Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Dondoo za Maisha,  Maisha ya kila siku,  Random

Jinsi wanaume wanavyoweza kushiriki kwenye mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia

(Mwezi huu nitakuwa naposti aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia na data zinazohusiana nao, follow @swahiliwomen Instagram ili kujifunza kwa undani kuhusu hii mada)

Wanawake ni nusu ya idadi ya watu wote waliopo duniani.

Lakini bado wanapitia ugumu kwenye maisha kwasababu tu ya jinsia waliyozaliwa nayo.

Sehemu nyingi duniani kuwa mwanamke ni kuishi na vikwazo vingi sana katika maeneo mengi, haupati fursa sawa za elimu, za kazi, unaozeshwa mapema, unaonekana kama mtaji, hauna faida kwenye familia, hauwezi kumiliki ardhi, unauliwa kwa ajili ya heshima, unapigwa kwenye mapenzi nk. Yote haya na zaidi unapitia kama gharama ya kuwa mwanamke.

Naamini kuwa kupigania usawa wa jinsia ni kupigania haki za binadamu, kwasababu wanawake pia ni binadamu na kila binadamu ana haki sawa ya kuheshimiwa, ya kupata fursa nk.

Hivyo katika mapambano haya ni muhimu sana wanaume pia kuwepo, kushiriki na kusimama kwaajili ya kumaliza tamaduni, mawazo au mambo ambayo tumejifunza /tumeona yakifanywa karne kwa karne yanayopelekea kuona wanawake kama sio watu kamili, wanaostahili kuheshimiwa na kupata fursa sawa kwenye jamii kama wanaume.

Kama wewe ni mwanaume na ungependa kujua jinsi gani unaweza kushiriki kwenye mapambano kwaajili ya usawa wa jinsia, hizi hapa ni njia chache ambazo nahisi zinaweza kukusaidia kupambana na unyanyasaji wa kijinsia:

1. Anza kuangalia jinsi unavyopendelewa

Kwenye jamii zetu mwanaume anaheshimika.

Mwanaume anapendelewa….. Majumbani, maofisini, vyuoni, kwaajili ya uongozi, popote ulipo unapata heshima yatofauti kwasababu tu umwanaume, unapata kuangaliwa kwa jicho la tofauti, jicho linalokukuza kuliko wanawake ulionao katika eneo hilo.

Anza kwa kuuona huu upendeleo.

Anza kuona vile kuwa kama mwanaume dunia imetengenezwa kukuweka wewe mbele.

Unaweza kuwa umekuwa sehemu ya maisha yako sana kiasi kwamba haujui kama unapendelewa.

Na kama unapendelewa basi lazima kuna mwingine ambaye anaumia/anagandamizwa ili wewe upate huo upendeleo.

Kujua hili ni hatua ya kwanza ya kuanza kujua jinsi gani utatue hili tatizo.

2. Fikiria tena kuhusu mambo mbalimbali uliyojifunza kuhusu mahusiano ya jinsia hizi mbili

Jamii yetu ina sheria zake, ina namna wanaume wanaruhusiwa kuwa, ina namna wanawake wanatakiwa kuwa.

Kazi zipi wazifanye wakiwa majumbani, wakiwa maofisini, wale vipi, waongee vipi, kiufupi ni vipi unatakiwa uwe ili uonekane mwanaume kweli au mwanamke kweliWatu wengi wanafuata masharti haya, wengine wanaona kwenye maisha yao masharti haya yanawaumiza na wanatamani kuona kitu gani kinawafaa na kipi hakiwafai.

Kama ungependa kushiriki kwenye mapambano haya ni lazima ujiangalie pia ni jinsi gani kuona kwako thamani ya wanawake kumetokana na masharti na mafunzo uliyoyapata kwenye jamii na sio kwa kuishi na kuwajua wanawake kama wanawake walivyo.

Ni jinsi gani mahusiano yako na wao yanafuata masharti ya jamii tu??

Ni jinsi gani kufuata masharti kuna kubana, kugandamiza na kukuumiza wewe pia kama mwanaume unayeyafuata hayo masharti ya vile unatakiwa kuwa kwenye jamii?

3. Wasikilize wanawake

Jamii zetu zinasikiliza sauti za wanaume sana.Mawazo ya wanaume yanaumuhimu.

Sauti zao zinaumuhimu.

Wanaume wanatengeneza mdahalo ambao wanaume ndio wanaongelea ishu kama hedhi🤣🤣
Na nimeliona hilo zaidi ya mara moja.

Sauti za wanaume ndio sauti zinazosikilizwa sana.

Wanaume wana neno la mwisho kwenye familia, Kwenye ofisi.

Hata ukienda hotelini, mwanaume ndio anaulizwa, ‘mnapendelea kula nini?’.
Nakumbuka nilikuwa nasafiri, binamu yangu alinisindikiza, watu walikuwa wanamuuliza yeye, ‘anaenda wapi, mkatie basi fulani’ kana kwamba mimi hawawezi kuniuliza mwenye safari.

Haya yote yanawafanya wanaume kuamini kuwa wanajua kila kitu.

Ila ukweli ni kuwa wanawake wana sauti, wanajua vitu kuhusu wao, kuhusu maisha, kuhusu wanaume pia.

Wanawake wanajua kuwa wanafuraha au hawana furaha kwenye maisha yao hauna haja ya kuwasemea.

Wanawake wanamaoni yao, wanafikra.

Wasikilize wanawake
Uliza maswali, sikiliza.

Anza na wanawake wa karibu kwenye maisha yako, wasikilize.

4. Ongea

Ukiona mwanamke ananyanyaswa usinyamazie ukatili huo.

Ukiwa ofisini kwenye kikao na mwanamke akawa anatoa point ila mwanaume akamkatisha aongee yeye bila kumsikiliza, mwambie kuwa mwanamke naye anapoint.

Kama umetoka na marafiki, au mpenzi wako, na wakakuuliza wewe mtakula nini, waambie wamuulize pia huyo uliyenaye maana anamdomo kwanini umjibie?

Ukiwa kwenye daladala, ongea.
Ukiwa nyumbani ukaona unyanyasaji, ongea.

Pia ongea sana jinsi gani mfumo dume na kukosekana kwa usawa kunavyokuathiri. Unapofunguka wanaume wengine pia wanafunguka.

Toa msaada na ushirikiano kwa wanawake waliopo kwenye maisha yako.

Tengeneza mazingira ambayo wanawake waliopo kwenye maisha yako wanajiona sawa na wewe lakini pia upo nao kwenye kupigaa kwaajili ya usawa wao. Watakusimulia stori nyingi sana.

Kuza sauti za wanawake kwemye maisha yako na wanaoongelea hili swala la usawa wa jinsia.

Jielimishe kwa kufuatilia zaidi kuhusu hili swala, waelimishe wanaume wenzio, kama hawatilii maanani au wananyanyasa wanawake kwenye maisha yao, kuwa na msimamo, waelimishe, waoneshe wanachokosea, usinyamaze wakati maisha, hisia, usalama wa binadamu mwingine unagandamizwa na wewe unaona.


Ni njia zipi nyingine unahisi wanaume wanaweza kushiriki kwenye mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia?

Eunice


(Mwezi huu nitakuwa naposti aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia na data zinazohusiana nao, follow @swahiliwomen Instagram ili kujifunza kwa undani kuhusu hii mada)

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป