Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku

Mawazo ya Jumatatu : Kila unayekutana naye ana tatizo lake analopitia

Jumatatu nilienda Ocean Road, kuandaa matibabu ya saratani ya mtu wangu wa karibu ambaye aliyaanza siku ya J4. Katika siku hiyo maisha yangu yalikuwa yana badilika bila mtu yoyote kwenye daladala kujua. Nilikuwa na mawazo na maswali yasiyo na majibu ambayo labda yalifanana na maswali ambayo ndugu na marafiki wa wagonjwa niliowaona hospitali walikuwa nayo.

Nilipokuwa hospitali nilikutana na baba mmoja ambaye nahisi alikuwa na mgonjwa pale, alikuwa akikimbia kushoto na kulia kukimbiza chakula kwa mgonjwa wake. Alinifanya niwaze kuhusu upendo na umuhimu wa kuwa na watu walio tayari kuwa nawe hata ukiwa umelazwa kwenye kitanda. Nikikumbuka sura ya yule baba, najikuta napata maana ya neno ‘kujali’, maana ya neno ‘kujaliwa’, maana ya neno ‘upendo’. Mtu yoyote akiwa kwenye shida anatamani awe na mtu kama yule, nahisi hata tukiwa kwenye raha pia inanoga kuwa na mtu mwenye upendo wa kweli vile.

Nilipoondoka pale nilipanda pantoni ambapo nilikuwa nimekaa huku naangaliana na mama mmoja ambaye alikuwa anaongea na mtu kwenye simu. Nilimsikia yule mama akiongea na mwenzie na kumsimulia jinsi hapo alipo nyumba yake imeungua kwa bahati mbaya. Nilishangaa sana nguvu zake maana sikutaka hata kuwaza mimi ningekuwa kwenye hali gani kama nyumba ambayo naishi ingeungua. Lakini yule mama alikuwa anajitia nguvu na huku akimtia nguvu mwingine anayeongea naye. Kwa wakati huo niliangalia watu wa mule kwenye pantoni na kugundua kuwa kila mtu ana lake, ni vile tu hatuongei, au hatutembei na karatasi lilioandikwa matatizo yetu ila ukweli ni kuwa kila mtu analake, la tofauti, na lenye uzito mkubwa kwake ambalo mwingine alisikie tu.

Nilishuka pantoni na kupanda daladala, ambapo nilikaa siti ya nyuma na kujikuta nimekaa na mtu ambaye alikuwa na mawazo sana. Alipigiwa simu na akaanza kuongea kwa sauti kubwa kweli, kwa maelezo aliyotoa ni kuwa ofisi aliyokuwa anafanya kazi imefungiwa, na ilikuwa ishu kubwa sana kiasi kwamba hadi waandishi wa habari walikuja. Jamaa ndio alipoteza kazi hivyo, chanzo chake cha mapato ndio kimepotea siku hiyo yani paap bila hata taarifa yoyote iliyomuandaa kukutana na siku hiyo pamoja na habari hiyo ngumu aliyoipata. Kijana ndio anatakiwa aanze moja au arudi mkoani kama Dar sio nyumbani maana chanzo cha mapato yanayomkalisha Dar kimepotea siku hiyo.

Siku hiyo ya Jumatatu ndio nilijifunza kuwa kila unayekutana naye analake, kwenye daladala, kwenye foleni, kwenye mitandao ya kijamii, ofisini, dukani, baa, kanisani, msikitini nk. Kila mtu ana lake analopitia, linalomuathiri, ni sehemu ya kuwa binadamu, kupitia hisia za kibinadamu.

Siku hiyo pia nilijifunza kuwa ni muhimu kuwa mkarimu kwa kila unayekutana naye kwa vile kila mtu ana maumivu yake, ukiwa kama wewe ni wale watu ambao ukiumizwa unakuwa na hasira na unaenda kumkaripia mwingine tutaendelea kuumizana maana kila mtu ana lake tukianza kuyashusha kwa kila tunayekutana naye tutaendelea kuumizana zaidi. Tuwe wakarimu ili tuwe tunawapa uponyaji na tulizo kidogo watu tunaokutana nao, ukifanya hivyo kwa mwingine, na mwingine akafanya hivyo kwa mwingine, dunia inakuwa sehemu nzuri kidogo ya kuishi. Sisi binadamu tunafanana sana, zaidi ya vile tunavyohisi tumetofautiana, hata kama tupo kwenye hali za kiuchumi tofauti, mambo ya msingi tunayohitaji kwenye maisha na hisia tunazopitia mara nyingi zinafanana, tunahitaji afya njema, upendo, tunapitia huzuni, furaha na tunajisikia wivu, hasira nk. Tunafanana sana zaidi ya tofauti zetu, haijalishi mtu yukoje, kuwa mkarimu kwake.

Kitu kingine ambacho nilijifunza Jumatatu ni kuwa najikumbusha kuwa kuna siku nyingine nilikuwa napitia mazuri, kuna siku nilikuwa na furaha na hili pia litapita. Duniani huwa tunapitia yote mazuri na mabaya, ingawa akili zetu hukumbuka zaidi hisia na maumivu ambayo mabaya yalituletea kuliko pale tulipojisikia furaha na hisia nzuri nyingine. Ukiwa kwenye siku kama Jumatatu jitie moyo kwa kujikumbusha siku zako za furaha, jikumbushe kuwa hilo pia utalishinda, ili usizame kwenye huzuni ambazo siku kama Jumatatu inaweza kukuletea.


Kama ungependa kujiunga group langu la WhatsApp ambalo natuma makala hizi moja kwa moja, BONYEZA HAPA.

Na pia kama unapenda kusapoti uendeshwaji wa blogu hii kifedha, unaweza nisapoti kwa kutuma kiwango chochote utakachopenda kwenda namba hii 0627975502. Fedha hizi zinanisaidia kulipia hosting ya blogu hii na pia vocha kwaajili ya mabundle ili kuweka maudhui hapa. Asante sana

Eunice

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป