndio unaanzisha hilo swala, basi kama mnafamilia wewe unashiriki malezi, yeye anashiriki kuleta hela, si lazima mfanye kitu sawa ila ni muhimu kuona kuwa na yeye anawekeza kwenye uhusiano wenu, kuna kitu analeta na si tu kuwepo na kutegemea wewe ufanye kila kitu. Ukiwa unategemewa ufanye kila kitu unaweza kuchoka na baadae kuwa na hasira na yule unayempenda maana unahisi unabeba uhusiano wenu wote mabegani mwako na bila wewe kuhangaika labda kungekuwa hakuna kitu kinachoendelea. Jitahidi kuangalia hili na kuliwasilisha kwa mwenzio, mahusiano ni mawasiliano, ongea vile unavyojisikia mpate suluhisho. Inawezekana mkakubaliana huyu apange hili na yule afanye lile, au akakwambia kuwa hajisikii kuwekeza kwenye huu uhusiano maana haoni umuhimu wake, ila bora kujua na kuwasiliana kuliko kuumia kimya peke yako kwasababu ya kuchoka ndani ya penzi.

Ushawahi kujihisi kuchoka ndani ya penzi?

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป