Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Dondoo za Maisha,  Maisha ya kila siku

Jinsi ya Kusamehe

(Naomba niseme naelewa hali zipo tofauti, na sio kwamba hizi njia zitamsaidia kila mtu, naelewa kuna mambo mengine ni magumu sina majibu kwayo, ila naweka tu vitu vilivyonisaidia mimi hapa nilipo)


Kusamehe sio jambo la siku moja

Hii itakuwa topic ngumu kwangu kwasababu nahisi kama bado kuna watu nafanyia kazi kuwasamehe.

Ubaya ni kuwa duniani sio mbinguni, kwahiyo hatujalindwa na kutokuumia. Kwa vile tunaishi duniani kuna watu watatuumiza, kutukwaza na kutufanya tuwe na uchungu.

Tutafanyia kazi kumsamehe mmoja na mwingine atatuumiza tena.

Kusamehe ni safari, sio neno unalolitoa mara moja, kwamba ‘nimekusamehe’ halafu ukajisikia vizuri ukaendelea na maisha yako.

Sijui kwa wengine ila kwangu, kusamehe kunachukua muda.

Kama niliyoelezea kwenye hii makala niliyoiandika nikiwa na uchungu mwingi sana, nikiwa bado sijafikia hatua ya kusamehe, kusamehe ni zaidi ya kusema tu neno nimekusamehe. Ni zaidi ya kuambiwa samahani na kuipokea.

Kwasasa nahisi kusamehe ni pale ambapo hausikii tena hasira uliyokuwa unaisikia ukisikia jina la mtu yule aliyekukosea.

Kusahau, sijui nisemeje kuhusu hili. Ila nahisi kuna vitu ambavyo vinakutokea kwenye maisha ambavyo vinabadili maisha yako yote, hivyo sidhani kama ni rahisi kusahau hivi vitu.

Ni kama kidonda, kitapona, ila kuna wakati unakumbuka kuhusu ajali iliyokusababishia.

Na nahisi ndio maana wengi wanahisi hawajasamehe. Kwasababu hawajasahau.

Ila sina uhakika unatakiwa usahau, ila nina uhakika unatakiwa usamehe.

Makala Inayoendana na hii : Church Wounds and My Trust Issues

Nimeelezea kidogo kuwa nilifanyiwa vitendo vya unyanyasi wa kijinsia nilipokuwa mtoto (sexual abuse) nilipokuwa na miaka 12-13. Sikumbuki vizuri umri gani.

Na mtu wa karibu yangu ambaye tulikuwa tunaishi naye. Nilikuwa namuita mjomba.

Na takwomu zinaonesha wengi hufanyiwa na watu wanaowajua.

Yule mtu aliniomba msamaha. Nilipomuelezea mama niliyokuwa nafanyiwa.

Nilimwitikia kwa kichwa. Nikimaanisha nimemsamehe au nimekubali aliposema samahani.

Ila bado nilibaki na uchungu, hasira na kila nikimuona nilikuwa sijisikii salama.

Kusamehe ni safari. Sio tendo la mara moja.

Kuna wakati nilikuwa najihisi labda mimi sio mkristo mzuri kwa kuumia kila nikikumbuka nilichotendewa, labda mimi sio mkristo mzuri kwa kukumbuka, kwa kutokusamehe mpaka leo nilichotendewa.

Nakumbuka stori ya Yona muda mwingine, na ingawa sijui vizuri Biblia, kwa niliposoma najua alitumwa kwenda kuwahubiria wale waliowahi kuumiza nchi yao, na ndio maana akabadilisha safari. Bado alikuwa na uchungu na hasira na bado Mungu alikuwa anamtumia, bado Mungu alikuwa anaongea naye kwenye maisha.

Kuna muda tunahisi sisi ni wabaya kwa kuumia, na hivyo Mungu hatujali. Lakini napenda kufikiria kuwa Mungu wetu ni kama Yesu alivyokuwepo duniani, aliuangalia mji na kulia.

Na sio kwamba kwenye machungu yetu hayapo, yupo, na huumia pamoja nasi.

Kama unashindwa kusamehe haya ni mambo machache yanayoweza kukusaidia:

++ Jiruhusu usikie hizo hisia unazozisikia

Ukizibana na kuzigandamiza ili ujisikie tu vizuri wakati wote haikusaidii kwenye uponyaji wala kusamehe.

Kama ni uchungu, usikie, ukisikia kulia, lia. Jiruhusu kuzihisi hisia zako kama zilivyo.

Aliyokutendea sio mazuri na una haki yote ya kujisikia kuumia kwasababu ya aliyokutendea.

++ Andika chini mawazo yako au ongea na mtu

Usiogope watu watakuonaje haswa wa karibu yako, ongea vile unajisikia kwa unayemwamini. Jiruhusu kuwa muwazi kwake, bila kufikiria kile utakachomwambia atakichukuliaje au atakuonaje. Kama huna unayemwamini andika.

++ Kubali kuwa sio rahisi kumsamehe

Watu wengi hufanya kusamehe ni kitu chepesi hasa wakristo. Na hufanya wale wanaochukua muda waonekane kama sio wakristo kamili. Lakini kila mtu anachukua muda tofauti kwenye kusamehe, kwa wengi sio tendo la siku moja na hasa inategemea na ukubwa wa kosa muda mwingine. Kubali kuwa sio rahisi kwako, lakini pia ona kuwa unajitahidi kwa uwezo wako wote kumsamehe na ndio maana hata unasoma makala hii. Ona vile unavyojitahidi kumsamehe na hivyo wewe sio mtu mbaya.

++ Tafuta kuongea naye kama unaona ni muelewa

Njia moja wapo rahisi ni kuongea na huyo mtu. Sijui wengine ila mimi nilikuwa natamani sana kumwambia kuwa, ‘ulichonifanyia sio kizuri na kimeathiri maisha yangu sana’. Lakini sijawahi pata hiyo nafasi. Ila mwanasaikolojia wangu aliniambia, ‘nifumbe macho na nifikirie yuko mbele yangu namuona, nimwambie ninayotamani kumwambia’. Hilo zoezi lilinisaidia sana.

Kama yupo na nimwelewa mnaweza mkaongea ukayatoa yote ya moyoni, kama sio unaweza fanya hili zoezi.

++Kumbuka kuwa unasamehe kwaajili yako

Mara nyingi huwa tunafikiria kusamehe kunamfaidisha aliyetukosea kuliko sisi na ndio maana tunajizuia kusamehe ili yule aliyetukosea asipate uhuru ambao utatokana na sisi kumsamehe.

Lakini ukweli ni kuwa kutokusamehe kunatuumiza sisi na si yeye.

Sisi ndio tunabaki na uchungu na hasira kuhusu huyo mtu wakati yeye anaendelea na maisha na muda mwingine hajali kuhusu kupata msamaha wetu.

Kusamehe kunakupa amani, kusamehe kunakupa uhuru wewe, unakuwa umeachilia mzigo moyoni, umeachilia watu uliowabeba.

Kwahiyo kila saa unapojisikia unashindwa kuachilia, jikumbushe, jitie moyo kwamba unajifanyia hivi wewe. Maisha yako hayatakiwi yasimame kwenye majira fulani wakati dunia bado inaendelea kwasababu ya kumshikilia mtu mmoja moyoni.


Na hayo ndio mambo nifanyayo ili niweze kusamehe. Wewe huwa unafanya nini?

Eunice

2 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป