Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya kila siku,  Self Care

Mambo ya kufanya unapopitia magumu

Labda ulishapitia, unapitia sasa au unaelekea kupitia, mambo magumu huwepo kwenye maisha. Hakuna anayependa kupitia magumu lakini huwa tunayapitia kwa namna moja au nyingine. Kufukuzwa kazi, vifo, kufeli kwenye masomo, kuumwa, ugomvi, kukosa fedha na mambo magumu yoyote ambayo unaweza ukajikuta unayapitia.

Hata kwenye Biblia imeandikwa hatutokuwa na safari isiyokuwa na misukosuko “Nimewaambia mambo haya ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”- Yohana 16:33. Kwahiyo labda tusahau kukosa magumu katika maisha au majaribu kwenye dunia hii, lakini labda tujue jinsi yakuishi wakati tunapitia magumu.

Makala inayoendana na hii : Mungu kwanini mimi ?

Mambo magumu tuliyoyapitia, tunayoyapitia au tutakayoyapitia yasitufanye kumuacha Mungu, kujiuliza kama yupo, kujiua au kufanya maamuzi mabaya katika maisha au maamuzi tutakayoyajutia, kutokana na niliyoyapitia nimejifunza mambo ya kufanya yafuatayo pale ninapopitia magumu, ambayo nawewe unaweza kuyatumia, na yakawa msaada sana unapopitia magumu. Nayo ni:

 1. Jikumbushe mambo ambayo Mungu alikuvusha na ukauona Mkono wake katika hayo- naamini Mungu aliwahi kukutendea mengi sana katika maisha na mpaka ukamshangaa, naamini Mungu alishawahi kukuvusha kwenye jaribu ambalo ulidhani ndo maisha yako yataishia hapo, naamini kuna jambo ambalo Mungu alishalifanya likakuacha mdomo wazi. Nimejifunza hili, nikipitia mambo magumu huwa nakumbuka lile jambo ambalo Mungu alifanya kwangu, na jambo hilo kwangu ni muujiza ambao Mungu alinifanyia, kuna mwaka ambao mama yangu alikuwa akiumwa mwaka mzima, lakini Mungu alimponya akawa mzima tena na yupo hai mpaka leo. Kila nikikumbuka jinsi Mungu alivyofanya kipindi kile naamini Mungu yule yule atafanya katika magumu mengine ninayoyapitia.
 2. Fanya maombi na kufunga pia: ni kweli nimeona nguvu ya maombi, na zaidi nguvu ya kufunga. Unaweza kuomba mwenyewe na nashauri uombe mwenyewe hata kama unasikia ugumu sana, unajua shetani anajua nguvu ya maombi kwahiyo mara nyingi ataepusha wewe kuomba kwa kukupa vitu vingine vya kufanya ili usiombe, lakini nashauri omba lakini pia ukishirikisha watu wengine ukaomba nao itakuwa vizuri. Ukisoma katika kitabu cha Isaya 58 utaona habari za kufunga na nguvu iliyopo kwenye kufunga lakini pia Mathayo 17:21 inatukumbusha juu ya Kufunga na kuomba. Maombi yananguvu sana, kiasi cha Mungu kukuondolea hayo magumu unayoyapitia. Usiache kuomba ukiwa unapitia mazuri, na zaidi usiache kuomba ukiwa unapitia magumu. Mwambie Mungu unayoyapitia, mwambie Baba anayeweza kuyaondoa kwenye maisha yako.
 3. Angalia na ongelea ukubwa wa Mungu: Mara nyingi tunapopitia magumu tunaangalia ukubwa wa tatizo na kuacha kuangalia ukubwa wa Mungu, tunakuwa tunaongelea sana ukubwa wa tatizo na kuacha kuongelea nguvu na ukubwa wa Mungu. Lolote tunalolikuza kwenye ufahamu wetu linakuwa kubwa kwenye maisha yetu, katika kipindi unachopitia mambo magumu angalia sana ukubwa wa Mungu, msifu Yeye na kumwinua katika maisha yako na sio tatizo lako. Tukumbuke Paulo na Sila walipo kuwa wanasifu na sio kuongelea kuhusu kifungo chao na jinsi Mungu alivyojitokeza kwao na kuwaondoa katika kifunge kile.Usiangalie tatizo lako mara zote, na hivyo kwenye ufahamu wako ukamtoa Yeye anayeweza kukuondoa kwenye hilo tatizo, bali mwangalie Yeye sana na kusudi lake kwenye maisha yako. Macho yetu yanaweza kuwa kwenye mambo tunayoyapopitia kwenye maisha au Neno la Mungu na Ukuu wake.
 4. Jikumbushe kusudi la Mungu katika maisha yako: Hivi unajua kwamba siku tutakayo simama mbele za kiti cha enzi, hatutowaza kuhusu tatizo tulilopitia, au miaka miwili ijayo hili kwako litakuwa ni jaribu au tatizo dogo sana ambalo umelipitia? Jikumbushe kwamba leo itapita na kuna mwaka mwingine ambao utakuja na mambo mengine ya kuyapitia, jikumbushe kwamba haya maisha yatapita na hivyo siku nitakayo kuwa mbinguni sito sumbuka wala kukumbuka hili, jikumbushe kuwa na hili nalo litapita.
 5. Tafuta mistari ya Biblia: kama unataka kujua umuhimu wa kusoma Neno la Mungu unaweza kusoma hapa . Lakini kuwa na mstari wa Biblia unaokupa nguvu na kukumbusha ushindi katika kipindi unachokipitia ni jambo zuri sana na linalotia moyo na kukupa faraja. Nimekuwa na tabia ya kuwa na mistari na mara nyingine na uandika kwenye karatasi na kuubandika kwenye ukuta ili kila ninapokuwa nyumbani niuone, au unaweza kuuweka kama wallpaper kwenye simu yako ili kila unapowasha simu uuone. Kuna mistari mbalimbali ambayo imenisaidia ninapopitia woga, matatizo na mambo magumu, naomba nikushirikishe nawe, kama ilivyonifariji mimi ikufariji na wewe pia.
 • Habakuki 1:5-” Angalieni, enyi mlio kati ya mataifa, katazameni, kastaajabuni sana; kwa maana mimi natenda tendo siku zenu, ambalo hamtaliamini hata mkiambiwa”
 • 2 Timotheo 1:7- ” Kwa maana Mungu hakutupa Roho wa kutufanya tuwe waoga, bali alitupa Roho wa kutujalia nguvu, upendo na nidhamu.”
 • Isaya 43:19, 1 Wakorintho 2:9
 • Waefeso 6:10 – “Hatimaye, muwe imara katika Bwana na katika nguvu zake kuu.”
 • Waefeso 4:1-16
 • 1 Wakorintho 10:13- ” Hakuna jaribu lo lote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Na Mungu ni mwaminifu; hata- ruhusu mjaribiwe kupita uwezo wenu. Lakini mnapojaribiwa atawapa na njia ya kutokea ili mweze kustahimili.”

Hiyo ni mistari ambayo hunitia moyo na nimeikariri, na unakuta nasoma tu Biblia na mstari ninaupata unagusa maisha yangu na jambo ninalolipitia, hivyo huwa ninaukariri ili kujikumbusha kila wakati.

Eunice

4 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate »