Hauwezi kumuiba mtu mwenye akili, unaweza kuiba vitu.

Mtu mwemye akili anafanya maamuzi ya kuondoka au anashawishika na kubadilisha maamuzi. Hajaibiwa ila amefanya uamuzi muda mwingine hata bila kushawishika.

Hauwezi kumuiba mtu mzima.

Inabidi tufike mahala tusiwafanye wanaume kama vile watoto au vitu, au watumwa wa hisia za kimapenzi ambao hawawezi kutumia akili au kufanya maamuzi.

Mtu mzima anayeweza kufanya maamuzi hawezi kuibwa, mtu mzima anayeweza kuongea hawezi kuibwa, mtu mzima anayeweza kutembea na kumfuata mtu sehemu nyingine hawezi kuibwa.

Sijajua hii kihistoria inatokana na nini, nahisi, nahisi labda inatokana na ile ya kuwa zamani kulikuwa na stori za kuwa watu wanaweka limbwata au kutumia uganga ili kuwa na mwanaume fulani, nimeangalia muvi za kinigeria nyingi kuona hili, na nahisi inabidi nielewe na kuacha nafasi ya kuwa inawezekana kihistoria au kiimani fulani hili linawezekana. Ila wanaume wa siku hizi ambao wanawake wanaenda kupigana na wanawake wenzao kuwa wamewaiba hata hakuna nguvu ya imani yoyote iliyotumika, jamaa aliamua tu kusaliti au alifuata tamaa zake.

Kwanini wanawake wanapigana wakati jamaa ndio amewafuata wote wawili? Au kwasababu hawawezi kumpiga jamaa? Au kwasababu wanahisi yeye ni mtu ambaye hawezi kuwa mwaminifu? Au wanahisi ni mtu ambaye hawezi kudhibiti hisia zake za kimapenzi? Au kwa vile ‘mwanaume ni mtoto wa kwanza’ katika familia utakayoanzisha naye kwahiyo unahisi hakuwa na uamuzi kwenye kilichotokea? Au kwa vile tunaamini kuwa mwanaume hawezi kubadilika ila mwanamke ndio angeheshimu kiapo cha ndoa alichokichukua mwanaume na mke wake? (Hapo ni kama tu huyo mwanaume atakuwa amesema kama yupo kwenye ndoa maana wengine hawasemi).

Pia Soma : Kwanini wanawake hawapendani?

Nahisi inashangaza kuwa tunaamini wanaume wanaweza kufanya maamuzi mazuri kwenye siasa, kwenye biashara, kwenye kuendesha ukoo na familia yani kwenye kila eneo kasoro hisia zao za kimapenzi. Likija kwenye makosa wanayofanya kwenye maswala ya mapenzi inakuwa kosa la mwanamke. Kwamba hata kama alifanya uamuzi wewe mwanamke ungekataa kwa kujua kuwa yeye ni mume wa mtu, vipi kama hukujua? Kwanini yeye kwakujua kuwa ni mume wa mtu asingetulia na mkewe?

Nahisi huu msemo unatoa nguvu ya wanaume kuwajibika kwa maamuzi yao, na tunapoondoa uwajibikaji tunatengeneza hii tabia kuendelea na kukubaliwa kwa misemo kama hii. Tunapoondoa uwajibikaji na kuwafanya wanaume kama watoto au watu wasioweza kuwa waaminifu au kama vitu vinavyoweza kuibiwa tunasababisha wanawake kupigana na wanawake wenzao sehemu ambapo ni makosa ya mwanaume ambaye aliamua kutokuwa mwaminifu.

Pia Soma : Mambo yakufanya unaposalitiwa na mpenzi wako

man in black long sleeved shirt and woman in black dress

Kila siku kwenye maisha tunafanya maamuzi, tunachagua yale tunayotaka kuyafanya, yanapotokea matokeo ya maamuzi yao tusifanye kama vile watu kuwa hawana nguvu ya kubadilisha tabia zao au kuwa matokeo hayo yametokea bahati mbaya na sio kwa vile walifanya uamuzi fulani.

Hakuna mtu mwenye nguvu juu ya maamuzi na maisha ya mwingine kama yeye mwenyewe.

Eunice

You May Also Like

Share Your Thoughts With Me

Translate »