Pata majibu ya maswali yako yote kuhusu maisha ya chuoni na changamoto zake

young muslim black woman in headscarf standing against marble wall
Afya Guest Post
Eunice Tossy  

Mambo 4 ambayo huzidisha maumivu kwa mtu anayepitia matatizo

Matatizo hutokea kwa kila mtu, lakini tofauti zipo kwenye kuyakabili matatizo hayo. Kwa mtu ambaye amelelewa na kuzoea kukabiliana na matatizo tangu mtoto mdogo huwa mtu mzima mwenye ujasiri na mwenye uwezo wa kuyakabili matatizo maishani mwake. Kwa mtoto ambaye tangu utotoni mwake alizoea kusaidiwa kwa kila kitu yaani ni mtoto wa kudeka tu kila kitu hufanyiwa, hupata wakati mgumu sana kuibuka baada ya kuanguka.

Wapo ambao wakipata matatizo huanza kulia, wapo hukaa na kulalamika, wapo hukaa na kuanza kuweka sura za huzuni ili kuonewa huruma na jamii. Wengine hujiona wenye mikosi, wengine wanajiona wamerogwa, wengine hujichukia kwa wingi wa matatizo wanayopitia 

Mambo ambayo hayawezi kukusaidia unapofeli maishani ni 
1.KUISHI KWENYE MAKOSA YAKO YA ZAMANI

Pia Soma : Jinsi ya kujisamehe mwenyewe maishani

Kila mtu huwa ni mwenye kukosea sana katika maisha. Kuna watu ambao huwa wakikosea huanza kuwalaumu wengine kama sababu ya kukosea kwao, wao huwa wanasifa ya kukosoa sana makosa ya wengine. Huwa wanayafanya makosa ya wengine kuonekana makubwa kuliko uhalisia. Huwa wanakukosoa kwa lugha ambayo inalenga kukufanya ujione mnyonge, ujidharau. Wanalaumu sana kila tendo lako hivyo hukufanya ujione mwenye makosa makubwa sana kiasi kwamba utaona huwezi kujirekebisha.

Kwanza kabisa huwezi kumzuia mtu kuwa na maoni tofauti na yako, kwa chochote utakachofanya kuna mtu atasema tofauti na vile unatarajia. Watu wengi watakusema kwa makosa yako kiasi kwamba utajiona mwenye kukosea sana kuliko wengine. Hakuna mtu ambaye hafanyi makosa duniani hivyo haijalishi utakosolewa kiasi gani hao wenye kukosoa sana makosa yako pia huwa wanakosea sana ila wao wakifanya makosa huelekeza lawama kwa watu wengine. 

Kubali kuwa wewe sio malaika ni binadamu tu hivyo sifa ya binadamu ni kukosea na kama hutaki kukosea maana yake huwezi kujifunza chochote. Ukitaka kumfurahisha kila mtu ni wewe utabaki na huzuni. Huwezi kuwa kipenzi kwa kila mtu wapo watakuchukia kwa sababu unapendwa na watu wengine

2.KUTAZAMA SANA MADHAIFU YAKO 

Watu wengi huwa wanabaki na maumivu moyoni kwa sababu huwa wanatumia muda mwingi kufikiria sana makosa yao kuliko mazuri yao. Unaweza kuwa umesema neno sio zuri lakini umetamka maneno mazuri mengi tu hivyo huwezi kufuta makosa yako bali unaweza kujifunza kupitia makosa yako. Ukitazama madhaifu yako utakuwa mnyonge sana. Watu wengi hawafikirii kabisa hivyo hutumia muda mwingi kulalamika kuliko kutafuta ufumbuzi. Hivyo jitenge na watu wenye mtazamo hasi kwa sababu haijalishi utakuwa na ujasiri kiasi gani unapokaa na watu hasi hasa kipindi kigumu utazidisha maumivu badala ya kuona nafuu. Ondoa fikra za kutaka kila kitu kiwe 100% ndiyo ufurahie maisha. Kila mmoja wetu ni dhaifu bila kujali umri, cheo, kipaji, umaarufu na kipato, hivyo bila kujali mtu yukoje bado hufanya makosa.

Makosa hutupa uzoefu na uzoefu hutupunguzia makosa. Acha kujilinganisha na wengine, ondoa hofu kuwa watu watasema nini juu ya makosa yako. Huwezi kuwa na furaha nyakati ngumu kama kila dakika unatazama madhaifu yako. Huwezi kubadilisha sura yako ila unaweza kubadilisha namna unavyo dhihirisha sura yako kwa wengine kwa kutabasamu au kwa hasira.

Makala inayoendana na hii : Mambo yakufanya unapopitia magumu

african american couple having conflict at home

 
3 . KUJILAUMU NA KULAUMU WENGINE

Ikiwa unapitia kipindi kigumu na kwenye maumivu ni kosa kubwa sana kujilaumu au kuwalaumu wengine
Huwezi kubadilisha kilichokwisha tokea kwa kulaumu wengine au kujilaumu wewe. Wapo watu huteseka kwa sababu walipata sifuri shule, wapo hujichukia kwa sababu ya muonekano wao, wapo hujilaumu kwa sababu walifanya makosa sana miaka ya nyuma. Unapomlaumu mtu yeyote huwezi kusaidia au kupunguza chochote kwenye matatizo yako. Lawama humzuia mtu kuona kama anao wajibu wa kutekeleza majukumu yake. Ukimlaumu mtu huoni kosa lako huoni pa kujirekebisha, huoni dosari zako wala huoni sehemu unaweza kufanya maboresho.


4.OVERGENERALIZATION 

Kuamini kuwa kwa sababu upo katika kipindi kigumu basi huwezi kupata nafuu. Hapa unazidi kuumia mwenyewe kwa sababu huoni kesho yako ikiwa nzuri. Wapo waliopoteza pesa basi huona hawawezi kupata pesa tena, wapo hujiona wa mwisho kwa kila jambo, wapo hujiona wamezaliwa ili kuteseka tu. Kwanza kabisa acha kutazama mabaya katika maisha yako. Wengine hujiona wamezaliwa kwa bahati mbaya na kutamani umri wao ungekuwa tofauti. Wapo wanawake wanahasira kwa sababu umri ni mkubwa na hawapo kwenye ndoa hivyo wanatamani wangezaliwa kipindi tofauti au wangekuwa na muonekano tofauti. Kutamani haisaidii chochote huwezi kuwa mrefu au mfupi au kuzaliwa nchi tofauti kisa tu unatamani kuwa hivyo. 

Ondoa kauli za “why me” kisha weka kauli “what now”

Jiulize nini ufanye uondoke kwenye maumivu sio useme kwanini wewe ndiyo unaumia. Bila kujali ugumu wa maisha unaopitia kuna watu wanateseka kukuzidi. Unaweza kuwa unalala njaa, sawa je unawaonaje waliopo hospitalini wanaopumulia mipira? Sawa huna kazi lakini unapumua, je unawaonaje waliopata ajali na kuvunjika miguu yote? Sawa biashara ni ngumu lakini unakula chakula kizuri, je unawaonaje ombaomba masokoni? Watu wasiokuwa na huruma huongoza kwa kuteseka sana kipindi kigumu cha maisha yao.

Imeandikwa na Psychologist Said Kasege, Temeke, Dar es Salaam

+255766862579+255622414991

Share Your Thoughts With Me

Muongozo wa Maisha ya Chuo

Je unaenda chuo? Au upo chuo?

Pata majibu ya maswali yako yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuoni hapa, pata dondoo na ushauri kwenye mahusiano, maswala ya pesa na biashara, afya yako chuoni, mitindo, skendo za chuo, kudili na walimu wasumbufu na ada mbalimbali zinazowahusu wanachuo kwenye kitabu hiki

Bonyeza Hapa Kupata Kitabu Hiki
Translate »