Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku,  Self Care

Bonge : Jinsi kuukubali mwili wangu ulivyo kulivyonifanya nijiamini na nijione mrembo

Hakuna kitu nilikuwa sikipendi kama nikipita barabarani halafu nisikie ‘bonge’. Huwa sipendi kuitwa itwa barabarani na wanaume ambao wamejiajiri kwa kazi hiyo ila kuitwa ‘bonge’ ilikuwa inaniondolea hata kujiamini nilikokuwa nako, maana nilikuwa najisikia vibaya kuwa bonge.


Kwa kawaida, kwa siku ninazojipenda na kujikubali mimi ni mtu ninayependa mitoko sana, lakini kwa mara ya kwanza mwaka huu nilikataa kwenda kwenye harusi na mitoko mbalimbali kwasababu nguo zangu hazinitoshi, lakini pia huwa sipendi kila unapotokea kitu cha kwanza watu/ marafiki zako wanachoongelea ni mwili wako, vile umebadilika, vile umenenepa vile haukuwa hivi, vile mikono yako iko hivi na vile.


Kwa muda mrefu nilikuwa nasubiria kupungua ili nguo zangu zilizo kabatini ambazo nilizinunua nilipokuwa mwembamba zirudi kunitosha ila imenibidi nifike muda wa kuacha kusubiria maisha yangu yaanze baada ya kupungua na ninunue nguo mpya zinazonitosha katika umbo langu la sasa, mwili wangu katika size yoyote unanifaa na unatosha kwa mimi kuishi maisha yangu mazuri, sina haja ya kusubiri wakati maisha yanaendelea, maisha hayanisubirii mwili wangu upungue


Kwenye dunia tunayoishi sasa, wembamba ndio urembo. Wembamba ndio unakubalika kama alama ya urembo na mwili unaokubalika. Unapokuwa mtoto kuwa mnene ndio kitu kizuri, ni alama ya kuwa familia yako ni matajiri, unalishwa vizuri, lakini pia unakua vizuri. Unapokua, unene ni alama ya kuwa wewe ni mvivu, mzembe na unakula sana (yani hauwezi kujizuia).

Kama binadamu ninayeishi dunia hii kila siku nakutana na hizi jumbe, kila ninapoangalia kuna bidhaa zinazouzwa zenye lengo la ‘kunisaidia’ mimi kupungua. ‘Kunisaidia kuwa mrembo’, ‘kunisaidia kuwa kwenye size inayokubalika’. Ukweli ni kuwa wao wanafanya biashara, wananifanya nijisikie vibaya kwa vile mwili wangu hauko vile wao wanadhani mwili unatakiwa kuwa ili uwe mrembo, kwa hiyo wanatumia hilo kupata faida kutoka kwangu. Ni biashara.

Lakini pia kitu ninachojifunza sasa ni kuwa miili yetu ipo tofauti. Yani watu wote duniani tuna miili tofauti, hakuna mwili mmoja ambao wote tunaweza kuwa. Haiwezi kutokea kutokana na sababu mbalimbali, kama vile ilivyo wote tuna mienendo tofauti, kila mtu anamwendo wake. Tuko tofauti. Utofauti ni mzuri.

Tuko tofauti kwasababu utofauti unaupendezesha dunia

@eunietj Instagram

Mimi kusubiria kuwa size fulani ambayo ya mtu fulani inayoonekana ndio urembo ni kusubiria jambo hilo maisha yangu yote na hata nikifika sitodumu sana maana sio size ambayo mwili wangu kiasili upo.

Ukweli kuhusu urembo ni kuwa huwa unabadilika, kutokana na muda na kipi kinauza kwa wakati huo. Zamani lips kubwa zilikuwa zinadharauliwa, sasa hivi ndio urembo. Zamani watu wenye makalio makubwa walikuwa wanachekwa, sasa hivi watu wanafanya oparesheni ili wawekewe makalio makubwa. Kitu kinachoonekana ni urembo huwa kinabadilika badilika kutokana na watu, ukiamua kufuata haya mambo utajibadilisha mara ngapi?

Mwili unabadilika kutokana na hali tofauti, badala ya kuutesa kuupunguza kwanini tusiangalie na kuushukuru kwa kazi ambayo miili yetu inafanya? Bila mwili wako, na kazi ambayo mwili wako unafanya ungekuwa wapi?

Mimi nimechoka kujibana kwenye maisha wakati naweza nikaenjoy maisha kwa asilimia 100, sijawahi kujaribu diet kwasababu sipendi kuishi maisha yangu nikihesabu kilo ninazokula, nikiangalia kila kitu na kujinyima vitu, nimechoka kuchukia mwili wangu kwa kutokuwa size fulani na kusikia aibu kwenda mitoko na kuenjoy maisha yangu kwavile nasubiria nifike size fulani ambayo inakuja baada ya kujiadhibu, kuadhibu mwili wangu, kujiadhibu mimi.

Nimeamua kujipenda na kujikubali, kuukubali mwili wangu vile ulivyo, kuuheshimu na kuupenda kwa mambo unayonifanyia, kuona thamani yake na kujua kuwa vitu ninavyoviwazia kuhusu size nk havina maana na uzito kama ninavyodhani vinavyo lakini pia miili iko tofauti, size ziko tofauti na hii ndio size yangu. Inaweza ikabadilika, inaweza isibadilike, ninaupendo mwili wangu kwa hali zote. Ninaukubali kwa hali zote.

Njia rahisi iliyonifanya kufika hapa, ni kukaa uchi, kujiangalia kwenye kioo na kuona jinsi mwili wangu ulivyo na kuangalia sehemu mbalimbali ambazo huwa najitahidi kuzificha na kuzikubali vile zilivyo. Sio jambo la siku moja na ndio maana kama tunavyojiambia maneno hasi kila siku, ni lazima kila siku tujiambie maneno chanya, tuiambie miili yetu maneno chanya.

Dunia tayari ina kampeni nyingi dhidi ya mwili wangu, sina haja ya kujiambia mimi mwenyewe pia maneno mabaya. Pia sina haja ya kusikiliza au kufollow watu wenye kampeni hizi pia. Ninaweza nisibadilishe watu wanaodharau miili iliyotofauti na wao, naweza nisiwabadilishe watu wanaofanya biashara kwa kwafanya watu wanajisikie vibaya kuhusu miili yao, ila ninaweza badilisha vile mimi ninavyojiona, ninavyojikubali, vile ninavyojipenda na kujithamini mwenyewe. Maisha yangu ni yangu, mwili ni wangu na maamuzi ya jinsi ninavyojiona na yenye uwezo wa kuniathiri ni yangu.


Nimeongeza ile suruali yenye sehemu inayoongezeka, nimegawa zile nguo zinazonibana, na zawadi yangu ya mwaka mpya 2021 ni kwenda kujinunulia nguo zinazonitosha sasa. Mimi ni mrembo, najiamini, najikubali, najipenda vile nilivyo.


Eunice

3 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป