Pata majibu ya maswali yako yote kuhusu maisha ya chuoni na changamoto zake

Imani Maisha ya kila siku
Eunice Tossy  

Mambo yanayotokea kanisani yanayonipa maswali magumu kuhusu ukristo

Kanisa ni sehemu ambayo wengi huenda kutafuta majibu ya matatizo yao, kutafuta ushauri na hivi karibuni nimekuja kuona kanisa kama sehehmu ambayo wengi huenda kukimbia shida zao, au kwa usahihi zaidi niseme therapy, tunapitia shida nyingi duniani muda ule wa kanisa unakutia moyo, unakupa tumaini unaondoka na nguvu mpya ya kukutana na wiki mpya yenye changamoto.

Ni kama kutiana moyo au kujipa moyo kwa kurudia maneno yenye kutia moyo ya mchungaji / nabii.

Siwezi kudanganya napata shida sana na ukristo na hivi karibuni nimekuwa na maswali mengi kuliko majibu kuhusu ukristo, kuna mambo mengi yanayotokea kanisani ambayo yananifanya nijiulize maswali haya, na leo naenda kushea mambo hayo.


— Kwanini wachungaji siku hizi wanataja sana shida na kuwa wanaweza kuzitatua kuliko kumuinua sana Kristo makanisani?

Dunia yetu inashida nyingi na wengi wanatafuta suluhisho la shida, magonjwa, uponyaji, utajiri hadi safari za ulaya ambazo vyote hivi na zaidi wachungaji huahidi kutoa kupitia Yesu ambaye atakuwepo kwenye maombezi (atakuwepo kama vile yeye sio ndio chanzo ni kama amealikwa tu kwa muda kutatua hayo).

Sielewi.


— Mbona wachungaji na manabii wanatumia sana shuhuda kama kuonesha uwezo wao wa kufanya yale wanayoyatangaza?

Kwenye mitandao ya kijamii, ukiwa na followers wengi ni alama ya kuwa bidhaa yako labda iko vizuri au inapendwa. Kanisani ukiwa na shuhuda ni alama ya kuwa unaweza kuponya. Na watu wanakuamini maana wengi wamekushuhudia wewe ndio wewe, kama kweli Mungu yuko na wewe au ndio unauwezo. Ushuhuda umekuwa ni marketing strategy.

Kwanini wachungaji wanashea shuhuda kwa kujisifia utafikiri wao ndio wamefanya?

Muda wa kuabudu na kuhubiri ni mfupi, muda wa ushuhuda ni nusu ibada na maombi ya kutatua shida za watu


— Manabii hawajali sana watu kuacha dhambi kwaajili ya utakatifu au maisha yao zaidi ya pale wanapowaona, ila wanasema dhambi zako ndio zimekufanya usiwe tajiri

Niseme tu kuwa nilipokuwa nakua watumishi walikuwa wakisoma mistari mingi na kuongea maneno yao wenyewe machache, sasa hivi wachungaji wanamaneno mengi, mstari mmoja tu ambao unatafsiriwa pande zote za dunia kuelezea ujumbe ambao ni kuwa shida zako zinatokana na kuibiwa nyota au dhambi au kwa kuwa haujakutana na huyo nabii.


— Watumishi kupokea mamilioni ya sadaka kutoka kwa wahudhuriaji maskini ambao wanaahidiwa utajiri kwa kumpa mtumishi hela au kununua bidhaa zake.

Afrika sio maskini, utajiri wetu wa akili na mali umetekwa na wachache, upo pia makanisani na kwenye mikutano ya injili. Mamilioni hupatikana kujenga kanisa, kupanua kanisa na kuweka geti wakati kuna watoto wa mitaani wanaopita na kulala nje ya kanisa.

Gari la milioni hununuliwa mchungaji wakati watoaji wana watoto ambao hawana hela ya kuwapa kwenda shule hivyo wanabidi wakope hela za shule za watoto.

Niulize je tunaabudu wachungaji?

Je kumpa mchungaji kila kitu wewe kuishi kwa shida ndio Mungu amesema njia ya kukuondolea shida?

Kwanini wachungaji ni matajiri wakati wanawashirika ambao jana usiku hawajala? Kwanini washirika wanawasaidia wachungaji kuwa matajiri kupitia mifuko yao?

Je baraka hununuliwa?

Je Mungu anapenda mchungaji aishi vizuri kwa raha mstarehe wakati wewe ukope ili kulipia maisha yake?

Je kumfurahisha na kumtajirisha mchungaji ndio kumfurahisha na kumtajirisha Mungu?

Pesa na dhahabu si mali ya Mungu tayari? Unamtajirishaje tayari, unampaje sana unayetegemea akupe?


— Je ukristo unatumika tu kutuondolea shida za hapa duniani na kutupa utajiri halafu basi mbona watumishi wasiku hizi hawatuambii kuhusu siku za mwisho na safari ya mbinguni au imeghairishwa tunabaki duniani hivyo inabidi tujikusanyie hapa hapa?


— Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la wachungaji wengi wakiongelea kusafisha na kurudisha nyota, mstari unaotumiwa ni ule wa mama jusi na hapo mchungaji ataongea masaa mawili jinsi gani nyota yako imeibiwa na haufanikiwi kwasababu hiyo. Miaka michache iliyopita maswala ya kurudisha nyota nilikuwa nayaona kwenye mabango ya waganga ila leo wachungaji wanafanya madhabahuni kwa kutumia mstari mmoja ambao hauongelei hilo swala hata.

Kwa matatizo mengi yanayotukumba binadamu, wengi wetu hufuata dini kutaka kujua jinsi ya kuyatatua, kupata tumaini au kujua tu ipo siku haya mambo yataisha tutaenda mbinguni kula raha.

Wachungaji wengi sasa hivi pia wanatumia shida hizi hizi kuleta vitu vingine ambavyo kibiblia havina maelezo yake, mimi sijasomea shule ya uchungaji, ila swala la mama jusi kufuata nyota ni swala la astrology, ukifuatilia astrology kwa undani wao husema kila mtu anapozaliwa kuna namna nyota zinajipanga na ndio maana mama jusi waliifuata ile nyota walikuwa astrologers, waliona upekee wa Yesu kupitia nyota yake alipozaliwa, nyota haiwezi kuibiwa ni vile tu sayari zinavyojipanga unapozaliwa. Unaweza kufuatilia vizuri kama hizo horoscopes na kadhalika ni mambo ya sayansi ya astrology.


— Kwanini tunapanda mbegu?

Nikija kwenye kupanda mbegu, ni jambo ambalo kusema ukweli sijawahi kuliona kibiblia lakini watumishi siku hizi wanalitumia sana.

Kwahiyo mimi ambaye sikupanda mbegu shida zangu zinatokana na hilo? Ni kama watumishi wanatumia shida na kutokufanya wanayotaka niyafanye ambayo yanawapa wao hela kama ndio sababu ya mimi kuwa na shida. Mimi siamini kama Mungu anashawishika kwa wewe kumpa hela, Mungu hapendi rushwa.


— Kumtenga mtu kuna msaidiaje? Na wakati kuna wengi tu ambao hawajatengwa kwasababu dhambi zao hazijulikani.

Ukristo wetu unawasaidiaje watu kushinda dhambi zinazowasumbua?

Tukiwatenga kunawasaidiaje? Kiroho na kimwili?

Binadamu tunapenda kukubalika ataonesha amebadilika mbele zetu lakini je mabadiliko ni ya muda kama tungemuonesha upendo?

Ukristo ni kutembea na kuishi na watu kwa vipindi vyote kwa upendo wa Kristo.

Kuwatenga ndio jambo ambalo Kristo angefanya?

Kanisani kuna dhambi kubwa na ndogo, danganya kila siku ila usifanye uzinzi, huu unafiki tutaacha lini?

Kwanini watu wote wasikaribishwe tu kanisani?

Watu wanaodharauliwa kwenye jamii zetu na kukosa haki ndio Yesu angekuwa anawapigania sana ila kanisa ndio linawafungia milango na kuwapa khanga ili wakutane na Kristo, kumbuka Yesu alifutwa miguu na kahaba hakumpa khanga, Yesu pia alisema ng’oa jicho lako sio umpe mtu khanga.


— Kwanini tunachangishana sana kujenga kanisa wakati;

1) hatujengi vile vigezo Mungu alivyosema kwenye agano la kale?

2) hiyo hela mamilioni na mamilioni inaweza ikatumika kusaidia jamii, Biblia inasema sifa za dini ya kweli na hakuna hata sifa moja ambayo ni kukaa kwenye jengo zuri, sifa zote zinahusisha kanisa kwenda nje kuwatumikia wafungwa, wagonjwa nk kwanini tuko bize kujenga makanisa, kuyapamba na kuyafunga kwa watu ambao tunaona wanashida au ‘hawafai’ kuja kanisani?

Tuko bize kuwa duniani ila sio wadunia kiasi kwamba tumefunga milango ya jinsi tunavyoweza kuwa wa msaada kwa watu wa dunia.


— Kwanini kanisa limekuwa sehemu ya biashara?

Je hili si ndo Yesu alilokasirikia sinagogi mpaka akasema nyumba ya Baba imekuwa pango la wanyang’anyi? Mbona kuna makanisa wanauza hadi bidhaa jumapili kama sokoni, wanauza mafuta, maji ya upako, samaki wanafugwa ndani ya kanisa?

Yesu alipotumia vitu vingine kuwaponya watu kama maji na mate vilikuwa vya bure, mbona siku hizi tunauza kama kweli vinafanya kazi ya Yesu?

Kweli mtu anashida na wewe mtumishi wa Mungu una mafuta ya upako wa Yesu yenye kuponesha ila unayauza? Sio watu ndio wanashida, wewe ndio unashida ya hela.

Na siku hizi kila mtu anafunuliwa vitu vipya mafuta, chumvi nk ila tu kuwawekea mikono watu ndio watumishi hawafanyi siku hizi. Jambo la bure ndio halifanyiki, oh nimesahau kuna watumishi kukutana nao wakuweke mikono unalipia, kama daktari au mganga.

Biashara.

Yesu na miujiza vinauzika, watu wanashida watalipia kutafuta suluhisho.


— Kwanini ni wepesi sana kuwahukumu watu kwenda jehanamu, kila tusiekubaliana naye basi na Mungu naye hakubaliani naye? Kwani kuhukumu ndio kazi yetu?

Wewe unajuaje nani ataenda mbinguni wakati wewe mwenyewe haujafika na unasubiria siku ya hukumu kama yeye?

Mtu akikukosea tu ataenda jehanamu na unamuombea mabaya Mungu ayatume kwake, Mungu sio kibaraka wako, yule pia ni mwanaye.

Na hii hutokea hata mtu akihama kanisa, tayari anakuwa adui yako na unamuombea mabaya.

Wakristo huwa tunadhani kuwa kwenye madaraja ya Mungu sisi tupo juu, tunapendwa na kusikilizwa, wengine wako chini. Mungu anawapenda wote sawa. Ndio maana Yesu alikufa kwa ajili ya wote, kupata wokovu hakukufanyi wewe bora.

Tumeanza lini kummiliki Mungu? Kuwalaani watu kupitia jina la Yesu, na kwamba njooni tutakuombea na Yesu atakuwepo?

Hivi Yesu ndio anatakiwa kuwa mgeni ambaye mnamiliki na mtamkaribisha? Kusudi la kanisa sio kuwa ni Yesu awepo muda wote?


— Wapiga picha huwa wanini kanisani?

Au tunahitaji kutengeneza content kwaajili ya mitandao ya kijamii? Labda kama tunarusha matangazo mubashara ila je wao huabudu lini?

Hasa kwenye concert mbona wao huwa hawaabudu? Wanapiga picha kitendo cha kipekee sana kuabudu, cha siri sana halafu kinawekwa Instagram.

Mbona tunahangaika sana kupiga picha kwaajili ya Instagram kuliko kuwa watulivu kuabudu?


—- Kwanini jumapili ni kama mashindano ya urembo na mavazi? Kimoyomoyo tunajilinganisha, kuchekana na kuangaliana


— Kwanini kanisa halipazi sauti kuhusu mabaya yanayotokea kwenye jamii zetu, kwanini hunyamaza kimya? Haiwasaidii wanaoteseka kwa namna mbalimbali.


Kwanini wakristo hawasomi Biblia

Tulianza lini kutafuta miujiza kanisani badala ya kumfuata Yesu.. maana tunataka miujiza ya Yesu kuliko Yesu mwenyewe.


— Tumeanza lini kuhubiri nguvu ya mapepo na shetani na sio Yesu?? Kanisa si la Yesu au ni la shetani / utajiri / safari za ulaya na magari?


Eunice

3 thoughts on “Mambo yanayotokea kanisani yanayonipa maswali magumu kuhusu ukristo

  1. James Chitemo

    Huna haja ya kujiuliza mengi wala kujadili sana, mfuate Apostle shemeji Melayeki, huyo ndiye aliyebaki kutufunulia maandiko.

    1. Eunice Tossy

      Asante sana kwa recommendation… Asante pia kwa kusoma rafiki

  2. […] Kuujua uongo wa dunia hii ila pia kuangalia kila kitu kupitia misingi ya Mungu, unajua dunia inapoel…. Yatupasa kusoma Neno la Mungu ili kuutenga ukweli na uongo kupitia Neno la Mungu ili tuishi kwa kumpendeza Mungu na sio kufuata mienendo inayoletwa na dunia. Biblia ina kila jibu la maswali yetu, Neno linasema hakuna jipya chini ya jua, kwa hivyo haya yote yalikuwepo na Neno la Mungu limegusia kila ishu na mambo yanayotokea duniani kwa mtazamo wa kiMungu. Tusome Neno tuujue mtazamo wake ili tumpendeze yeye katika maisha yetu. […]

Share Your Thoughts With Me

Muongozo wa Maisha ya Chuo

Je unaenda chuo? Au upo chuo?

Pata majibu ya maswali yako yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuoni hapa, pata dondoo na ushauri kwenye mahusiano, maswala ya pesa na biashara, afya yako chuoni, mitindo, skendo za chuo, kudili na walimu wasumbufu na ada mbalimbali zinazowahusu wanachuo kwenye kitabu hiki

Bonyeza Hapa Kupata Kitabu Hiki
Translate »