Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maoni

‘Unakuwa kama mwanamke’ sio tusi

Mwanamke sio kitu kibaya zaidi wewe kuwa. 

Kama kuwa mwanamke ni kitu kibaya kuwa au ni tusi, unafikiri sisi wanawake tunajisikiaje kusikia / kuwa hivyo?


Kuna siku nilikuwa kwenye basi nikamsikia dereva anamwambia konda aende ‘kuongea’ na trafiki haraka waondoke baada ya kuwa tulisimamishwa kwa muda. Konda akaenda ‘kuongea’ naye halafu akachukua muda kurudi, dereva akamuita kwa sauti ya hasira na kusema, ‘we nawe unachelewaga sana, jambo la dakika moja tu hilo, unampa tunaondoka unakaa, unakuwa kama mwanamke, tukupe poda na rangi upake?’.

Nikiwa nimekaa upande wa dereva nikajisikia vibaya kusikia vile, ila niliendelea kuwaza na kujiuliza maswali ambayo sikuweza kumuliza dereva msemaji, nilitamani kumuuliza kuwa uanamke labda kwake alimaanisha uvivu? kuwa taratibu? au kwa vile kaongelea poda ni kitu kibaya kupenda urembo? au kitu cha kudharauliwa kupaka rangi kucha? au unapofanya mambo hayo kuna sehemu ya chini kwenye macho ya watu na jamii unayokuwa umeshushwa. Sikupata majibu.

Pia Soma : Kudharauliana kutaisha lini?


Siku hizi nimekuwa nikimsikia mpwa wangu akimwambia dada tunayeishi naye kuwa, ‘wewe mwanamke tu‘. Ni namna anayoiongea hiyo sentensi inayonifanya nielewe anachomaanisha. Mpwa wangu naye ni wa kike, ila tayari kashajua kuwa unaweza mnyamazisha mtu kwa kumwambia hivyo au unaweza kumfanya ajisikie vibaya kwa kumkumbusha jinsia yake au kwa kumwambia kuwa wewe ni kama mwanamke, kwavile mambo ambayo jinsia hiyo inatambulika kwayo au watu kwenye jamii wanavyoifikiria itamfanya tu akose kujiamini na akose jibu.

Pia Soma : Dondoo 10 zitakazokusaidia kuongeza kujiamini


Matusi kwenye jamii yetu yanatukana kwa kutumia sehemu za siri za mwanamke, mimi sijui hata kama nikisema tuache naanzia wapi kuongelea jambo ambalo linaonekana ni sawa kwenye jamii kama hilo. Na wanawake pia tumenyamaza. Nahisi pia tumekubali sehemu ya udhaifu ambayo jinsia yetu inaonekana inayo au imepewa na hivyo tumekubali kutumika kama tusi pale mwanaume anapotaka kumshusha thamani au kumuonesha dharau mwenzie.

Ni dharau hii tuliyonayo kwenye akili zetu muda mwinginge bila kujua au kufikiria inayofanya wanawake nao wajaribu kuonesha kuwa sio wadhaifu, sio wa kudharauliwa, katika kujaribu kujitoa kwenye jinsia yao kutumiwa kama tusi na kitu cha kudharauliwa ndio tunajikuta tuna vita za jinsia.

Ukweli ni kuwa hatuna jinsia moja iliyobora kuliko nyingine, zote zina uhitaji na umuhimu kwenye jamii, zote zinahitajiana, pale mwingine alipo dhaifu mwingine ana nguvu na pale mwingine ana nguvu, mwingine ni dhaifu, tunasaidiana, tunatoshelezana katika upekee wetu, utofauti wetu na ukamilifu wetu.

Kuwa mwanamke sio tusi, kwavile wanawake kwa utofauti wao na upekee wao nao wanavitu wanaleta kwenye dunia, wana mchango chanya na wanawezesha maisha ya jinsia nyingine pia kuwepo na kuendelea kufanikiwa. Labda badala ya kudharauliana kwa lugha za matusi na kuigandamiza jinsia nyingine kimaneno, tungeanza kukubaliana na kuona mchango ambao jinsia nyingine inaleta, tungeheshimiana. Kama unataka kumtukana mtu huwezi kutumia jinsia nzima na kuidhalilisha ili tu umtukane mtu mmoja. Unakua unadharau mchango wa jinsia ile, unasahau umuhimu wake kwako, unasahau kuwa usingekuwepo hapo bila jinsia hiyo.

Labda badala ya kutumia ‘unakuwa mwanamke’ kama tusi, tungewaza ningejisikiaje ningekuwa mimi ni mwanamke? Wanawake waliopo kwenye maisha yangu wanawaza nini au wanajisikiaje ninavyosema haya?

Eunice

One Comment

Share Your Thoughts With Me

Translate »