Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Dondoo za Maisha,  Maisha ya kila siku

Mambo ya kufanya unaposalitiwa na mpenzi wako

Kusalitiwa kunauma.

Usaliti ni jambo ambalo kila mtu anaomba Mungu amuepushie ili lisimpate, ni jambo ambalo linawafanya watu waogope kuingia kwenye mahusiano kwasababu wanahisi litawapata.

Kama umegundua kuwa mpenzi wako anakusaliti, najua unapitia hali ngumu akilini na moyoni, kwasababu akili yako inaenda mbio kurudia matukio yote ya maisha yenu ili ujue wapi alianza huo usaliti, labda wapi ulikosea, labda hivi, labda vile.

Na moyo wako unaumia kwasababu uliyemkabidhi sio mwaminifu, uliyeamini yupo nawewe tu, peke yako, amemwingiza mtu mwingine kwenye dunia yenu.

Kusalitiwa ni kugumu sana lakini napenda ujue kuwa sio makosa yako.

Mtu anapokusaliti ni yeye ameamua kufanya hilo swala, na sio kwamba kuna jambo lolote ambalo wewe umekosea au umemfanyia yeye ambalo limempelekea kukusaliti. Yeye ni binadamu mwenye maamuzi yake, ambayo aliona ni bora aharibu mahusiano yenu kwa jambo la muda mfupi alilolichagua.

Ni maamuzi yake, haujachangia jambo lolote kwenye maamuzi hayo.

Muda mwingi tunasahau kuwa sisi watu tuna mambo mengi tunayopitia yanayotuathiri kwenye maisha, hivyo mambo watu wayotufanyia sio lazima yawe ni sisi ndio tumesababisha mpaka wakatufanyia, mara nyingi ni wao wenyewe wanashida zao ambazo sisi hatujashiriki kuzitengeneza.

Lakini pia mtu anapokusaliti anakuwa amekuonyesha makucha yake hauna haja ya kuyapaka rangi.

Muda mwingi ukigundua mtu amekusaliti huwa unajaribu kujielezea moyoni, kumpaka rangi ili tu usifikirie au usiumie kuhusu ubaya huo aliokufanyia.

Unajitia moyo. Kwavile bado unampenda, labda.

Utapona moyo haraka sana ukikubali kuwa hilo jambo limetokea, ni makosa ya huyo aliyoyafanya na hayo ndio makucha yake ambayo ulikuwa haujayaona sasa umeyaona. Ni aibu yake sio yako.

Mara nyingi wanawake huwa wanaambiwa, ‘umeshindwa kufanya A, B na C ndio maana amekusaliti’ ila ukweli ni kuwa kwa mtu mwenye tabia au maamuzi hayo hata kama ungefanya mpaka Z angekusaliti. Wewe unatosha, ni aibu yake na matendo na tabia yake.

Kama ni kweli ni makosa yako ndio yaliyompelekea kukusaliti kwanini asingekuambia ubadilike / kukuvumilia / kukuchukulia? Ila akaamua kukusaliti ili kukuonesha/kukufundisha, upendo hapo uko wapi?

Sio makosa yako, ni maamuzi yake.

Wewe ndiye uliyeumizwa, wewe sio ambaye unatakiwa ubebe aibu, aibu ni ya mtendaji.


Ukigundua kuwa mpenzi wako anakusaliti haya hapa mambo ya kufanya ambayo yatakusaidia;

Tuliza akili kwa muda

Ni rahisi kuandika kuliko kufanya, ila pia sikupangii ufanye mambo gani pale utakapomkamata kwasababu kila mtu ana namna yake anavyosuluhisha mambo na hasira pia inachangia maamuzi yako kwa wakati huo. Ila baada ya kujua kuwa unasalitiwa jaribu kutuliza akili ili kufikiria kwa umakini, unaweza ukaandika chini mawazo yako, ukalia au hata ukatulia tu mwenyewe ili ufikirie taratibu.

Unaweza pia ukamshirikisha rafiki yako wa karibu, wa kweli, ili awe nawe kipindi hiki kigumu.

Chukua muda kukaa mbali na aliyekusaliti

Hakuna kitu kama kusamehe haraka, yani umegundua anakusaliti halafu amekuomba msamaha umemsamehe. Chukua muda kufikiria, inachukua muda pia kurudisha imani kwake, lakini pia je msamaha unaoutoa unatokana na presha yoyote ile au ni kweli umeutoa moyoni?

Ukikaa naye mbali unapata muda wa kuwaza na unaepuka kufanya maamuzi yanayotokana na hasira au presha za watu au hali uliyonayo.

Unaweza kusoma : Jinsi ya Kusamehe

Nyamazisha kelele za watu na ujisikilize

Nilikuwa naongea na rafiki yangu ambaye aliniambia akiangalia YouTube kuna shauri nyingi sana anazozisikia za watu kuhusu mambo mbalimbali. Ukimsikiliza huyu anasema hili, na huyu anasema lile, wote wanatofautiana shauri zao ila wanaongelea jambo hilo hilo moja. Akaniambia vile anabaki anachanganyikiwa tu, hajui ushauri wa kuufuata.

Sio vibaya kusikiliza shauri, ila mwisho wa siku maisha ni yako, wewe ndiwe unatakiwa ufanye maamuzi.

Hatujajizoesha sana kujisikiliza na kufanya maamuzi yetu, hivyo mara nyingi huwa hatusikii mioyo yetu inapotushauri jambo au hatuamini kama shauri tunazojipa wenyewe zinanguvu au zinatufaa.

Ushauri wa kuufuata ni wako mwenyewe, maamuzi yako.

Haya maisha ni wewe unaishi.

Wewe ndiwe uliyesalitiwa.

Wewe ndiwe unaamua.

Umrudie au umuache.

Wewe ndio utaishi matokeo ya maamuzi yako.

Usiruhusu woga wa jambo lolote au hali yoyote au mtu yoyote akulazimishe ubaki, wengi wapo kwenye mahusiano na watu wanaowaumiza kila siku kwasababu ya woga wa kuwa peke yao, woga wa kulea watoto peke yao, woga wa hali ngumu ya maisha.

Amani yako na furaha yako ni muhimu, wewe ndio unaamua kama unastahili kuishi katika hali hiyo.

Napenda ujue kuwa kuna maisha bila ya huyo aliyekusaliti, na pia kuna furaha.

Kwa alilokufanyia hastahili wewe kwenda jela kwaajili yake au kufa kwaajili yake, hivyo usifanye maamuzi ambayo yanahatarisha maisha yako, najua sasa unaumia ila niamini ninapokuambia kuwa furaha ipo, na unaweza kuishi bila yeye.

Jaribu kufanya yale mambo yaliyokuwa yanakuletea furaha kabla ya mahusiano yenu

Ulipokuwa naye ulikuwa na furaha, kabla ya kujua kuhusu usaliti wake. Lakini naamini ulikuwa na furaha hata kabla hajaja kwenye maisha yako, uliishi tu vizuri kabla ya kumjua, unaweza kufurahi na kuishi tena bila yeye. Jaribu kufanya hayo mambo yaliyokuwa yanakuletea furaha.

Raha jipe mwenyewe.

Chukua muda kujipenda, kujifurahisha kabla haujamwingiza mtu mwingine kwenye moyo wako.

Chukua muda kujiponya, kujifunza na kusamehe.

Niamini ninapokuambia kuwa ipo siku moyo wako hautauma tena kama unavyouma leo.

Eunice

Unaweza kusoma : Kama unafikiria kujiua

2 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป