Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Dondoo za Maisha,  Maisha ya kila siku

Jinsi nilivyoacha kuogopa mbwa, na vitu nilivyojifunza kuhusu woga baada ya kuushinda woga huo

Nilikuwa darasa la nne mwaka 2004, nilipoenda kuwatembelea bibi na babu kijijini.

Usiku wake nilitoka nje kwenda kujisaidia, bila kujua kuwa babu amewafungulia mbwa wake, ambao walikuwa hawanijui na walioanza kunikimbiza usiku huo.

Mbwa wale walinikimbiza, nilipiga kelele, mpaka babu akatoka kunisaidia, akawafungia, nikajisaidia, nikarudi ndani kulala. Asubuhi yake, watu wote wakawa wanakuja kwa babu kuulizia mtoto aliyekuwa anakimbizwa na mbwa yuko wapi.. Mtoto wa Dar???.

Toka siku hiyo, mpaka hivi karibuni mimi na mbwa vilikuwa haviivi.

Nikimuona mbwa popote, jasho jembamba linanishuka, moyo unaenda mbio na nabadilisha njia.

Nimesoma mahali kuhusu woga wa mbwa, na wamesema kuwa unakuwa na sababu mbili:

1- Kuwa na experience mbaya na mbwa (mfano mimi)

2- Kuwaona mbwa baadae sana maishani, siunajua wale wanyama, kama haujamzoea unaona ni hatari tupu.

Hivi karibuni nikaweza kuushinda huo woga.

Na hizi ndio hatua nilizozichukua, lakini pia ndio mambo niliyojifunza kuhusu woga:

+++ Kukubali kuwa naogopa mbwa

Kukubali kuwa unatatizo ndio hatua ya kwanza ya kutatua tatizo. Nilipokubali kuwa mimi niko radhi nibadilishe njia kwasababu nimepishana na mbwa au natetemeka kwasababu mbwa anapita ndipo nilipoanza kutafuta suluhisho.

+++ Kuamua kutaka mabadiliko

Nilifika mahali nakuona kuwa siwezi nikaogopa mbwa maisha yangu yote, nichague niogope mbwa au nijifunze kuwazoea kwenye maisha yangu. Nikachagua kujua jinsi ya kuwazoea

+++ Kutembea na watu wasioogopa mbwa

Nikitembea peke yangu nilikuwa nageuza au nafanya chochote ili nisikutane macho kwa macho na mbwa, ila nikitembea na wasioogopa nilikuwa nakuwa katikati yao, na mimi naonekana siogopi.

Walikuwa wananipa mipango na jinsi ya kuonekana siogopi, wakawa wananiambia mbwa ananusa harufu ya mtu na kujua kuwa huyo mtu anaogopa kwa jasho analolitoa, na ndio maana wanajua mwizi kwasababu ya jasho wanalolitoa wakiogopa.

Wakanifundisha ukimuona mbwa, mwangalie usoni, usipindishe macho, muangaliane aone hauogopi.

Wakaniambia usikimbie, akija nawewe mfuate njia hiyohiyo, ikiwezekana mnyooshee kidole.

Wakaniambia mbwa anakudhuru kwasababu nayeye anajaribu kujilinda, muda mwingine ni woga wake ndio unamfanya akudhuru.

Sijajua kama yote ni ya kweli, ila yalinisaidia sana kuwa jasiri.

+++ Nikachukua hatua ndogo ndogo kuwazoea

Marafiki zangu hao walinitia moyo kuwabeba. Wakimbeba mbwa, wakawa wananizoesha na mimi nimbebe, taratibu mwaka juzi nikambeba mbwa kwa mara ya kwanza, huku naogopa lakini walinitia moyo mpaka nikaweza.

Sijafikia mbali sana kwamba ndo nimewazoea kihivyo, lakini sasa hivi nikipishana nao sikimbii, wakinijia kwa fujo, nawatishia wanaondoka, sijawazoea kivile ila ule woga sina tena.

+++ Kujikumbusha ukweli kuhusu huu woga kila ninaposahau

Kuna muda woga unarudi hasa nikiwa na wengine wanaoogopa ila najitahidi kujikumbusha na kuwatia moyo hao wanaoogopa pia ili wote tuwe jasiri.

Mambo niliyojifunza kuhusu woga kutokana na hii experience ni..

Woga ni Uongo unaojaribu kutuaminisha kama wenyewe ndio ukweli

Mbwa ni hatari, lakini sidhani kama kila ninapopishana nao wanahatari hiyo ambayo woga unaniaminisha wanayo. Kwahivyo akili yangu ukichanganya na woga nashindwa kufikiria vizuri kuhusu ukweli wenyewe.

— Unahitaji watu jasiri kukutia moyo kwenye kufanya vitu vinavyokuogopesha

Kama kuna jambo unaliogopa kulifanya, livunje vunje ili ufanye kwa hatua, usilikatae moja kwa moja na usiingie mazima

— Kila jambo linaweza kubadilika, ukiamua kutaka mabadiliko kwenye hilo eneo

Vipi wewe, ushawahi kuogopa mbwa??

Eunice

2 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป