Pata majibu ya maswali yote uliyonayo kuhusu maisha ya chuo na changamoto zake

Being African,  Maisha ya kila siku,  Maoni

Kwanini waAfrika tunatabia ya kujidharau?

Kuna siku nilikuwa kwa fundi wa laptop, akaja fundi mwingine na mteja wake, wakachomeka laptop yao halafu ilipowaka, mteja akasema, ‘mzungu huyo’. Fundi akamjibu, ‘mzungu huyo baba, hakosei’. Mteja akamwambia, ‘mzungu ana akili’. Wakacheka. Mteja akaondoka na ile laptop wakaenda kuelewana kwenye ofisi ya huyo fundi.


‘mzungu mtu mbaya aisee’
‘mzungu yuko vizuri’
‘mzungu ana akili’
Ni maneno ambayo tunayasema sana mtaani hasa kwa vile vifaa vingi tunavyovitumia vinavyoonekana kama vimeendelea kiteknolojia vinaonekana kutengenezwa na wazungu, hivyo kwa kuona hayo tunaona ametupita, tunahisi ametupita pia kiakili.

Katika somo la historia ambapo tumesoma vitu vyote vimegunduliwa na wazungu ni rahisi sana kuona hakuna mtu ambaye sio mzungu anayeweza kufanya chochote kikubwa, kizuri na cha tofauti au cha maendeleo kama sio mzungu.

Hii imetufanya kujidharau. Hii imetufanya kujiona wa chini, na ndio maana tumefikia hatua ya kusema maneno hayo bila kufikiria mara mbili maana tunayaamini.

Hii pia inawezekana ni madhara ya ukoloni kwa vile wale waliokuwa na rangi nyeupe au wanakaribiana sana na weupe walikuwa wanaonekana kama daraja la juu wakifurahia matokeo ya ngozi zao kuwa karibu na weupe. Hili na maneno wazungu waliyosema na kuandika kuhusu watu weusi ili kututawala yametufanya kuamini kuwa, kuwa mwaAfrika ni jambo la chini, la kudharauliwa. Kuwa hauwezi chochote kwasababu ya rangi ya ngozi yako.

Ukweli ni kuwa katika historia watu weusi ndio walikuwa wa kwanza kugundua Marekani.
Watu weusi walisafiri sehemu nyingi sana na nchi nyingi sana. Kwa vile malighafi nyingi zinapatikana Afrika, sisi ndio tulikuwa wa kwanza kuzigundua na kuzitumia.
Kihistoria watu weusi ndio watu wa kwanza kuwepo duniani, nchi kama Benin, nchi ya Afrika ndio ilikuwa ya kwanza kuendelea, ukisoma historia kabla ya ukoloni kuna miji ambayo wazungu waliona imeendelea sana ikabidi waichome, walitoa maendeleo huko na kuyapeleka kwao.

Kuna historia kuwa Tanzania na Uganda walianza kufanyisha oparesheni ya wamama wenye mimba mpaka mzungu mwenyewe akawa amekuja kujifunza yote haya ni kabla ya ukoloni.

Ukisoma historia tuligundua matumizi ya chuma nk.

Ukoloni ndio umechelewesha maendeleo, umetudumaza kuamini misaada na kuwa hatuwezi, na kutufanya tujione kuwa wachini na historia ambayo tunafundishwa ni ile ambayo haituambii tulikuwaje miaka kabla ya ukoloni, tunaanzia kwenye ukoloni, uhuru halafu tunaendelea na hali ya sasa. Historia yenyewe tunayosoma shule haituambii vyote, kuna vitu vingi vilivyotokea kabla ya ukoloni, historia yetu ni zaidi ya tu wazungu kututawala.

Yote haya naandika ili ujue kuwa wewe sio wa chini, mzungu hana akili kukuzidi, vitu vyote havijagunduliwa na wazungu lakini pia kusema maneno kama hayo ni kama kuwaabudu na kuwaheshimisha kuwa wakubwa juu yako na ndio maana watu wengi wanaogopa wazungu, au wanahisi kila wanachofanya ni sawa hakitakiwi kuulizwa maswali maana wako sahihi au wanahisi wanajua kila kitu au wanahisi wao ndio mwanzo na mwisho wa ishu zote kitu ambacho inabidi tukibadilishe, wewe pia ni wa pekee, unaakili, na hauko chini ya mtu yoyote, mzungu pia anaweza kuwa hana akili kama vile mchina anavyoweza kuwa hana akili, na wewe pia unaweza ukagundua vitu, una ubunifu huo. Ukijidharau wewe, usishangae wanapokudharau na kukunyanyapaa.

Badilisha vile unavyojiona. Badilisha vile unavyomuona mzungu au mtu mwenye ngozi nyeupe.

Kimtokacho mtu ndicho kimjazacho, maneno kama haya yanamaanisha moyoni mwako umejaa kuamini ukuu na ubora wa wazungu na udhaifu wa mtu ambaye sie mzungu. Hiyo inachangia jinsi unavyowafikiria watu weusi, mambo ambayo watu weusi wanaweza kufanya, vile unavyojifikiria wewe, mambo unayoweza kuyafanya, hii inachangia kujidharau na kuwadharau waAfrika wenzio, kwamba hakuna jema linaloweza kutokea toka kwenu.

Badilisha vile unavyojiona, utabadilisha vile unavyozungumza pia. Utabadilisha yale unayoamini unaweza kuyafanya pia, wewe pia unaakili kama mtu mwenye rangi yoyote duniani, unaweza kuleta masuluhisho duniani kwa vile una akili pia.

Eunice


Niliiposti hii Instagram, nikaona nishee na hapa kwenye blogu.

Pia soma : It’s time for Africans to change the way they see themselves

2 Comments

Share Your Thoughts With Me

Translate »