Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Maisha ya Chuo,  Maisha ya kila siku

Kwa wanafunzi wa kike wanaotamani kuwa viongozi vyuoni

(Tembelea maishayachuo.com kupata makala, dondoo na msaada kuhusu chuo kutoka kwa waliomaliza vyuo)

—-

Sikumbuki kama kuna kipindi niliwahi kuwa kiongozi huko nyuma, zaidi ya kuwa mjumbe wa kwaya??

Nahisi naweza kuigusa jamii kivingine lakini mimi ni wale tunaoamini kuwa kuna watu wamezaliwa kufanya siasa, ingawa najua siasa inagusa maisha yetu katika kila nyanja.

Ila nilipokuwa chuo kuna muda nilitamani kuwa kiongozi, kwasababu ya uchache wa viongozi wa kike.

Nilitaka niwe kiongozi ili tu kuwakilisha jinsia, huwa sijisikii vizuri sehemu ambapo wanawake hatuchukui nafasi au kuwa mstari wa mbele, kwahiyo hiyo ndio ingekuwa sababu pekee nataka kuwa kiongozi tena nilitaka nigombee uraisi kwasababu wasichana wengi walikuwa wanagombea vyeo vingine na kulikuwa na mmoja tu aliyekuwa anagombea umakamu wa raisi.

Inawezekana hiyo isiwe sababu nzuri ya kugombea uraisi na ndio maana sikugombea, ila wewe inawezekana uongozi upo kwenye damu yako, naomba niongee na wewe leo.

Mdada aliyekuwa anagombea umakamu wa raisi alipata ushirikiano wa watu, alifanya kampeni na alisimamia msimamo wake na sera zake.

Hakushinda ila alinifundisha mengi sana kuhusu kujiamini, kuwa mwanamke na kuwa mwanasiasa.

Nilipenda kujiamini kwake.

Na ndio kitu ninachopenda kukuambia leo, jiamini, una uwezo wa kuwa kiongozi, na haijalishi jinsia yako na tena tunataka watu wa jinsia yako wawe viongozi kwa vile wewe unaelewa shida za jinsia yako kuliko mwanaume anavyoelewa, lakini pia kwasababu wewe unauwezo, akili na nguvu za kuwa kiongozi kama jinsia ya kiume ilivyokuwa na uwezo huo.

Usijishushe, usiogope watu watakuonaje au watakufikiriaje, unahitajika na unastahili kuwa kiongozi pia. ‘You belong here’, wewe pia unaweza kuwa kiongozi.

Niliumizwa sana na watu walivyokuwa wanamfanyia kwenye kampeni yake.

Kuna wasichana walikuwa wanamuonea wivu na wengine walimcheka. Sijui kwanini walikuwa hawampi ushirikiano. Lakini kuna wengine walimpa ushirikiano.

Niliumizwa na mfumo dume ambao wanafunzi wengi wa kiume walikuwa nao, na labda ndio maana wanafunzi wa kike waliukubali na kutotaka kushirikiana naye.

Kuna wengine walikuwa wanamwambia mtoto wa kike hawezi kuwa kiongozi, kuna wengine walikuwa wanaongea maneno yaliyokuwa yanamshushia kujiamini, kama vile, ‘tunajua una mimba’, na wengine walikuwa wanamhukumu kwa mavazi na staili anayovaa.

Vitu ambavyo hawakuwa wanavisema kwa wagombea wa kiume.

Kupitia yote hayo na kesho kusimama kusema sera zako inahitaji kujiamini, kujua mapungufu ya jamii tuliyopo na jinsi tamaduni yetu ilivyoathiri vile tunavyoiona dunia na tunavyojiona, na kuamka tena kufuata kile moyo wako unakuambia hata kama unapitia vikwazo hivyo.

Nikuambie tu kwa mfano niliouona kwake, utapitia vikwazo.

Unaweza usishinde pia, ila haimaanishi usiwe mshindani, tengeneza sera, tafuta sehemu ya chuo unayotamani kuibadilisha, waelezee watu waelewe unachotamani kufanya, hauhitajwi kupendwa na kila mtu ili upite, ila unatakiwa kuwa na sera na haiba ya uongozi.

Hauwezi jua kwa wewe kusimama na kugombea ukawagusa wanafunzi wa kike wengine wakagombea na kushinda baada yako, ukaja kuona mabadiliko unayotamani kuyaona kwenye uongozi wenu.

Au ukaishia kuandikwa kama ninavyomwandika mdada aliyegombea nilipokuwa chuo.

Lakini chukua hatua, usiache vile jamii ilivyokuambia kuhusu uongozi ikufanye uache kufanya yale moyo wako yanapenda kufanya, unaweza kuwa kiongozi, unafaa kuwa kiongozi.

Ukiwa kiongozi chuo inaweza kukuongezea CV hata ukimaliza chuo, viongozi wengi sehemu mbalimbali pia walikuwa viongozi chuoni.

Ichukulie kama sehemu ya majaribio, ukiacha kuingia kwenye kampeni hapo utaweza jimboni kama anavyofanya Halima Mdee? Fanya majaribio ya kuongea kwa hao watu 4000, kuchukiwa na hao watu 4000, kupewa maoni na kutendea kazi sera zako ulizoziahidi kwa watu 4000.

Inabidi uanze mahali, anza hapo ulipo.

Na ukishinda, timiza wajibu na sera ulizoahidi. Kumbuka unawajibu wa kusaidia wanafunzi waliokuchagua lakini pia na kuinua wanafunzi wengine wa kike kwenye nafasi za uongozi.

Eunice

(Kupata dondoo hizi na nyingine nyingi, pata kitabu cha Your Guide to University Life, kinachokusaidia kupata majibu ya maswali na kila jambo unaloweza kupitia kama mwanachuo, kwenye kitabu hiki utapata ushauri kutoka kwa waliomalia chuo kuhusiana na maswala ya pesa na biashara, urafiki, supp, carry, disco, mahusiano, migomo, mambo ya kufanya ukipata skendo chuo, jinsi ya kudili na walimu wasumbufu, ushauri wa mitindo, jinsi ya kujiandaa na maisha ya mtaani ukiwa chuo na mada nyingine kedekede, kukipata kitabu hicho kwa Tsh 5000/= tu, bonyeza hapa)

Share Your Thoughts With Me

Translate ยป