Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Guest Post,  Maswala ya Pesa

Hii ndio sababu mitaji mingi ya biashara mpya hufa mapema

Ushawahi kujiuliza kwanini mitaji mingi ya biashara mpya huwa inakufa mapema? Hii ndio sababu👇🏿


Mtaji wa kuanzisha biashara unahusisha fedha na mali za kuanzishia biashara, jumlisha na fedha za kuendeshea biashara kwa angalau miezi miwili (2) mpaka sita (6) ya mwanzo kwenye biashara au mradi mpya.

Fedha na mali za kuanzisha biashara zinatumika;

– Kusajili biashara

Kulipa makadirio ya kodi ya mapato, kupata TIN na kulipia leseni pamoja na vibali vyote vya kuanzisha biashara

-Kununua malighafi

Za kutengenezea bidhaa au kununua bidhaa kwa bei ya jumla.

-Kununua mashine za Uzalishaji

-Kukodi eneo la Biashara

-Kurekebisha eneo la Biashara

-Kununua samani za ofisi

Viti, Meza n.k

Gharama za kuendesha biashara mpya ni pamoja na;

– Kuzindua biashara mpya

– Kutangaza bidhaa mpyakwa njia mbalimbali

(T.v, radio, Mitandao ya kijamii, Magazeti, vipeperushi e.t.c )

– Kulipa mishahara ya awali kwa miezi miwili ya mwanzo.

– Gharama za usambazaji bidhaa mpya kwa miezi miwili ya mwanzo

-Gharama za umeme na maji kwa miezi miwili ya mwanzo

Na kulipia Gharama zingine zote kwa miezi miwili ya mwanzo.

Mtaji wa biashara unatakiwa kuhusisha gharama za kuanzishia biashara na gharama za kuendesha biashara kwa angalau miezi miwili mpaka sita ya mwanzo kwasababu biashara yoyote mpya haiwezi kujiendesha yenyewe kwa kutegemea mauzo ya bidhaa mpya pekee yake.

Mara nyingi bidhaa mpya huwa zina sifa ya kutojulikana na wateja, kuwa na mauzo madogo na usambazaji mdogo, hivyo hata faida inayopatikana kutoka kwenye bidhaa mpya kwa miezi miwili mpaka miezi sita ya mwanzo huwa ni ndogo sana kuweza kulipia gharama zote za kuendesha biashara mpya husika.

Ndio maana gharama za awali za kuendesha biashara mpya kwa miezi miwili mpaka sita ya awali zinatakiwa kujumuishwa kwenye mtaji wa biashara husika.

Maana yake ni kwamba, mfanyabiashara mpya hatakiwi kutumia fedha yoyote kwenye biashara mpya au mradi mpya kwa kipindi cha miezi miwili mpaka miezi sita ya mwanzo tangu biashara husika ifunguliwe. Kwenye biashara mpya kila mfanyabiashara anapofanya mauzo anatakiwa kuiweka ile fedha akiba.

Pia Soma : Namna biashara ya Network Marketing ilivyonipeleka polisi

Maana yake ni kwamba kwa miezi miwili mpaka sita ya mwanzo;

– Mishahara ya wafanyakazi na mmiliki haitakiwi kutoka kwenye fedha za mauzo ya miezi miwili ya mwanzo, inatakiwa kutoka kwenye mtaji.

– Gharama za kununua mzigo mpya ukiisha hazitakiwi kutoka kwenye fedha za mauzo ya miezi miwili ya mwanzo, inatakiwa kutoka kwenye mtaji.

– Gharama za matangazo na usambazaji, umeme, maji, usafi, kula ofisini na gharama zingine zote za miezi miwili ya mwanzo kwenye biashara hazitakiwi kutoka kwenye fedha za mauzo ya miezi miwili ya mwanzo, inatakiwa kutoka kwenye mtaji.

Fedha hizo zinatakiwa ziwe zilipigiwa hesabu kwenye mtaji wa kuanzisha biashara husika mapema.

Na fedha za kumudu gharama zingine zozote za kuendesha biashara mpya kwa miezi miwili ya mwanzo zinatakiwa ziwe mkononi mwa mmiliki. Hapo ndipo biashara husika inakuwa na asilimia kubwa za kuanzishwa na kuendeshwa kwa mafanikio Makubwa.

Wafanyabiashara wengi wapya wanalalamika biashara ni ngumu, kwasababu huwa hawapigi kwenye mtaji wao gharama za kuendesha biashara husika kwa angalau miezi miwili ya mwanzo.

Wafanyabiashara wengi wapya punde tu wanapoanzisha biashara mpya, wanataka hapo hapo waanze, kujilipa mishahara kila mwisho wa mwezi kwa fedha za biashara changa, kujitangaza kupitia fedha za mauzo machanga, kusambaza bidhaa mpya kupitia fedha za mauzo ya awali, na kulipia gharama zingine zote kwa kutumia fedha za mauzo ya awali.

Hili ni kosa kubwa ambalo huwa linaua biashara nyingi sana mpya. Ndio maana biashara nyingi mpya haziwezi kuendelea tena baada ya miezi 6 tu au mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake. Wafanyabiashara wengi wapya huwa hawajipangi vya kutosha ndio maana biashara nyingi mpya huwa zinafeli mapema.

Pia Soma : Mambo ya kuzingatia unapotoa na kupokea ushauri

USHAURI WA KITAALAMU.

Kama kuna mtu anataka kufanya Biashara mpya au anataka kuwekeza fedha kwenye mradi fulani mpya.

Kwanza apige hesabu zote za kuanzisha hiyo biashara au mradi husika.

Kisha apige na hesabu za gharama za kuendesha biashara husika kwa angalau miezi miwili ya mwanzo

Jumla yake ndio afahamu ndio mtaji wa kuanzisha biashara husika.

Kama mtu husika hauna hizo fedha zote, unaweza;

-kuunza hizo fedha chache ulizonazo mpaka zifikie mtaji unaohitajika ndio uanze biashara husika

-kumshirikisha mtu mwingine wazo lako la biashara ili kama atavutiwa muungane kwa pamoja kimtaji kufanya hiyo biashara au mradi husika mpya.

-kuuza vitu vya thamani ambavyo havitaathiri maisha ya kawaida kwa kipindi hicho ili upate fedha za kuongezea kwenye mtaji unaohitajika kuanzisha biashara husika. Baadae sana biashara ikikaa vizuri hata baada ya mwaka mmoja zile faida za biashara husika ndio utazitumia kidogo kidogo kununua hivo vitu binafsi unavyohitaji.

Usinunue kwasasa vitu vya thamani sana wakati hauna chanzo cha uhakika cha kukuingizia fedha kwa wakati huu.

Hizo fedha ziweke zikifikia, anzisha biashara kwanza, faida za mauzo ndio huwa zinanunua mahitaji binafsi ya anasa, tena ni baada ya miezi 6 hadi mwaka tangu biashara mpya husika ianzishwe.

Kila biashara inalipa na ina faida. Inategemea umeingiaje kwenye hiyo biashara husika.


Imeandikwa na Mr. Godfrey Edward.

Mr Godfrey Edward ni mwanzilishi wa GEMIX company limited, ni mshauri wa mambo ya biashara na mwandishi wa Kampuni ni dhahabu na Ushindani wa biashara, anapatikana kwa namba 0656058184.

2 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป