Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

ripe tomatoes in ceramic bowl placed on marble table
Maoni

Thamani ya vyombo vya udongo na vile inavyobadilisha tunavyojiona.

Kuna vitu viwili nimeviona kwa jicho la tofauti jana ambavyo vimenifanya nifikirie sana. Kukaa kwenye mawazo ambako nakuwa nawaza maana au imani nilizonazo kwa undani ili kujielewa na kujijua vizuri ni kitu ambacho napenda sana kukifanya, sasa ngoja nikuambie kuhusu vitu vilivyotokea.

Wakati napita mtaani, kuna nyumba niliipita ambayo kwenye geti lake la nje wameweka urembo wa juu ambao unakuwaga na bati, natamani ningepiga picha nikuelezee, kusema ukweli sijui kazi yake ila kama kuna mtu anaifahamu naomba aniambie kwenye comments. Ila katika maisha yangu niliyoishi hapa duniani mara nyingi huwa naona ni jinsi gani vitu huwa vinavuma, na sisi wengine wote huwa tunavifanya bila kufikiria, kwa vile vinavuma, tunaamini kuvifanya kutatufanya tuonekane watu wa aina fulani. Sio kwamba nachukua fursa hii kumsema mjenzi wa nyumba ile, hapana, kwanza hata nilipoiona ile nyumba na kuwaza hivi nilijiangalia mimi kwenye maisha yangu na vitu ninavyovifanya, nilijiuliza mimi ni vingapi nafanya kwasababu ni trend, ni vingapi nimevipa thamani nakuviona vya muhimu wakati ukweli ni kuwa labda hata kazi yake siijui au thamani yake na ukubwa wake kwangu ni wa fikra tu au wakufuatisha watu na mawazo yao tu….

Pia Soma : Ukiwa busy kuangalia maisha ya wenzako, ya kwako yanakupita

Ukubwa na kutukuza jambo kwenye fikra kunaweza kubadilisha namna unavyojichukulia au kuona thamani za watu. Usiku wa jana nilikuwa maeneo ambayo tulikuwa tunakunywa chai, na mwingine akapewa kikombe cha udongo, halafu mimi nikapewa kikombe cha plastiki, si jambo kubwa sana, labda vikombe viliisha. Ila nikajikuta nawaza kwanini nimepewa kikombe cha plastiki na sio cha udongo, je muuzaji anahisi mimi sina thamani sana zaidi ya yule? Je muuzaji anamuona yule bora na wa kuheshimiwa kuliko mimi?

Nilipogundua nawaza hivi, nikajiuliza kwanini ninalinganisha thamani yangu binadamu na kikombe ninachowekewa chai? Kwanini nimekipa kikombe cha chai uzito sana mpaka nahisi anayepewa kikombe cha udongo amethaminiwa sana kuliko mimi ninayepewa kikombe cha plastiki? Na vipi kama muuzaji alikuwa hata hawazi hayo, vipi kama ni vile tu vikombe vilimuishia?

Hapo ndipo nilipoanza kuwaza je kuna namna huwa naangalia vitu fulani na kuwathamini na kuwa heshimu watu kiutofauti kwasababu ya vitu walivyonavyo au wanavyonionesha? Mfano nikikutana na ombaomba, je sitakiwi kumheshimu au kuona ana thamani kama nikikutana na mtu aliyevaa saa ya dhahabu? Nikimuona mtu mwenye gari la gharama sana, je yeye ndio ana thamani sana kuliko mwenye gari la bei ndogo? Je inawezekana kuwa wao huwa wananunua vitu hivyo vya gharama kwasababu ya kuongeza thamani na kuheshimiwa kitofauti na watu wengine?

Pia Soma : Kudharauliana Kutaisha Lini?

Toka lini vyombo vya udongo vilianza kuwa na thamani na vikaonekana ni bora zaidi kuliko vya plastiki wakati vyenyewe vinavunjika kiurahisi? Na kuvipa vitu thamani, mpaka tukawa tunafungwa kiakili kwa namna ambayo nilianza kujishusha thamani kwasababu tu nimepewa kwenye sahani ya plastiki, kunaniathiri vipi kwenye maeneo mengine mbalimbali ya maisha yangu na vile ninavyoiangalia dunia?

Kama wewe ni kama mimi basi umekulia kwenye familia ambayo mzazi anasisitiza kuna vyombo vya wageni na vyenu vya kutumia kila siku, huwa sielewi kwanini vile vya wageni vinakuwaga vizuri zaidi, ni kama nyie wenye nyumba hamstaili kutumia vyombo vizuri? Au ni muhimu kuwapa wageni vile ili wawaone katika jicho la tofauti, je vitu vyote tulivyovipa thamani kwenye maisha yetu ni kwaajili ya maonyesho au ni kweli ni kwaajili yetu?

Labda hii ndio sababu nilijisikia vibaya, kama mteja nilitegemea kikombe cha udongo kwasababu nimezoea wageni wanapewa vizuri na nimekariri kuwa kikombe cha udongo ndio kizuri, cha plastiki sijakipa thamani na kwa kunipa hicho kikombe ni kama hakunithamini. Kwasasa sifikirii haya, ila labda hii ndio sababu.

Eunice

Share Your Thoughts With Me

Translate ¬Ľ