Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Being African

Mambo 6 kuhusu uongozi niliyojifunza kutoka kwa rais Magufuli

WaTanzania tumepata pengo kubwa sana kutokana na kifo cha Mhe Magufuli, ni mara ya kwanza kiongozi anakufa akiwa bado yupo ofisini kama rais wetu, ni mara ya kwanza anaapishwa rais mwingine baada ya kifo cha aliyekuwepo madarakani, ni mara ya kwanza kama taifa kupitia hili, na kwa moyo niwape pole waTanzania wenzangu, naiona huzuni iliyopo kwenye nyuso zetu na mioyo yetu na jinsi tunavyoendelea kuwa na tumaini na kuendelea mbele kwa nguvu kama vile ambavyo mhe rais aliyetutoka alivyokuwa anatusisitiza tuwe.

Njia pekee ya kumuenzi kiongozi wetu ni kuwa natumaini na kuendelea katika njia aliyotuonesha, kutosahau yale mema aliyotuambia, alitufanya tujiamini sana na tuamini kuwa tunaweza na tuna maliasili zinazoweza kutusaidia kuendelea, sio tu kwa maneno, Magufuli alifanya kwa matendo, katuonesha inawezekana pia mbali tu na kutuambia kwa mdomo. Likija kwenye swala la uongozi haya hapa ndio niliyojifunza kuhusu uongozi kwa kumuangalia yeye anavyoongoza;

  • Uongozi ni kujitoa kwaajili ya unaowaongoza

Kwa matendo na maneno mara kadhaa tulikuwa tunaona alivyokuwa anajitoa, hata kuendelea tu na kazi baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali inaonesha ni jinsi gani aliwekeza akili na nguvu zake kwenye kuboresha maisha ya mTanzania.

Uongozi wake haukuwa wa kukaa ofisini, bibi yangu ananisimulia jinsi Magufuli alivyoenda kuwatia moyo na kuwaambia watu waache kuuana kwa uchawi kwenye kijiji ambacho kwa maneno ya bibi yangu, hakuna kiongozi aliyewahi kufika. Kila mtu anamkumbuka kivyake, ila mimi naona kiongozi ambaye alijitoa kwa asilimia mia kwenye uongozi wake kwani hata wajibu hauwajibiki kwa aliyoyafanya mwingine unawajibika kwa uliyoyafanya wewe kwenye muda wako na huko kuwajibika ndiko tulikokuona kwake, nitaendelea kumuenzi kwa kujitoa kwake.

  • Kubadilisha namna watu unaowaongoza wanavyojiona na kuwawezesha

Nilipokuwa Mbeya mwaka ambao Magufuli alichaguliwa kwa mara ya kwanza kipindi nipo chuo, mchungaji alisema kuwa anampenda sana Magufuli kwasababu katika viongozi wote waliowahi kuiongoza Tanzania yeye pekee ndio alisema Tanzania sio maskini. Nchi za Afrika sio maskini, tuna maliasili, tuna idadi ya watu wengi sana ambao ni mali watu pia, tuna akili, kwahiyo sio umaskini ambao ni tatizo linalosababisha au kuchelewesha sisi kuendelea.

Magufuli aliondoa hayo mawazo hasi ambayo tulikuwa nayo, jinsi tulivyokuwa tunajiona kama waTanzania, kama waAfrika. Alitupa ujasiri, kujiamini na kujaribu. Kiongozi ana kazi ya kuwawezesha anaowaongoza, ili wajue kuwa wanafya maendeleo pamoja, anawajibu wa kubadilish na kuondoa mawazo chanya ambayo watu wanayokuhusu wao, muda mwingine unakuwa na uwezo ila haujui au haujafikia kuishi katika ule uwezo, kiongozi anatakiwa kukutia moyo na kukufanya ujione katika mwanga chanya ambao anauona kwako.

Magufuli pia naona amebadilisha jinsi watu wanavyochukulia uongozi, kabla yake viongozi wengi tukiwachagua walikuwa sasa wao wanakaa juu yetu na kutudharau mpaka kipindi cha kampeni, yeye alisisitiza sana kuwa yeye ni mtumishi wetu, yeye yupo pale kututumikia, mpaka sasa viongozi wengi nao wameanza kusema hivyo hivyo, hayo mabadiliko ya fikra ya namna viongozi wanavyojiona unapowachagua huathiri pia yale wanayotutendea au kutuona sisi wananchi.

  • Kuwa na maono

Maendeleo yoyote unayotaka kuyaleta hata kwenye maisha yako ni lazima uwe na maono. Inaweza ikachukua muda mfupi wa kujibana na kujinyima ili ufikie kule unapotaka kwenda, ila inabidi tu ufanye hilo au upitie kipindi hicho ili ufikie maendeleo. Kiongozi ni lazima uwe na maono, sio tu uwe muongeaji na sio mtekelezaji, ukiwa na maono matendo pia yanahitajika. Jambo hili nimejifunza kwake, alikuwa na maono na aliyafanyia kazi na muda mwingine alifanyia kazi haa yale yaliyokuwa yakiongelewa tu bila kufanyiwa kazi na viongozi waliopita.

  • Kujisikiliza na kuamini hekima zako

Kuongoza nchi sio mchezo au kazi ndogo, uamuzi wako sahihi unaathiri maisha ya wengi, uamuzi wako mbaya pia unaathari kwenye maisha ya wengi. Kuna mengi ambayo Magufuli aliyasema wakati ambao atu wote walikuwa wanaenda kushoto na baadae ikaja kuonekana ni sahihi. Mfano mzuri ni jambo la Corona.

Kwamba unauwezo wa kusikiliza nafsi yako na kufanya uamuzi ambao uko tofauti na watu wote na bado ukajiamini kusimama ni jambo ambalo kama binadamu inabidi tulifikie na sifa ya kiongozi ni kuona mbali, kuweza kufanya uamuzi wa haraka na kusimamia uamuzi wake. Maono na kuona mbali ni sifa muhimu kwa kiongozi kuwa nayo, lakini pia kuishi katika njia inayokupeleka kwenye maono yako (njia sahihi) na kuamini maono yako kiasi cha kufanya maamuzi ambayo hata kama watu hawaoni kule uliko ona wewe wataona baadae ni jambo la msingi zaidi.

  • Kuwa mtu wa kuthubutu na kujaribu kupita njia ambayo wengine hawajapita

Magufuli alikuwa ni kiongozi mwenye uthubutu, kiongozi mwenye utendaji. Kwa muda mrefu kama waAfrika tulihitaji kiongozi mwenye uthubutu na kutuweka waAfrika mbele na maendeleo yetu mbele kama yeye alivyofanya na ndio maana hata msiba wake umetuumiza sana, umetugusa sana na inaoneakana kwa jinsi wananchi tulivyoomboleza.

Uthubutu wake wa maneno lakini pia na vitendo ulidhihirika katika miradi aliyoifanya pia, alipita na alifanya yale ambayo hakuna kiongozi yoyote aliwahi kufanya huko nyuma. Kiongozi ili kuleta mabadiliko popote unapoongoza lazima uwe na uthubutu, uweze ku-take risk.

  • Kujua kuwa hautomfurahisha kila mtu ila bado endelea kufanya yanayohitajika kufanywa kwa faida ya wengi

Unapokuwa kiongozi hauwezi kumfurahisha kila mtu, kuna maamuzi yenye faida ya wengi yatawaudhi wengine kutokana na labda namna walivyozoea kuishi hapo kabla au sababu mbalimbali binafsi, lakini kama kiongozi kutokubalika unapofanya vitu sahihi isikuvunje moyo au kukufanya uache maono yako, ukitaka kufurahisha kila mtu huwezi kufanya lolote maana kila unalofanya linaweza kumkera huyu na kumfurahisha huyu, hivyo fanya tu yale unayoona yanafaidisha wengi, yale unayoona yako sahihi.

Pole sana kwa msiba, Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amen

Na sisi tuliobakia hasa vijana sasa tuna mfano chanya wa jinsi ya kuleta mabadiliko, tuna mfano chanya wa uongozi ambao unafanya kazi kwa uzalendo, njia nzuri ya kumuenzi ni kushirikiana pamoja na kuwa wazalendo wenye kuijali nchi yetu, maendeleo yake na wananchi kama yeye alivyofanya.

Napenda kuchukua nafasi hii pia kushukuru kwa maisha yake, kwa zawadi hii kubwa kwetu. Maisha yake yamekuwa baraka kwetu, japokuwa tuna huzuni ya kuondoka kwake ila alama ambayo maisha yake yameacha mioyoni mwetu na kwenye nchi yetu ni kubwa sana, anaendelea kuishi mioyoni mwetu.

Eunice

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป