Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Dondoo za Maisha,  Self Care

Kwa anayejisikia upweke sikukuu hii ya Christmas..

Inaweza ikawa ni kwasababu mbalimbali ukawa unajisikia mpweke leo.

-Inaweza ikawa ni kwasababu uko mbali na familia..

-Umetengwa na watu..

-Umeachwa..

-Unatamani kuwa nyumbani ila hauwezi kwasababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wako..

Au sababu yoyote inayokufanya ujisikie mpweke na sijaitaja,natamani ujue kuwa naelewa.

Nimeshawahi kujisikia mpweke kwenye Christmas, sikukuu ya wapendanao hadi kwenye kumbukumbu ya siku yangu ya kuzaliwa.

Natamani kwanza ujue hauko peke yako.

Na Wewe sio wa Kwanza kujisikia mpweke kwenye sikukuu hii.

Upweke unakufanya uone sikukuu hii Ni mbaya na ndefu Sana. Na unaumia na kupata wivu unapowaona wengine wanasherehekea.

Katika miaka minne yote nilipokuwa chuo, nilitamani Sana kurudi nyumbani sikukuu, ila sikuweza, nilikuwa najisikia vibaya Sana na mpweke.

Mwaka Jana, ndio mwaka ambao nilitarajia nitakuwa nyumbani pia sikuwepo, nilikuwa Malawi kwa watu ambao nilikuwa mgeni kwao lakini pia nilikuwa naona marafiki zangu mitandaoni wanavyofurahi na familia zao wakati Mimi nimesafiri siko na yangu.


Nilikuwa mpweke.

Nilijawa na wivu, uchungu, hasira na mawazo ya jinsi ambavyo ningekuwa na furaha Kama ningekuwa nyumbani.

Na hayo mawazo yaliniharibia sikukuu, nilishindwa kufurahia na wale watu nilionao, kwani hauwezi kuishi kipindi Fulani Cha maisha Mara mbili.

Kwa anayejisikia mpweke sikukuu hii, natamani ujue kuwa inawezekana kabisa hautojisikia tena hali hiyo sikukuu ijayo, labda utakuwa sehemu tofauti kabisa kimaisha mwakani.

Lakini pia hivi Ni vitu vichache vilivyonisaidia nilipokuwa mpweke:

  • Kuacha kuwaza jinsi vile maisha yangekuwa Kama nisingekuwa kwenye Hali hii ya upweke – hili linaumiza tu, kwasababu unawaza jinsi vile maisha yangekuwa badala ya kuishi hivi Sasa yalivyo.

  • Kufanya Jambo ninalolipenda kwaajili yangu mwenyewe – kwavile Ni sikukuu jifurahishe. Mimi huwa napenda kula keki ya chocolate inayoitwa black forest, ndio Jambo linalonifurahisha. Na Wewe pia fanya Jambo Lile ambalo ukijifanyia huwa unasikia furaha, Kama Ni kwenda kula sehemu unayoipenda au lolote Lile, jifanyie mwenyewe. Japokuwa unajisikia mpweke, lakini bado una Haki ya kuwa na furaha.
  • Ukikaribishwa kubali mwaliko – Ni rahisi Sana ukiwa mpweke, kujihisi kuwa Wewe Ni mzigo.. na hivyo hata watu wakikualika unajihisi unaenda kuwaongezea mzigo nyumbani kwao. Hapana, Hilo si kweli, watu wakikualika ina maana wanapenda kuwa na Wewe kwao, nenda, kafurahi nao.
  • Kama Kuna kitu kinakufanya ujisikie vibaya, usikifanye – mfano; Kama umeachwa, sio wazo zuri kuangalia filamu za mapenzi. Ni heri uangalie vichekesho. Kama unawaonea wivu marafiki zako na familia zao, sio vizuri kuangalia mitandaoni wanavyofurahia na maisha yao.
  • Fanya Jambo jema kwa unayeona hawezi kufurahia sikukuu – Kuna furaha unaweza ukaipata kwa kumfanyia Jambo jema mwingine, ukimpa omba omba chakula ulichopika, ukapiga naye stori unaweza ukaondoa upweke kwa kuwa unaongea na mtu, lakini pia Kama una rafiki unajua naye Yuko peke yake, muite mkae wote, muangalie filamu, mle, msheherekee pamoja. Kupata mtu wa kuongea naye kunapunguza upweke.

  • Kuwapigia familia au watu uwapendao uliowakumbuka – Kama Ni familia unaweza kuwapigia na kufurahia nao japo kidogo kwenye simu, hii inapunguza upweke kidogo kwani unajisikia kama upo nao kidogo.


Kwa anayejisikia mpweke sikukuu hii, hauko peke yako, na Kama unataka mtu wa kuongea naye kuhusu unavyojisikia nitumie ujumbe mfupi hapa.

Eunice

Translate ยป