Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku

Kwanini siamini kwenye kuweka malengo ya mwaka mpya

Tarehe 30 December mama aliniita asubuhi sana, tupange.

Tupange mwaka 2020 tunataka kufanya nini.

Nikaomba udhuru kwanza niende msalani.

Nikaomba tena udhuru niweke simu chaji.

Nikajizungusha, nakujizungusha, nikamkuta bado mama ananisubiri tuweke malengo ya mwaka mpya.

Mimi huwa kama kitu sipendi kukifanya na siwezi kukuambia ukweli, huwa najizungusha.

Na kwa kujizungusha kwangu ndipo nilipogundua kumbe sipendi kuweka malengo, na pia sioni umuhimu wake.

Sio kwamba ni vibaya ni vizuri, kwa watu ambao huwa wanayafanyia kazi.

Ila kwa mimi ambaye ninakuwa na mizuka ya kushtukizwa na kufuata mkumbo kwasababu kila mtu anafanya, tarehe 10 tu Januari nakua nishayaacha malengo, naishi tu kama mtu wa kawaida, ambaye anajutia na kusubiri mwaka uanze tena ili aanze upya.

Nina mambo ambayo natamani yatokee mwaka 2020 na nimeyaandika chini kabisa, lakini hata yasipotokea sina shaka maana najua hayo yatakayotokea ndio yatakuwa malengo na mipango ya Mungu kwa maisha yangu.

Huwa siamini kwenye kuweka malengo ambayo yanatakiwa yaanze tarehe 1 Januari kufanyiwa kazi kwasababu;

+++ Malengo yanaweza yakatimia au yakaanza kufanyiwa kazi muda wowote sio lazima tu iwe tarehe 1 Januari ndo yaanze kufanyiwa kazi

+++ Kukosa maandalizi, huwa tunaweka malengo makubwa ambayo hayana maandalizi, halafu tunajisikia kama watu waliofeli kwenye mwaka mzima jambo ambalo sipendi kujisikia hivyo. Unapanga kupungua uzito, ila unataka tarehe 1 ndo uanze kuufanyia kazi, haujaweka mikakati, namna na hatua utakazozifikia kufika huko, ikifika tarehe 10 motisha inapotea, unakua umeshauzoea mwaka unaachana na malengo yako. Unaanza kujiona wewe ni wa kushindwa, hakuna ulilowahi panga likafanikiwa.

+++ Malengo yangu muda mwingi huwa hayatimii. Kuna msemo unasema,’ sisi tunapanga, Mungu anapangua’. Na wazungu husema, ‘we plan, God laughs’. Ndo hayo hayo yakwamba yanayotokeaga kwenye mwaka ni yale tu Mungu ameplan. Hivyo natamani jambo fulani litokee, ila lisipotokea pia haina shida, mwezi wa 12 siwezi kujiona nimeshindwa, maana pia nitakuwa nimeshinda kwa kupata yale yaliyotokea.

Hivyo badala ya kuweka malengo ya mwaka mpya, huwa ninaanza popote ninapotamani kuanza jambo, sio lazima iwe mwaka mpya. Hata ikiwa October nalianzisha.

-Huwa ninaweka mikakati ninayoweza kuitendea kazi kwaajili ya jambo ninalotaka kulifanya, siku zote ni sawa kwangu, tarehe tu ni tofauti ila masaa ni yaleyale 24. Hivyo jambo ninaweza kuanza kulifanya hata Alhamisi, ili mradi tu nataka kulifanya.

Lakini pia mwisho wa mwaka huwa nafanyaga ukaguzi wangu, kujikagua jinsi nilivyokua, wapi natamani kujiona naenda na kumshukuru Mungu kwa mwaka uliopita, na kumuomba yote ambayo amepanga yatokee mwaka mwingine, yatokee vile vile, na kama yale ninayoyatamani yatokee ni moja ya mambo anayotamani yatokee kwangu pia ni sawa, kama sio anayotamani pia ni sawa.

Na hizo ndo sababu za kwanini siamini kwenye kuweka malengo ya mwaka mpya.

Heri ya mwaka 2020!!

Eunice

2 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป