Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku

Kwa mwanamke aliyewahi kubakwa

Unaweza ukawa hauelewi ni jina gani unatakiwa uite kitendo kilichokutokea, inawezekana ukawa hauamini, inawezekana ukawa umeamua kuacha yote nyuma ili uendelee mbele na maisha, umefungia vizuri kwenye kabati yaliyokutokea.

Unacheka na watu wanaokuzunguka, hakuna anayeona kidonda ulichonacho ndani.

Unaongea na wanaume wanaokuzunguka ila unashindwa kujizuia jinsi mwili wako haujisikii salama hata mmoja wapo akikusogelea.

Muda mwingine unapata ndoto za tukio zima, na jinsi mwanaume mmoja aliyedhani mwili wako ni mali yake na ananguvu kuliko wewe na anaweza akakufanya chochote alivyoitumia haki hiyo aliyojipa kukupa kidonda ambacho unachosasa.

Na labda hakuwa mmoja.

Na labda haikuwa mara moja.

Na labda kwa kitendo hicho umejikuta haujui kama mwili huu ni wako, haujui kuwa una maamuzi nao, hauamini kuwa kuna wanaume wengine ambao hawako kwaajili ya kuonesha mabavu yao kwa kukuumiza.

Kwa mwanamke aliyewahi kubakwa, nakuamini.

Watu wako wakaribu wanaweza wasikuamini, wanaweza wakakunyamazisha kutokuliongelea hilo au unaweza ukawa unajiuliza maswali ukitamani tu kufuta hilo tukio akilini b mwako, lakini bado lipo.

Nakuamini, kwasababu na mimi ni mmoja wao. Stori zetu zinaweza zisifanane, zinaweza zikawa zimetokea kwenye pande tofauti za dunia lakini kilichotutokea ni kimoja, mtu/watu waliodhani wana haki kwenye miili yetu walichukua utu wetu na kutuacha na aibu na kujihisi ni makosa yetu.

Kwa mwanamke aliyewahi kubakwa, sio makosa yako.

Haijalishi ulikunywa kiasi gani, ulivaa nguo gani, ulikuwa na mahusiano naye gani au ulifanya makosa gani, aibu sio yako kuibeba ni ya huyo aliyekubaka.

Kwani kuna kitu chochote kinachomfanya mtu astahili kubakwa? Sio makosa yako, usijilaumu. Hamisha aibu unayoisikia kutoka kwako kwenda kwa yule aliyekubaka, ni makosa yako.

Kuna mambo mengi yanayofanya watu wakose utu na kufanya vitendo vya kinyama kama ubakaji, ila wewe sio sababu ya wewe kubakwa. Na wala siyo jinsi ulivyovaa au ulivyonyamaza.

Kwa mwanamke aliyewahi kubakwa, inachukua muda kuongea.

Ilinichukua muda sana kumwambia mama yale niliyokuwa nafanyiwa, lakini pia ilinichukua muda kuwaambia watu wengine hii habari, kwanza nilikuwa nawaza je wataniamini, lakini pia kuna wengine ambao niliwaambia ambao walitamani tuifukie nisiiongelee tena, hivyo sikuwa na motisha ya kuiongelea maana wengi hawakuonesha kupenda kusikia.

Watu wa nje wanaweza kuigiza kuwa hiki kitendo hakijakutokea, wewe hauwezi kuigiza.

Inachukua muda kupata sauti yako na kusema kilichokutokea, nakuombea upate mtu mmoja utakayemwamini, na atakayekusikiliza utakapomwambia, atakayeelewa na kuumia na wewe kwa uliyoyapitia.

Familia nzima inaweza ikawa imesahau kilichotokea au haijui, lakini kwako tukio zima unalikumbuka kama ndio kwanza limetokea dakika mbili zilizopita… Au umelisahau ila maumivu yaliyobakia hayakuachi usahau tukio hilo.

Kwa mwanamke aliyewahi kubakwa, naelewa, nakuona na najua kuwa maisha yako yalibadilika. Mwanamke uliyekuwa kabla ya kubakwa ni tofauti na mwanamke unayemjua sasa, ni kama tukio lile lilikubadilisha, dunia inajidanganya na picha ya jinsi ulivyokuwa na wanakuumiza wanapokuuliza, ‘mbona umebadilika?’.

Kubadilika ni lazima, maana umeona ubaya wa dunia na ubaya ambao watu wanaweza kuufanya, umewahi kutokuwa salama kwenye dunia ambayo bado unaendelea kuishi, kubadilika ni lazima.

Nakuombea upate msaada, nakuombea upate haki, nakuombea upate uponyaji wa moyo, na kuombea ufike mahali kwa kusamehe na kujisikia salama duniani.

Una thamani, wewe sio binadamu uliyeharibika au uliyepungua thamani.

Kutoka kwa mwanamke aliyewahi kubakwa, kwenda kwa wanawake waliyowahi kubakwa.

Eunice.

One Comment

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป