Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Imani,  Maisha ya kila siku

Unapoumizwa na watu unaosali nao…

Nilitaka kichwa kiwe Unapoumizwa na wakristo ama Unapoumizwa na watu wa kanisani au Unaposalitiwa na waamini wenzio.


Sijui ni mimi tu au na wengine mnahili, ila nikisikia mtu anasali huwa nakuwa na mategemeo makubwa sana na tabia yake, kwamba anaweza kuwa na matendo mema lakini pia huwa na namwamini kwa uharaka kwasababu naamini anamuogopa Mungu hawezi kunisaliti, kuniumiza au kunidanganya.


Nilipokuwa kidato cha sita, shule ya sekondari ya Tambaza nilikuwa na wazo la kipindi cha redio kwaajili ya vijana. Nakumbuka nilikuwa siwezi hata kuandika vizuri wazo langu ila nililiandika tu shagharabaghara kwenye karatasi halafu nikamtafuta mtangazaji mmoja wa redio moja kubwa ya Kikristo hapa Tanzania nikamwambia nina wazo, akaniahidi kunisikiliza na kulipeleka majuu hivyo tukapanga siku tukutane nimpe karatasi langu maana nilikuwa siwezi kuandika hata maombi yangu hayo vizuri.

Siku ikafika tukakutana, nikampa.

Tokea hapo akawa hapokei simu, hajibu ujumbe wala Facebook pia hajibu.

Nilikuja kuona wazo langu likitumika kama kipindi na bado mpaka sasa ni kipindi kizuri tu cha dini kwenye tv fulani hapa nchini.

Jamaa namjua ni mkristo.

Jamaa namjua anaongoza kipindi cha dini.

Nilimuamini.


Nilipokuwa sekondari Jangwani nikiwa na miaka 13, niliota ndoto mbaya sana usiku mmoja. Nikamsimulia mama, mama akamwambia mjomba wangu wa hiari tuliyekuwa tunaishi naye, mjomba akasema ataniombea. Lakini alikuwa ananifanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia, vitendo vya kingono kwa jina la kuniombea.

Najua ni mkristo.

Tena alikuwa akiomba kwa sauti sana. Kutufafsiria mistari ya Biblia pamoja na ‘hekima yake ya kiMungu’ ndio vitu vilivyonifanya nimuamini.


Kuna jamaa ambaye alikuwa anasali na mama, ambaye alituibia milioni moja na gitaa langu. Walikubaliana kufanya biashara alivyopata tu hizo hela akapotea, mimi nilimuazima gitaa sijalipata mpaka leo. Walikutana kanisani. Walikuwa wanaitana mama na mwana. Mpendwa. Mtumishi.

Hivi karibuni watu wengi wanatumia dini kuiba hawana tena woga.


Kuna mambo mengi tu makubwa na madogo ambayo yamewahi kunitokea kwenye maisha, kanisani na yakanifanye nijiulize maswali mengi, niumie, imani itikisike, nijilaumu kwa kuamini watu na nijiulize kama huyu aliyenifanyia haya ni kweli mwamini mwenzangu au sio.

Najua umewahi kuumizwa iwe vikubwa au vidogo ila ulishawahi kuumizwa na mtu wa kanisani kwako, au mtu unayejua kabisa anaamini na anasali mpaka ukajiuliza, ‘ hivi huyu mtu mkristo kweli mbona anafanya matendo haya jamani?’

Ukiumizwa na mkristo mwenzio inauma sana kwasababu ni sawa na kama umeumizwa na mtu wa nyumbani kwako, ukweli ni kuwa ni kweli huyo mtu ni wa nyumbani kwako, mnatoka nyumba moja kiroho.

Kama umeshawahi kupitia hilo ningependa ujue kuwa hauko peke yako, sehemu yoyote ambayo inawatu wengi lazima kuna kukwazana, kuumizana, kusalitiana nk. Hata vikombe hugongana. Lakini kwasababu hao unaokutana nao ni wakristo muda mwingi huwa tunaondoa hayo mawazo ya kugongana na tunaamini tutaishi tu kwa furaha kwavile tuna nia mamoja.

Na hicho ndicho kitu nilichojifunza.

Kuona watu kama watu kwanza

Hata Yesu alijua kuwa Petro atamkana. Muda mwingine watu wana tabia zao wanazificha ndani ya Yesu au wanatabia zao wanaona watatubu baadae, lakini pia bado tupo duniani tamaa za dunia na mambo mengine yanaweza kuchangia hata mkristo kufanya maamuzi yanayokuathiri wewe pia.

Natamani niseme kuna namna ambayo unaweza kupona hivi vidonda lakini namna ninayoijua ni kulia na kuumia. Wakristo wengi hata tupitie magumu vipi hatukai chini kulilia yale magumu maana tunahisi kwamba tunamdhalilisha au tunamshusha nguvu Yesu, lakini hata Yesu alilia. Kama umeumia lia, kusalitiwa kunauma, lia, tafuta mtu mkae naye na uongee yale ya moyoni kuliko kuigiza amani.

Unaweza pia kumuita yeye pamoja na kiongozi mmoja muongee. Hii inaweza kuwa njia nzuri ya kutafuta amani, au aombe msamaha lakini kama alikuwa mwizi kama aliyeniibia gitaa basi ataondoka kanisani utabaki tu wewe ukilia na majonzi yako.

Lakini pia muda mwingine wengine huamua hata kuhama kanisa hiyo pia husaidia, wengine huacha kwenda kanisani kwa muda hiyo pia inaweza kukusaidia kupona, lakini tafuta kupona na kupata amani ya kweli.

Kitu ambacho ningependa kumalizia na kukitilia mkazo kwa leo ni kuwa kama kanisa tuwe sehemu ya makimbilio, tutengeneze mazingira ambayo watu wanaponywa na sio kuumizwa na hata ikitokea mtu anaumizwa kwa vile sisi ni mwili mmoja tuwe wepesi kumsapoti na kutafuta uponyaji wa kweli kwaajili yake badala ya kuigiza kuwa tuna amani wakati hatuna au kumtenga zaidi aliyeumizwa.

Je huwa tunawafuatilia wapendwa wenzetu?

Je wakiumizwa tunawasema tu chinichini na tukiwaona tunajifanya hatujui kinachoendelea?

Je kanisa unalosali unajisikia kusapotiwa ukipitia magumu?

Unajisikia huru kushea pale unapoumizwa?

Sisi ni familia, sisi ni mwili mmoja, tuishi kama hilo jambo ni kweli. Mmoja wetu akiumia, wote tunaumia. Lakini pia kama unajipenda, jitahidi usimuumize mwenzako, maana hakuna anayeuumiza mwili wake kama anaupenda.

Eunice


Pia unaweza kusoma : Church Wounds and My Trust Issues

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป