Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Dondoo za Maisha

Mambo 5 yatakayokusaidia unapotaka kuacha tabia fulani

Hivi karibuni nilijiunga na gym, najua kwa wale wanaopenda mazoezi watashangaa lakini kwangu mimi hakuna uamuzi mgumu niliowahi kuufanya kama huo, kuna mazoezi nilikuwa nafanya mpaka najiuliza hivi kwanini nilijiunga na gym?
Hivi kwanini nimelipia maumivu yangu mwenyewe?
Lakini pia kuna muda nilibidi niache vitu fulani ili nipate matokeo au niende gym, mpaka nikawa naona kama ni shida tu, lakini mimi huwa sipendi kuacha vitu katikati lakini pia nililipia kwa hiyo ilibidi tu nikamalizie hela yangu?
Hakuna kitu kigumu kama ukiwa kwenye safari ya kubadilisha maisha yako, kuacha tabia au kutengeneza tabia mpya ni kazi ngumu kwasababu ya mazingira yanayotuzunguka, kwasababu ya kuzoea hali zetu tulizonazo au tabia zetu au pia kwasababu ni uwekezaji. Kubadilisha maisha ni uwekezaji unaokutaka uwe kipofu kwa mazoea uliyonayo. Mara nyingi tunajua mambo mema ya kuyafanya, tunahamu ya kuyafanya, tunatamani kuwa tunayafanya, lakini kazi inaanzia pale kwenye kuyafanya.
Leo naomba nikuambie vitu ambavyo nimejifunza,ambavyo unaweza kuvifanya unapotaka kubadilisha maisha yako:
Badilisha mazingira
Moja wapo ya vitu vinavyotufanya tushindwe kubadilika ni mazingira, marafiki na vitu vinavyotuzunguka. Mtu anayetaka kuacha bangi akiendelea kukaa na wavuta bangi wenzie kuacha huyu ni historia, mtu anayetaka kuacha pombe akikaa na chupa za pombe kwenye friji, kuacha huyu asahau, lakini pia mtu anayetaka kuachana na boyfriend/ girlfriend ambaye anaona kabisa hawaendi popote na hamfai akiendelea kuwa karibu naye au kumuona, huyu kumuacha ni jambo gumu (ndio maana simu zinasehemu za kublock,mblock kwa muda kwenye kila social media mpaka utakapomtoa moyoni).
Jiandae
Wikiendi hii kuna mtu kaniambia kitu kikubwa sana, “hesabu gharama kwenye maisha”. Mara nyingi tunaamua kubadilisha maisha bila kuhesabu gharama, gharama ya kufika tunakotaka kwenda na kujua kwanini tumeamua kuacha vile tunavyotaka kuviacha, usipoona uzito wa kubadilisha maisha yako hautochukulia kwa uzito sana process, kwahiyo ukipitia jambo dogo tu utarudi katika hali yako ya zamani. Lakini hata ukirudi kwenye hali ya zamani, jikaze uanze tena process ya kubadilisha maisha yako. Usikubali kabisa kushindwa.
Waambie watu wakaribu ili wakufuatilie
Nimeambiwa moja ya mambo yanayowafanya watu warudi nyuma kwenye wokovu ni kukosa watu wa kuwa keep accountable, ukiamua safari mpya na kubwa katika jambo lolote uwe na watu wanaokuwazia mema na wanaotaka kukuona umefanikiwa kwenye jambo lako ambalo umelipanga, watu ambao watakukumbusha kuendelea na mwendo mpya au pia kukutia moyo utakapo shindwa kuendelea na safari yako ya mabadiliko. Mara nyingi ni rahisi kuvunjika moyo ukiwa peke yako kwasababu huwezi kuona matokeo kwa haraka,unahitaji watu. Ndio maana watu wanaotaka kuacha bangi wanapelekwa rehab ili wafuatiliwe kwa ukaribu, tumia marafiki zako wakukeep accountable.
Uwe jasiri na uendelee mbele
Kuna wale watu walioshindwa kwenye hilo lakini pia kuna wale ambao hupenda kuvunja moyo, jitie nguvu umeamua kubadilisha maisha yako, ni kwaajili ya faida yako. Fanya ukijifikiria wewe unavyotaka kuwa. Puuzia unapovunjwa moyo. Usipoona matokeo haraka ,jitie moyo.
Usighairishe
Unapotaka kubadilisha maisha yako unaenda kinyume na ile hali uliyoizoea toka mwanzo, unapopeleka vitu mbele kwamba utavifanya baadae unaufanya mwili urudi kwenye comfort yake, utapata shida kujitia nguvu kuendelea kufanya tena yale. Kama ulipanga utakuwa unasoma vitabu muda fulani kila siku, ukipeleka mbele huo muda kwa wiki, itakupa shida tena kuizoea hiyo tabia.
Unapotaka kubadilisha maisha yako katika jambo lolote lile, iwe tabia au jambo kubwa zaidi ya hilo, jitie moyo, usikubali kubaki vile vile toka kizazi hadi kizazi, unaweza ukabadilisha vitu na ukafanikiwa katika hayo mabadiliko. Nikutie moyo, sio rahisi kubadilisha maisha yako kwasababu mazoea ni magumu sana kuyaacha lakini unaweza.
Usikubali kufa kabla ya kuona yale makubwa ambayo ungeyafanya.
Eunice

3 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป